Na John Walter-Babati
Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini (CCM) Mheshimiwa Daniel Sillo ameahidi kutoa mabati 110 kukamilisha ujenzi wa shule shikizi ya msingi Datar iliyopo kata ya Ufana wilayani hapo.
Amesema mabati hayo atayatoa kutoka kwenye fedha za mfuko wa jimbo 2021/2022 ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu na kuwapunguzia msongamano.
Sillo aliitembelea shule hiyo ambayo ujenzi wake unaendelea ikiwa ni mwendelezo wa kuzitembelea shule mbalimbali na kutoa misaada ambapo ameshatoa mifuko ya saruji kwenye shule zilizopo jimboni kwake pamoja na mashine za kutolea nakala (photocopy) kwa baadhi ya shule za Sekondari.
Mheshimiwa Sillo amefanya Ziara kwa Kata ya Secheda na Ufana ikiwa ni muendeleo wa Ziara yake kwa kata zote 25 zilizomo ndani ya Jimbo hilo katika kuwashukuru, kuwasikiliza wananchi, kutatua kero zinazowakabili sambamba na kuwahamasiha juu ya utendaji wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Katika ziara hiyo Mhe Mbunge ameambata na Viongozi wa chama cha Mapinduzi pamoja wataalamu kutoka Idara mbalimbali ili kuweza kubainisha changamoto zinazowakabili wananchi na kuzipatia majawabu ya papo kwa hapo.
Akizungumza katika Ziara hiyo Mhe Mbunge amewahimiza wananchi wa kata hizo juu ya kuwa wamoja na kushirikiana katika kutatua changamoto za kata hiyo sambamba na kuwataka kupokea fedha za maendeleo zinazotolewa na serikali ili kuruhusu huduma za kijamii kuendelea.
Kwa upande wake katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Babati Vijijini George Sanka amewataka viongozi wa vijiji kuwa sehemu ya utatuzi wa migogoro mbalimbali katika maeneo yao na kuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo huku akisisitiza ushirikiano na umoja.
Mbunge wa Babati Vijiji, Daniel Sillo akizungumza na wakazi wa kata ya Ufana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Daffir ambapo ameahidi kuendelea kuwatumikia na kuwasemea Bungeni.
Diwani wa Kata ya Ufana Bernad Bajuta akizungumza katika mkutano huo katika kijiji cha Daffir Julai 15, 2021.
Wananchi wa kata ya Ufana wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Daniel Sillo alipowatembelea.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment