Na Mwandishi Wetu, Dar
Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo, amegeuka mbogo kwa kile alichokiita kuwepo kwa baadhi ya watendaji wanaoiba fedha serikali.
Shigongo aliyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Global zilizopo Sinza jijini Dar es Salaam.
Alisema: “Ninaomba Halmashauri ya Buchosa ikaguliwe sababu pesa zinapotea, fedha zinaliwa, mtu anakuja pale anafanya kazi miezi miwili tayari ana nyumba mbili wakati kipato chake hakitoshi kujenga nyumba mbili, kwa niaba ya watu wa Buchosa nasema jambo hili hatulikubali niungwe mkono ama nisiungwe mkono na Madiwani mimi nitasimama imara kuhakikisha fedha zinzokuja zinatumika vizuri".
Aliongeza kuwa, tangu serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan iingine madarakani fedha nyingi za maendeleo kwa wananchi zimepelekwa kwenye halmashauri mbalimbali lakini akadai huko zinatumiwa vibaya.
“Nianze kwa kuelezea Serikali ya Awamu ya Sita, imekuwa ikijikita sana kwenye kupeleka fedha za maendeleo kwa wananchi. Mimi ni shahidi kama Mbunge wa Buchosa, nimeshuhudia fedha nyingi zikija kwa ajili ya maendeleo,” - Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Mhe. Eric Shigongo
Aliongeza kwa kumuomba rais Samia kuwahamisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buchosa pamoja na Idara ya uhasibu katika Halmashauri hiyo, akiwatuhumu kwamba wamekuwa wakiibia fedha halmashauri hiyo.
“Mimi nilikuwa sijawahi kuhitilafiana na Mkurugenzi wangu hata mara moja mpaka nilipoanza kufuatilia mapato ya ndani, mimi naomba Mheshimiwa Rais aniondolee Mkurugenzi, aniondolee idara ya uhasibu isipokuwa amuache Mwekahazina peke yake," amesema Mbunge Shigongo.
Aidha, Shigongo amewaomba wananchi kuzidi kutoa ushirikiano kwa serikali kutokana na kile alichokiita kwamba uongozi wa Awamu hii unakwenda kuleta maendeleo yatakayowashangaza wengi.
Kuhusu kuwepo kwa malalamiko ya Tuzo kwenye Miamala ya simu ambalo liliidhinishwa na bunge na kwamba sasa linalalamikiwa na wananchi kwamba linawaumiza kiuchumi Shigongo alisema:
“Mimi siyo msemaji wa serikali lakini kinacholalamikiwa na wengi siyo kuwepo kwa Tozo bali ni kiasi kikubwa kinachotozwa, mimi naamini serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu italiangalia jambo hilo.”
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment