Amshukuru Rais Samia kwa kufuta tozo katika urejeshaji mikopo
Azungumzia TZS 570 bilioni zilizotengwa kwa wanafunzi 160,000 mwaka 2021/2022
Na Mwandishi Wetu – Dar es salaam
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (pichani) amewataka wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu iliyoiva kurejesha ili iwanufaishe watanzania wengine wahitaji kwa kuwa Serikali imewapunguzia mzigo kwa kufuta tozo ya kulinda thamani iliyokua inalalamikiwa.
Akizungumza mwishoni mwaka wiki jijini Dar es salaam katika hafla ya uzinduzi wa Mwongozo wa Uombaji Mikopo kwa mwaka 2021/2022, Prof. Ndalichako amesema Serikali imefuta tozo na adhabu katika mikopo hiyo ili kuwapa ahueni na hivyo hawana budi sasa kurejesha.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kufuta tozo ya asilimia 6 ya kulinda thamani ya mikopo iliyokuwa inatozwa kwa wanufaika. Naomba niwasihi sana wanufaika wote wa mikopo kufanya marejesho ili fedha mtakazorejesha ziendelee kuwanufaisha vijana wengine wenye uhitaji,” amesema Waziri Ndalichako.
Mei 1 mwaka huu, akiwa katika sherehe za Mei Mosi jijini Mwanza, Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza kufutwa tozo ya kulinda thamani baada ya ombi la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) wakieleza kuwa inaongeza mzigo kwa wafanyakazi.
Aidha, Mei 4 mwaka huu, wakati akihitimisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia bungeni, Prof. Ndalichako alielekeza kufutwa kwa adhabu ya asilimia 10 kwa wanufaika ambao hawajaanza kurejesha mikopo iliyoiva.
Akizungumza kuhusu maelekezo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wan HESLB Abdul-Razaq Badru amesema maagizo hayo yote yameshatakelezwa na kuanzia Julai 1 mwaka huu, taarifa binafsi za madeni hazina tozo na adhabu.
Kuhusu utoaji mikopo kwa mwaka 2021/2022, Prof. Ndalichako amesema Serikali imetenga TZS 570 bilioni katika mwaka 2021/2022 zitakazowanufaisha zaidi ya wanafunzi 160,000.
Kwa mujibu wa Prof. Ndalichako, kati ya wanafunzi hao 160,000, wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanatarajiwa kuwa 62,000 wakati wanaoendelea na masomo watakua 98,000.
“Niwaibie siri tu. Hadi mwezi uliopita, bajeti ya mikopo kwa mwaka 2021/2022 ilikua TZS 500 bilioni. Lakini katika siku zake 100 za uongozi kama Rais wetu, Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan ameongeza TZS. 70 bilioni na kufikia hizi TZS. 570 bilioni kwa mwaka 2021/2022 sawa sawa na ongezeko la TZS. 106 bilioni (22.8%)” alisema Prof. Ndalichako.
Aliongeza kuwa ongezeko hilo linathibitisha nia ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kuwawezesha vijana wengi kupata fedha na kusoma ili watumikie nchi yao na kuwataka waombaji wahitaji watulie, na kusoma maelekezo na kuomba kwa usahihi ili watimize ndoto zao.
Katika mwaka huu wa masomo wa 2020/2021, Serikali imetenga na kutoa TZS 464 bilioni zinazowanufaisha jumla ya wanafunzi 149,398. Kati yao, wanafunzi 55,287 ni wa mwaka wa kwanza na wengine 94,111 ni wale wanaoendelea na masomo.
Aidha katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako aliitaka HESLB kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa waombaji ili waweze kuelewa sifa na utaratibu wa kuomba mkopo kwa usahihi na kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuwasaidia vijana wengi wanaoomba mikopo.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za HESLB, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema wamepokea maelekezo na kuanzia Julai 12 mwaka huu, maafisa wa HESLB wataanza kuendesha programu za elimu ya uombaji mikopo kwa usahihi chini ya kampeni ya #WeweNdoFuture.
“Tunakamilisha utaratibu na uongozi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili tuwafikie vijana wote waliopo katika kambi 19 za JKT kuanzia Julai 12 … tutaendesha pia programu hizi kupitia televisheni, redio, mitandao ya kijamii na mikutano na wadau,” amesema Badru.
Kuhusu utaratibu na muda wa kuomba, Badru amesema Mwongozo wa Uombaji mkopo unaoeleza sifa na utaratibu wa kuomba mkopo unapatikana katika www.heslb.go.tz kuanzia juzi (Ijumaa, Julai 2, 2021).
“Mwongozo upo katika tovuti kuanzia Julai 2 na tunawashauri waombaji wausome kabla ya kuomba. Aidha, mfumo wa kupokea maombi kuwa wazi kwa siku 53 kuanzia, Julai 9 hadi Agosti 31, 2021,” amesema Badru.
Mkutano huo wa uzinduzi pia uliohudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe na wawakilishi kutoka Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambao pia huwahudumia waombaji mikopo.
HESLB ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria, ikiwa na majukumu makuu ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji na kukusanya mikopo iliyoiva iliyotolewa na Serikali kwa wanafunzi wa elimu ya juu tangu mwaka 1994/1995.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment