TANESCO KUWA MAHALI SALAMA PA KUFANYIA KAZI,KUONDOA AJALI ZINAZOHUSIANA NA UMEME | Tarimo Blog

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limejipanga kuwa mahali salama pa kufanyia kazi pamoja na kuondoa ajali zote zihusianazo na Umeme kuanzia kwa wafanyakazi mpaka kwa wateja.

Hayo yamebainishwa na Mhandisi Stephen Manda, alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO katika maadhimisho ya siku ya afya na usalama kazini. TANESCO huadhimisha siku hiyo mara moja kwa mwaka ambapo awamu hii ilifanyika mkoani Rukwa, baada ya Mkoa huo kuibuka kinara katika kuzingatia na kufuata kanuni na taratibu za afya na usalama kazini.

“Shirika limejipanga na limedhamiria kwa dhati kufanya kazi kwa ufanisi kwa kuzingatia sera ya Shirika ya usalama na afya mahala pa kazi katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme,"amesema Mhandisi Manda.

Mhandisi Manda ameongeza sera hiyo inapaswa kuzingatiwa na kufuatwa na wafanyakazi wote, ili pasiwepo na mfanyakazi yeyote atakayepata ajali akiwa kazini na kushindwa kurejea nyumbani kwake na familia yake akiwa salama.

Aidha, kwa upande wa wateja na wananchi, Mhandisi Manda alieleza kuwa, uzingatiaji wa taratibu zote za usalama katika miundombinu ya Umeme sambamba na kuchukua tahadhari na kuzingatia matumizi salama na sahihi ya umeme, kutaondoa kabisa ajali zinazoweza kujitokeza kutokana na Umeme.

Wakati huo  Meneja wa Afya na Usalama kazini, Fredy Kayega akizungumza katika hafla hiyo alieza kuwa, TANESCO imekuwa ikizingatia na kusimamia masuala yote ya usalama na afya mahali pa kazi kama moja ya vipaumbele wezeshi katika kutimiza malengo ya Shirika, ambapo Ofisi ama Mikoa inayofanya vizuri katika kuzingatia Sera ya Afya na Usalama mahala pa kazi hutambuliwa na kupewa motisha ya zawadi.

Ameongeza kuwa Mikoa ama Ofisi zinazofanya vibaya kwa kuwa na ajali nyingi hupewa onyo kali na kutakiwa kujitathmini upya namna ambavyo usalama na afya za wafanyakazi na Wateja zinavyozingatiwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Katika uzingatiaji wa Sera hiyo kwa mwaka 2019/20, Bw. Kayega aliutaja Mkoa wa Rukwa kama mshindi namba moja ukifatiwa na Mkoa wa Tabora na Ruvuma na Huku Vituo vya kufua Umeme vya Kinyerezi 1, Nyakato na Hale vikiongoza upande wa kundi la vituo vya Umeme.

Maadhimisho hayo ya Siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi TANESCO (TANESCO Safety day) yaliambatana na bonanza lililojumuisha michezo mbalimbali kwa wafanyakazi kwa lengo la kuimarisha afya ya mwili na akili.

Mhandisi Stehen Manda akikabidhi cheti kwa moja ya kiongozi wa TANESCO Mkoa  wa Rukwa ambao umeibuka kinara katika kuzingatia kaununi na taratibu za afya na usalama kazini


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2