MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR AKUTANA NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI | Tarimo Blog

MKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR AKUTANA NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuandaa mpango maalumu wa kushirikiana na Zanzibar kwa lengo la kuendelea kuitangaza na kuboresha uhusiano wake na nchi mbalimbali duniani. 

Ametoa kauli hiyo leo (Julai 29) wakati alipokutana na ujumbe wa Wizara hiyo uliofika ofisini kwake Migombani Mjini Unguja, kwa lengo la kujitambulisha pamoja na kueleza kazi zinazofanywa na wizara hiyo sambamba na kusikiliza maoni ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika kuimarisha mahusiano na utendaji kati ya ofisi mbili hizo kwa mustakabali mpana wa kuiinua kimaendeleo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

"Zanzibar inategemea pia washirika kutoka nchi mbali mbali duniani katika kuinua uchumi wake hivyo Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki kuandaa mpango mahususi wa kimaendeleo na mashirikiano kutasaidia kufanikisha malengo ya Serikali ya kuiweka Zanzibar katika mazingira bora". Alieleza Makamu huyo wa Kwanza wa Rais.

Mhe. Othman ameongeza kuwa kuwepo kwa mipango madhubuti kutatoa wepesi kwa Zanzibar katika utekelezaji wa mipango ya kimaendeleo ambayo hufadhiliwa na nchi mbalimbalimbali washirika.

Aidha Mhe. Othman ameikumbusha Wizara hiyo kuangalia namna Zanzibar itakavyoweza kufanya kazi na taasisi zilizopo Nairobi nchini Kenya zinazoiwakilisha Tanzania, ambazo zimekuwa zikijihusisha na masuala mbali mbali yakiwemo Mazingira na Madawa ya kulevya ili kuisaidia Zanzibar katika masuala ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kupambana na biashara haramu ya madawa ya kulevya, yote mawili yakiwa masuala muhimu kitaifa na kimataifa pamoja na kutambulisha uwepo wa Zanzibar ndani ya Jamhuri ya Muungano.

Sambamba na hayo, Mhe. Othman ameeleza umuhimu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kuweka mkakati maalumu wa kukutana na watendaji wa Serikali ya Zanzibar kwa lengo la kufahamu nafasi ya Zanzibar na Tanzania kiujumla kimataifa jambo litakalokuza ufanisi katika kazi zao.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Rutageruka Mulamula, alimuelezea Mhe. Othman mipango ya kubadilisha Sera ya Wizara hiyo na jinsi itakavyotatua baadhi ya changamoto mbali mbali pamoja na kutanuwa wigo wa uwakilishi na ushiriki wa pande mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.

Aidha, Waziri Mulamula ameipongeza Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo imekuwa ni chachu kubwa ya kuifungua Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kimataifa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Saada Mkuya Salum, naye amemueleza Waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki haja ya kujitahidi kuiangalia Zanzibar na kuisaidia katika mapambao ya kudhibiti madawa ya kulevya pamoja na kuzikabili athari za mabadiliko ya tabianchi, nakusisitiza umuhimu wa kukutana mara kwa mara ili kuona namna bora ya kusaidiana katika kupambana na changamoto zinazojitokeza.









Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2