KUNAMBI AKAMILISHA UJENZI DARAJA LA MTO MPOFU ASEMA UCHUMI WETU UTAKUA | Tarimo Blog


Charles James, Michuzi TV

KAZI Inaendelea! Mbunge wa Jimbo la Mlimba Godwin Kunambi ameendelea na ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Jimbo lake ambapo amekagua na kuridhika na ujenzi wa Daraja la Mto Mpofu na hivyo kuondoa changamoto ya muda mrefu iliyokua ikiwakabili wananchi wa Kata hiyo.

Mbunge Kunambi amefika katika daraja hilo na kueleza kuwa kukamilika kwake kutachangia kuinua uchumi wa Kata hiyo kwani magari makubwa ya mizigo yataweza kupita juu yake kwenda kuchukua mazao kwa ajili ya kupeleka Mikoa mingine.

Amesema wakati akiomba kura za Rais katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana aliahidi kuanza ujenzi wa daraja hilo kutokana na adha ya muda mrefu waliyokua wakipata wananchi wake hasa kipindi cha mvua ambapo mto ulikua ukijaa na kuhatarisha maisha yao.

"Nawaeleza kwa dhati ni kweli kwa miaka mingi hatukuwahi kuwa na daraja la uhakika hapa, tulikua tunapata shida kuvuka hapa lakini baada ya kwenda kuomba fedha Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ilitupatia na leo wananchi wanapita hapa bila shida.

Naamini uchumi wa Igima kupitia daraja hili unakwenda kukua kwani Sasa magari makubwa yatakua yanapita kwenda Mpofu kuchukua Ndizi na mazao mengine na hivyo kuchochea ukuaji wa mapato ya ndani kwenye kata yetu," Amesema Kunambi.

Ameongeza "Hili daraja litaanza kupitisha Fuso Kubwa ambazo zinakuja kubeba mazao kama Mpunga, Ndizi na mengineyo tutapata fedha sisi kama wananchi na tutaongeza mapato yetu ya ndani na kupata fedha za kujenga Zahanati zetu, Madarasa na kuendesha maisha yetu,".

Akizungumzia sekta ya Maji, Kunambi amemshukuru Rais Samia kwa kuwezesha upatikanaji wa mradi wa maji kwenye Kata za Mbingu na Igima.

"Tayari tumeshapata fedha za mradi huu wa Maji mserereko kwenye kata hizi mbili ambapo tayari umeshaanza katika Kata ya Mbingu na kisha watamalizia Kata ya Igima, hizi zote ni juhudi za Serikali ya CCM inayoongozwa na Mama yetu mpendwa Samia Suluhu Hassan," Amesema Kunambi.

Mmoja wa wananchi wa Kata hiyo, Victor Joseph amemshukuru Mbunge Kunambi kwa kufanikisha ujenzi huo na kuondoa changamoto ya muda mrefu iliyokua ikiwakabili.

" Kwa muda mrefu hapa tulikua hatupiti hasa kipindi cha masika, tumeangaika kwa miaka mingi leo tumejengewa hili daraja tukushukuru sana Mbunge wetu," Amesema Mwananchi huyo.

Mbunge wa Jimbo la Mlimba Morogoro, Godwin Kunambi akizungumza na wananchi wa Kata ya Igima alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo jimboni kwake.
Wananchi wa Kata ya Igima, Mlimba wakimsikiliza Mbunge wao, Godwin Kunambi alipofika kujionea Daraja la Mto Mpofu ambalo limekamilika.

 Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi akikagua ujenzi wa jengo la Zahanati Kata ya Namawala ambalo yeye analisimamia.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2