MO DEWJI AWEKA BILIONI 20 ZA UWEKEZAJI SIMBA SC | Tarimo Blog


Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi, Simba SC, Mohammed Dewji (MO Dewji) leo hii amekamilisha mchakato wa kuweka kiasi cha Shilingi Bilioni 20 za Uwekezaji wake wa asilimia 49 (49%) katika Klabu hiyo baada ya kukamilika kwa mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji ulioanza miaka minne iliyopita uliosimamiwa na Tume ya Ushindani Tanzania (FCC).

Kupitia Mkutano wake na Waandishi wa Habari mkoani Dar es Salaam, MO Dewji amekamilisha kuweka kiasi hicho cha fedha huku akisema amewekeza jumla ya zaidi ya kiasi hicho alichotakiwa kuweka. Mo Dewji amesema hadi sasa amewekeza Shilingi Bilioni 45 za Uwekezaji wa Hisa zake (49%).

“Miaka minne iliyopita tulianza mchakato wa Uwekezaji katika Klabu ya Simba SC, lakini nimetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 21.3, kwenye Mishahara na Pesa za Usajili wa Wachezaji na Makocha wa timu yetu. Kila mwaka nilikuwa nikitoa kiasi cha Shilingi Bilioni 5.3 hadi kufikia hiyo Bilioni 21.3”.

“Hapo Afisa Mtendaji Mkuu anasema bado kuna usajili, bonasi kwa Wachezaji baada ya kufanya vizuri na kambi ya timu nje ya nchi kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, hapo inafika zaidi ya Bilioni 24 kutoka kwenye Bilioni 21.3.”Amesema MO Dewji.

MO Dewji amesema awali Tume ya Ushindani (FCC) ilimtaka aweke kiasi cha Shilingi Bilioni 19.6 lakini amekabidhi mfano wa Hundi ya jumla ya Shilingi Bilioni 20 ili kuondoa kelele kwa baadhi ya watu waliokuwa wakidai awekeze Pesa hizo kama sheria za Uwekezaji zilivyomtaka kufanya hivyo.

“Kwenye asilimia 49 (49%) za Uwekezaji wangu, FCC walitaka niweke kiasi cha Shilingi Bilioni 19.6 tu lakini naweka hizo Bilioni 20 kuondokana na mijadala, nimefanya hivyo lakini pia tunaona Simba SC inafanya vizuri na kuiweka Tanzania katika ramani ya Soka, tumetoka nafasi ya 22 hadi nafasi ya 12 barani Afrika.” Ameeleza MO.

Mohammed Dewji amesema Simba SC ina mipango mikubwa zaidi ikiwa pamoja na kujenga Viwanja vikubwa vya Michezo, kutengeneza Academy bora za Vijana, kutengeneza timu bora ya Wanawake (Simba Queen) ili kuendana na kushindani na timu bora Afrika kama Al Ahly SC ya Misri.

Nilimsikia Kocha wa Al Ahly, Pitso Mosimane akisema msimu uliopita katika Mashindano ya Kimataifa kafungwa na timu mbili tu yaani, Simba SC na Bayern Munich, hayo ni mafanikio kwetu lakini tusizungumzie sana kufika Robo Fainali ya CAF CL peke yake, sasa tuzungumze kwenda mbali zaidi hadi kufika Fainali ya Michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.”Ameeleza MO.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2