Na Mwandishi Wetu
Kaimu Postamata Mkuu Macrice Daniel Mbodo amewataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania kushirikiana na uongozi wa Shirika katika kuhakikisha wafanyakazi wanatimiza wajibu wao katika utekelezaji wa malengo ya Shirika.
Wito huo umetolewa wakati wa kikao na Viongozi wa vyama vya Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania Bara na Zanzibar, katika Makao Makuu ya Shirika la Posta Tanzania, jijini Dar es Salaam.
Mbodo ametumia nafasi hiyo kuelezea mpango mkakati wa Shirika kwa mwaka 2021/2022, ikiwa ni pamoja na kuongeza masoko kwa kutafuta na kutumia fursa mpya za kibiashara ndani na nje ya nchi.
Aidha, katika kikao hicho Mbodo amewaeleza viongozi wa wafanyakazi mwelekeo wa Shirika katika kipindi hiki cha maendeleo ya kiteknolojia na namna ambavyo Shirika limejipanga kiutekelezaji hasa katika maeneo matano.
Ameyataja maeneo hayo ambayo ni usismamizi wa rasiliamali watu, utawala bora, utoaji wa huduma kwa wateja, kusimamia kazi za msingi za Shirika, utendaji na ufanisi wa usimamizi wa fedha.
“Tumekutana hapa leo ili tujadiliane na tuangalie nini mwelekeo wa Shirika kwa mwaka 2021/22 hasa katika maeneo haya matano ili tutembee pamoja na tuwe na mwelekeo unaofanana, kwa sababu naamini viongozi wa wafanyakazi ni viongozi kama tulivyo sisi”. Amesema Mbodo
Pia ameongeza kuwa Shirika limejipanga kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake ili kuboresha utendaji kazi na kuhakikisha Shirika linatoa huduma kulingana na mahitaji ya umma.
Mbodo amesema, ndani ya miaka mitano ijayo anataka kuona Shirika la Posta linafanya vizuri zaidi duniani na kuongeza kuwa Posta imekuwa moja ya taasisi kubwa nchini yenye kuleta tija kwa taifa.
"Shirika la Posta ni Shirika lenye Mtandao Mpana sana, limeunganishwa na Ofisi zaidi ya 600,000 kote Duniani, ambazo zote zipo chini ya Umoja wa Posta Duniani, kwa upana huo Shirika linaweza kufikia wananchi wengi kwa wakati mmoja”. Amesema mbodo
Kwa upande wa Meneja Mkuu Rasiliamali za Shirika Aron Samwel ameeleza kuwa, kwa sasa Shirika liko kwenye maboresho makubwa ya kiutendaji hasa kwa upande wa mifumo yake ili kuhakikisha Shirika linatoa huduma stahiki kwa wananchi kama inavyotarajiwa.
“Hatujakaa kimya maboresho ya mifumo yetu yanaendelea kufanyika na tunafanya kazi usiku na mchana kulishughulikia hilo”. Amesema Aron.
Naye Meneja Mkuu Uendeshaji Biashara Constantine Kasese ameongeza kuwa Shirika linaendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ambapo kwa sasa tayari mchakato wa kuagiza magari 13 ambayo yatatumika kuwezesha shughuli za usafirishaji umeshaanza.
“Tumepata kibali cha kununua magari na tayari mchakato umeshaanza, niwatoe hofu Shirika linaendelea kuboreshwa kila siku”. Amesema Kasese.
Kikao hicho kilihuhudhuriwa na Meneja Mkuu Rasilimali za Shirika, Meneja Mkuu Uendeshaji Biashara, Meneja Rasilimali watu, Viongozi wa vyama vya Wafanyakazi na baadhi ya wawakilishi wa wafanyakazi.
Kaimu Meneja Mkuu Rasilimali za Shirika la Posta Tanzania Aron Samwel akizungumza katika kikao cha Viongozi wa vyama vya Wafanyakazi wa Shirika hilo Bara na Zanzibar, Makao Makuu ya Shirika, jijini Dar es Salaam.
Kaimu Meneja Mkuu Uendeshaji Biashara wa Shirika la Posta Tanzania Constantine Kasese akizungumza katika kikao cha Viongozi wa vyama vya Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania Bara na Zanzibar, Makao Makuu ya Shirika hilo, Dar es Salaam. Kaimu Postamasta Mkuu Macrice Daniel Mbodo akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa vyama vya Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania, mara baada ya kikao na viongozi hao, Makao Makuu ya Shirika la Posta, jijini Dar es Salaam.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment