NDEJEMBI: TUTAHAKIKISHA WANAFUNZI WANAPATA MAFUNZO YA TEHAMA CHAMWINO | Tarimo Blog

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deo Ndejembi amesema atahakikisha mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanatolewa kikamilifu kwa wanafunzi wilayani Chamwino ili kuwaandaa wanafunzi hao kuwa watumishi wa umma bora watakaolitumikia taifa kwa weledi.

Ndejembi ametoa ahadi hiyo kwa Kiongozi wa Kitaifa wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 Luteni Josephine Mwambashi, mara baada ya kiongozi huyo kuzindua Mradi wa Ujenzi wa Vyumba Vitatu vya Madarasa na Madawati 120 katika Kituo cha Sekondari Msamalo kilichopo kijijini Msamalo wilayani Chamwino.

Ameongeza kuwa,wanafunzi wakipewa mafunzo mapema yatawaandaa mapema zaidi wanafunzi hao kuwa Watumishi bora wa umma na weledi ambao watalitumia taifa kwa uzalendo na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Amesema kupitia madarasa hayo yaliyozinduliwa wilaya yake itahakikisha mafunzo ya TEHAMA yanatolewa kwa ufanisi ili kuendana na Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu isemayo “TEHAMA NI MSINGI WA TAIFA ENDELEVU ITUMIKE KWA USAHIHI NA UWAJIBIKAJI”.

Ndejembi amemshukuru Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, Luteni Josephine Mwambashi kwa kukagua na kuridhia yatumike kutoa elimu kwa wanafunzi wilayani Chamwino ambao ni Watumishi wa Umma wa baadae.

Sanjari na hilo, amempongeza kiongozi huyo wa mbio za mwenge kitaifa na viongozi wenzie alioambatana nao kwa kuwa makini katika ukaguzi wa miradi yote waliopangiwa kuikagua kabla ya kuizindua rasmi.

“Mmedhihirisha kuwa, hamzindui ilimradi mmezindua bali mnazingatia ubora na thamani ya fedha iliyotumika, ikizingatiwa kuwa Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi husika” Mhe. Ndejembi amefafanua.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Kitaifa wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 Luteni Josephine Mwambashi amewapongeza wasimamizi wa mradi kwa kusimamia vema ujenzi wa madarasa hayo ambayo yatakuwa na manufaa kwa wanafunzi wilayani Chamwino.

Luteni Mwambashi amesema, kazi imefanyika na inaonekana na anatarajia kuwa uwepo wa madarasa hayo yatawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora.Kiongozi huyo, ametoa wito kwa wanafunzi watakaotumia madarasa na madawati hayo kuyatunza ili yatumike na wao na wanafunzi wengine ambao watapata fursa ya kusoma hapo.

Mbio Maalumu za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 baada ya kuhitimisha mbio zake Wilayani Chamwino kwa kukagua miradi mbalimbali na kutoa ujumbe wa mbio maalum za uhuru za mwaka 2021, umekabidhiwa Wilayani Kongwa ili kutoa fursa ya kukagua miradi na kutoa ujumbe maalum katika wilaya hiyo






 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2