MBUNGE KAMONGA AIBUA TUMAINI JIPYA KWA WAKAZI WA WILAYA YA LUDEWA - MBINGA, WANANCHI WAWASILISHA KILIO CHAO. | Tarimo Blog

Na. Shukrani Kawogo, Njombe.

Wakazi wa wilaya ya Ludewa mkoani Njombe na wakazi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wamefurahishwa kwa kutembelewa na mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga katikati eneo la mpaka wa wilaya hizo na kudai kuwa nu mbunge wa kwanza kufika eneo hilo na kusikiliza shida zao.

Wananchi hao wamekuwa na kilio cha muda mrefu kuhusu ujenzi wa daraja katika mto Ruhuhu unaotenganisha wilaya hizo ili waweze kusafiri kwa urahisi ikiwemo kujenga ushirikiano wa kiuchumi baina yao.

Wakiwasilisha kilio hicho baada ya mbunge huyo kuwasili katika eneo hilo la mto akiwa ameongozana na baadhi ya madiwani kutoka kata ya Ibumi Edward Haule, diwani wa Milo Robert Njavike, diwani wa Luilo Matei Kongo pamoja na diwani wa Mawengi Leodga Mpambalyoto na kukutana na wananchi wa pande zote mbili.

Wakizungumza kwa masikitiko wananchi hao wamedai kuwa wamekuwa wakipata changamoto katika kusafirisha bidhaa zao kwenda Ludewa na Mbinga kwani hutumia usafiri wa mtumbwi kitu ambacho hupelekea baadhi yao kutumbukia kwenye maji na kuliwa na mamba hivyo wanatumai kufika kwa mbunge huyo ni njia mojawapo ya kusikika kwa kilio chao.

Sylvester Majaliwa ni mkazi wa kijiji cha Kingole kilichopo katika kata ya Litumbandyosi wilayani Mbinga amesema kuwa kutokuwepo kwa daraja kunawakosesha fursa nyingi za kiuchumi kwani kwa sasa wanalazimika kufuata bidhaa za chakula kama maharage katika wilaya ya Songea wakati wangeweza kuyapata kwa jirani zao wa kata ya Ibumi iliyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe.

Ameongeza kuwa katika daraja hilo pia litakuwa msaada mkubwa hata miradi ya Liganga na mchuchuma itakapoanza kwani itarahisisha watu kutumia njia tofauti tofauti za usafirishaaji bidhaa hizo sambamba na kupata uwekezaji zaidi katika uchimbaji manidi kwakuwa maaneo hayo yanasemekana kuwa na madini ya aina nyingi.

Naye Patrick Mwinuka ambaye ni mkazi wa kata ya Ibumi wilayani Ludewa amempongeza mbunge huyo kwa kufika katika eneo hilo la mto kwani wabunge wengi waliopita hawakuwahi kufika na kuwasikiliza kero yao hiyo.

"Wewe ni mbunge wa kipekee sana! na tunaimani kubwa sana na wewe kwa kitendo cha kufika na kutusikiliza tunaamini utaenda kutupambania serikalini ili tupate daraja kwani daraja hili likijengwa litakuwa na manufaa makubwa sana kwetu na wenzetu wa Mbinga", alisema Mwinuka.

Aidha kwa upande wa diwani wa Ibumi Edward Haule amesema wananchi wake wameonyesha nia ya dhati ya kuhitaji daraja hilo kwa kutumia nguvu zao kuchimba barabara inayotoka Ibumi hadi kufika mtoni hapo yenye urefu wa km. 20 kwa kutumia majembe ya mkono ambayo waliichimba kwa kipindi cha miaka minne.

Amesema endapo daraja hilo litakamilika litaokoa uhai wa wananchi wake sambamba na kukua kiuchumi kwani wananchi hao wamekuwa wakisafirisha mazao yao kwa kutumia mtumbwi kitu ambacho kimepoteza wananchi wengi kwenye maji akiwemo mtendaji wa kijiji aliyetumbukia hivi karibuni.

Prisca Haule ni diwani wa kata ya Litumbandyosi iliyopo wilayani Mbinga amesema wananchi wa wilaya hiyo pamoja na mbunge wao wanahitaji sana daraja hilo hivyo kwa kushirikiana kwa pamoja wanaamini wataweza kukamilisha ujenzi huo ambao utakuwa msaada mkubwa kwa wananchi hao.

Hata hivyo kwa upande wa mbunge wa jimbo la Ludewa amewapongeza wananchi wa Ibumi kwa kujitoa kuchimba barabara hiyo kwa mikono huku akiwahabarisha kuwa serikali tayari imetenga kiasi cha shilingi milioni 200 kwaajili ya kutengeneza barabara hiyo.

" Serikali yetu inathamini sana mchango wa wananchi katika maendeleo hivyo nguvu mlizotumia kuchimba barabara hii haziwezi kupotea bure na ndiomaana serikali imeleta fedha hizi ili kuunga mkono juhudi mlizozianzisha", Alisema Kamonga.

Ameongeza kuwa kwa kushirikiana na mbunge wa jimbo la Mbinga watahakukisha wanapeleka andiko la ujenzi wa daraja hilo serikalini ili waweze kupata fedha za ujenzi wa daraja hilo.

Kwa mujibu wa mhandisi kutoka wilaya ya Ludewa James Gowele amesema daraja hilo linahitaji nguzo nne zenye urefu wa mita 21 ambazo zitawekwa kwa umbali wa mita 20 kutoka moja kwenda nyingine.

Ameongeza kuwa mpaka sasa tayari wamekwisha andaa michoro ya muundo wa daraja na watafanya makisio ya gharama zake ili kuweza kutafuta fedha za kukamilisha ujenzi huo.

Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (aliyevaa kofia) akiwa kwenye mtumbwi ambao hutumika kusafirishia wananchi wa wilaya ya Ludewa na Mbinga pamoja na bidhaa zao.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kulia) akiongea na wananchi wa kijiji cha Masimavalafu kilichopo katika kata ya Ibumi ambao walimsubiri mbunge huyo na kumsimamisha mpaka nyakati za usiku alipokuwa akirejea kutoka eneo la mpaka wa Ludewa na Mbinga kwa lengo la kumsalimia
Baadhi ya wananchi wa kata ya Ibumi na Litumbandyosi wakiwa wamemzunguka mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga wakati wakiangalia eneo litakalofanyika ujenzi wa daraja.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga pamoja na diwani wa Ibumi Edward Haule wakiwa katikati kijiji cha Masimavalafu baada ya kusimamishwa na wananchi wa kijiji hicho huku wakiwa na vumbi mwilini kutokana na umbali wa eneo walilotoka na kutumia usafiri wa pikipiki
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (aliyevaa kofia) akiwa ameongozana na baadhi ya wananchi na madiwani wakitokea eneo la mto ambalo linatakiwa kujengwa daraja.
Baadhi ya viongozi kutoka wilaya ya Ludewa kutoka kushoto ni diwani wa kata ya Ibumi Edward Haule, mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga, mhandisi wa wilaya ya Ludewa James Gowele, diwani wa kata ya Luilo Mathei Kongo, diwani wa kata ya Milo Robert Njavike na diwani wa kata ya Mawengi Leodga Mpambalyoto.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kulia) akizungumza na wananchi wa kata ya Ibumi na Litumbandyosi (hawapo pichani) baada ya kukutana nao katika eneo la mto Ruhuhu. Kushoto ni diwani wa kata ya Ibumi Edward Haule na diwani wa kata ya Litumbandyosi prisca Haule.
 
Baadhi ya viongozi pamoja na wananchi wakitembea pembezoni mwa mto kuelekea eneo linalotakiwa kuwekwa daraja
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2