UJUMBE WA KAMPUNI KUBWA TISA ZA NCHINI UFARANSA ZINAZOJIHUSISHA NA UCHUMI WA BULUU UPO TANZANIA KUANGALIA FURSA ZA UWEKEZAJI | Tarimo Blog

 

Na Said Mwishehe,Michuzi TV
WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa kwa kushirikiana na Taasisi ya Business France ya Ufaransa wameratibu ziara ya ujumbe wa Wafanyabiashara kutoka kampuni kubwa tisa za nchi hiyo ambayo yanayojishughulisha na uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu (blue economy)kuja nchini Tanzania kwa mkutano wa siku mbili. 
Aidha ujumbe wa kampuni hizo umekutana na wadau mbalimbali kutoka Tanzania wakiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Uvuvi, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi,Mamlaka ya Bandari TZ (TPA), Shirika la Meli la Taifa(TASAF),Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC)pamoja na wadau wengine.
Mkutano kati ya wadau hao umefanyika leo Julai 29,2021 katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam ambapo washiriki takriban 60.Kwa mujibu wa ratiba mkutano huo utafanyika kwa siku mbili kuanzia leo na kesho Julai 30 mwaka huu wa 2021.
Kwa siku ya leo ambayo ndio ya kwanza wadau hao kukutana na kujadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano katika maeneo ambayo wameyapa kipaumbele ujumbe wa Ufaransa umeonesha shauku kubwa za kutaka kushirikiana katika sekta hiyo. 
Akizungumza wakati wa mkutano,Balozi wa Ufaransa hapa nchini Fréderic Clavier amesema ujumbe wa wafanyabishara kutoka Ufaransa wako tayari kufanya kazi kwa karibu na Tanzania ambayo ina utajiri mkubwa wa rasilimali mbalimbali ikiwemo bahari, mito na maziwa.
"Tanzania na Ufaransa zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika maeneo mbalimbali na kwamba  ujio wa kampuni hizi kutoka nchini Ufaransa kutazidi kuuimarisha ushirikiano huu na kuleta faida kwa pande zote mbili.Kampuni hizi kwa sehemu kubwa zinazojishughulisha na masuala ya uvuvi.
"Usalama wa baharini,kilimo,ujenzi wa miundombinu na utalii na uwezo mkubwa wa utendaji, zimewekeza katika mataifa mbalimbali na kwa hatua yao ya kutafuta fursa ya kuja kuwekeza nchini kunaonyesha nia yao ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuleta maendeleo,"amesema Balozi Clavier.
Kwa upande wake Waziri wa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dk.Leonard Chamuriho ametumia mkutano huo kueleza kuwa Serikali inawakaribisha wawekezaji  hao wa  Ufaransa na amewaleza uwepo wa fursa mbalimbali  katika sekta ya bandari na uvuvi.
Amesema Tanzania chini ya mpango wa 'Uchumi wa Blue' imeainisha fursa mbalimbali za uwekezaji zikiwemo za uvuvi, ufugaji wa baharini, ufugaji wa samaki, ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki, ukulima wa mwani, bandari, usafiri na usafirishaji baharini  hivyo na kwamba ujio wa makampuni utaongeza chachu ya kufikiwa kwa azma hiyo.
Aidha amesema suala la utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia baharini ni miongoni mwa mambo yanayofungamana na uchumi wa bluu."Serikali tunazidi kuendelea kuwakaribisha wawekezaji wote kuja kutumia fursa hizo zilizopo hapa nchini."
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk. Rashid Tamatamah amesema kupitia fursa ya ujio wa wawekezaji hao, matarajio sekta ya uvuvi nchini itapiga hatua zaidi kutokana na uwepo wa fursa mbalimbali ndani ya sekta hiyo yenye mchango mkubwa katika pato la taifa.
"Tanzania ipo katika mpango mkubwa wa kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta huyo hususani kwa kuboresha uvuvu katika eneo la maji makuu ambapo licha ya mikakati yake ya ununuzi wa meli za uvuvi pia inazo fursa kwa wawekezaji wenye nia ya kuja kuwekeza katika eneo hilo,"amesema Dk.Tamatamah.
Awali Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Kampuni ya Wafanyabiashara wa Ufaransa (Business Frabce) Ludovic Prévost amewashukuru washiriki na kueleza kufurahishwa kwake na washiriki waliojitokeza na kueleza wako tayari kwa ajili ya kuona maeneo ya ushirikiano hapa Tanzania.
Amemshukuru Balozi Samwel Sherukindo kwa ufafanuzi mzuri na maelezo kuhusu uwekezaji na biashara nchini ikiwa ni pamoja na ushirikiano alioutoa kufanikisha ziara yao.
Waziri wa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dk.Leonard Chamuriho(kulia)akisoma moja ya lenye maelezo ya ujumbe huo wa kampuni tisa kutoka nchini Ufaransa wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaa.Kulia ni Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Fréderic Clavier wakiwa na washiriki wengine.
Waziri wa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dk.Leonard Chamuriho akizungumza wakati wa mkutano ulioshirikisha ujumbe kutoka kampuni tisa za nchini Ufaransa pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya uchumi wa buluu nchini Tanzania.Mkutano huo umefanyika leo Julai 29,2021 jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya ujumbe wa kampuni tisa kutoka nchini Ufaransa ambao upo nchini Tanzania kwa lengo la kujadili na kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji hasa kwenye eneo la uchumi wa buluu.
Meneja Ukanda wa Afrika Mashariki Mariam Faridah kutoka Kampuni ya SEAOWL akifafanua jambo wakati wa mkutano huo.
Baadhi ya maofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na maofisa kutoka taasisi nyingine wakiwa kwenye mkutano huo.
Sehemu ya washiriki wakifuatilia majadiliano wakati mkutano huo ambao umeanza leo Julai 29,mwaka 2021 na unatarajia kumalizika kesho Julai 30,mwaka 2021.
Washiriki wakiendelea kufuatilia majadiliano ya mkutano huo ambao umehusisha taasisi mbaimbali za umma pamoja na ujumbe wa kampuni tisa kutoka nchini Ufaransa.
Waziri wa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dk.Leonard Chamuriho(katikati) akifuatilia hotuba ambazo zilikuwa zinatolewa na baadhi ya wawakilishi wa kampuni kutoka nchini Ufaransa ambao wapo nchini Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk. Rashid Tamatamah akizungumza wakati wa mkutano huo.
Mmoja ya wajumbe kutoka nchini Ufaransa ambao wamekuja nchini Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji akifafanua jambo kuhusu shughuli zinazofanywa na kampuni yao



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2