Na Abubakari Akida,MOHA
Katika kukabiliana na wimbi la mahabusu katika magereza mbalimbali nchini na kuwapunguzia mzigo Jeshi la Magereza Serikali imeanzisha Operesheni Maalumu ijulikanayo kwa jina la “Operesheni Punguza Mahabusu” ambayo inafanyika nchi nzima.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo wakati akizungumza katika kikao kilichohusisha Wafungwa na Mahabusu wanawake katika Gereza Ruanda jijini Mbeya ambapo pia alitoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo magodoro, Taulo za Kike, Miswaki na sabuni kwa wafungwa na mahabusu hao.
“Miongoni mwa mambo ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassani hapendi kuyaona ni mrundikano na muongezeko wa watu katika majela hasa wanawake kwa kuwa anaamini wanawake ndio wanaojenga nchi na jamii wakishirikiana na wanaume, kikubwa tunaichukua changamoto na tayari tunaanzisha operesheni maalumu itakayoitwa Operesheni Punguza Mahabusu”
Aliongeza pia tayari serikali imeanza kuyaendea mbio baadhi ya mambo ikiwemo changamoto ya kuchelewa kwa upelelezi, utolewaji dhamana kwa kesi ndogondogo ambazo ndio zinaongoza kwa kujaza mahabusu wengi katika magereza hali inayopelekea magereza kuhemewa na mzigo mkubwa wa kulisha mahabusu.
Akizungumzia hali ya msongamano katika Gereza hilo Mkuu wa Gereza la Wanawake, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Rehema Mwailunga alikiri kuwepo kwa msongamano ambao unasababishwa na mkoa wa Mbeya kuwa na Mahakama ya kanda.
“Mheshimiwa Naibu Waziri,nashauri ili kupunguza msongamano nashauri tuone umuhimu wa kujenga bweni la wafungwa na mahabusu wa kike sambamba na hili lililopo hapa lakini nakiri msongamano huu unasababishwa na kuwepo kwa mahakama ya Kanda hapa Mbeya hivyo mahabusu na wafungwa wengi kutoka magereza ya wilaya wanakuja kusikiliza kesi na rufaa zao hapa” alisema SSP Rehema.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo akimkabidhi miche ya sabuni,Mkuu wa Gereza la Wanawake Ruanda,Mrakibu Mwandamizi wa Magereza,Rehema Mwailunga kwa ajili ya wafungwa.Naibu Waziri yupo jijini Mbeya kwa ziara ya kikazi ambapo alipata fursa ya kuzungumza na kuwasikiliza wafungwa na mahabusu lengo ikiwa kushughulika na msongamano wa mahabusu katika magereza mbalimbali nchini.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment