WANANCHI WA MADABA KUNUFAIKA NA SHAMBA LA MITI WINO | Tarimo Blog


Na Happiness Shayo –Madaba- Songea

Wananchi wa Halmashauri ya Mabada Mkoani Ruvuma hususan katika vijiji vya Wino, Igawisenga, Lilondo, Mkongotema, Lutikila, Magingo, Maweso na Ifinga wataendelea kunufaika kiuchumi kutokana na uzalishaji wa miti katika Shamba la Miti Wino linalomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) katika mkutano na wananchi wa vijiji vinavyolizunguka shamba hilo uliofanyika katika ofisi ya TFS, Madaba-Songea.

“Serikali kwa kutambua mchango wenu katika kusaidia uhifadhi wa shamba hili, hatutasita kuwaletea maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa, vituo vya afya na ujenzi wa mabweni kwenye shule za sekondari ”amesema Mhe. Masanja.

Ameongeza kuwa kupitia shamba hilo wanavijiji hao watanufaika na ajira za muda mfupi na mrefu zinazotokana na kuisaidia TFS kupanda miti, kusafisha shamba kwa kufyeka na kufanya palizi ya shamba la miti Wino.

Mhe. Masanja ameweka bayana kuwa Serikali itaboresha miundombinu ya maeneo yenye umuhimu sana ya vijiji hivyo katika mwaka huu wa fedha kwa kushirikiana wananchi hao ili maendeleo ya Madaba yasonge mbele.

Aidha, Mhe. Masanja ameahidi kutatua changamoto ya kitalu cha uwindaji cha Wembele ambacho kimesitisha kutoa gawio kwa vijiji vilivyo katika eneo hilo na kuahidi kuhakikisha fedha za uwindaji wa kitalii zinazopatikana ziwanufaishe wananchi hao.

Kuhusu changamoto ya moto wa msituni unaotokea katika shamba hilo, Mhe. Masanja ameelekeza watendaji wa vijiji, kata na madiwani wa eneo hilo kuelimisha wananchi wao kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa kwa uongozi wa shamba wanapotaka kusafisha mashamba yao ili kuepuka moto pori.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Wino, Hezron Mwageni ametoa ushuhuda wa kuwepo kwa shamba la miti Wino kwamba limesaidia kujenga mradi wa maji katika kijiji cha Ifingo.

Pia, memshukuru Msimamizi wa shamba hilo kwa kuendelea kutoa miche ya miti bure kwa wanavijiji wa eneo hilo.

“Shamba hili la miti Wino kupitia TFS limekuwa likitupatia  miche ya miti kwa ajili ya kupanda kwenye mashamba yetu katika vijiji vya Wino, Igawisenga, Lilondo, Mkongotema na hili ni jambo la heri sana kwa sababu hii linawafanya wananchi wawe walinzi katika mashamba ya miti”ameongeza Bw. Mwageni.

Ameelezea kuwa TFS imekuwa msaada mkubwa kwa kusaidia katika ujenzi wa majengo mbalimbali ya wanavijiji hao ikiwa ni pamoja na ujenzi wa makanisa , shule za sekondari na shule za msingi.

Awali akiwasilisha taarifa ya shamba hilo, Mhifadhi wa Shamba la Miti Wino,  Lucas Manyonyi amesema shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 39,000 limefanikiwa kujenga mradi wa maji mtiririko uliogharimu shilingi milioni 482  katika kijiji cha Mkongotema.

Amesema mafanikio mengine yaliyopatikana ni kutoa ajira za muda mrefu na mfupi kwa wanavijiji takribani 4000 kila mwaka katika shamba la miti Wino.

Bw. Manyoni amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kutokana na uzalishaji wa miti katika shamba hilo viwanda vingi vya kuchakata mazao ya misitu vitasimikwa katika maeneo ya Halmashauri ya Madaba.

Mkutano huo wa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja umehudhuriwa na wananchi wa Halmashauri ya Madaba, Watendaji wa Vijiji, Madiwani ,Watendaji na  baadhi ya watumishi wa TFS.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) kushoto akimsikiliza Mhifadhi wa Shamba la Miti Wino, Lucas Manyonyi (katikati) akitoa maelezo kuhusu historia ya shamba hilo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua shamba hilo lililopo Halmashauri ya Madaba,  Mkoani Ruvuma leo. Kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Songea, Pendo Ndumbaro.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (kushoto) akimsikiliza Mhifadhi wa Shamba la Miti Wino, Lucas Manyonyi (kulia) akitoa maelezo kuhusu historia ya shamba hilo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua shamba hilo lililopo Halmashauri ya Madaba,  Mkoani Ruvuma leo. Wengine ni  Mkuu wa Kanda ya Kusini wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Manyisye Mpokigwe (katikati), Katibu Tawala wa Wilaya ya Songea, Pendo Ndumbaro (wa tatu kulia) Mwenyekiti wa Halmashauri ya Madaba Teofanes Mlelwa (wa pili kushoto) na Diwani wa Halmashauri ya Madaba (wa pili kulia).
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Madaba (hawapo pichani) kuhusu jitihada za Serikali za kuhakikisha Shamba la Miti Wino linalomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) linanufaisha wananchi, katika ofisi za TFS, Halmashauri ya Madaba-Songea leo. Kulia ni Mhifadhi wa Shamba la Miti Wino, Lucas Manyonyi.
Baadhi ya Wananchi wa Halmashauri ya Madaba wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)(hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi katika Shamba la Miti Wino, Halmashauri ya Madaba Ruvuma leo.



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2