UJUMBE WA MRISHO MPOTO KWA WATANZANIA KUHUSU KUPENDA VYA TANZANIA, AWAHIMIZA KUWA WAZALENDO | Tarimo Blog

Na Said Mwishehe, Michuzi TV.

MSANII maarufu nchini Mrisho Mpoto 'Mjomba Mpoto' ameamua kutumia Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea Viwanja vya Mwalim Nyerere ,Dar es Salaam kuhamasisha Watanzania kuwa wazalendo kwa kupenda vitu vya nchi yao , hata wanapotaka kusafiri au kusafirisha mizigo yao basi watumie kampuni za Tanzania.

Akizungumza katika maonesho hayo baada ya kutembelea banda la Kampuni ya Huduma za Meli, Mpoto ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha Watanzania kuweka kipaumbele kwa kusafiri au kusafirisha mizigo yao kwa kutumia kampuni hiyo ambayo meli zake ziko katika maziwa makuu yote nchini.

"Kampuni hii ya huduma za meli ni ya Serikali ya Tanzania, inafanya kazi ya kusafirisha abiria na mizigo , unajua lazima tuwaambie Watanzania kampuni hii inafanya kazi kwenye maziwa yote Ziwa Victoria,Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika .Kwa hiyo niwaombe tutumie kampuni hii tunapotaka kusafiri.

"Kampuni hii ni ya kizalendo kwa ajili ya kusafiri sisi wenyewe na mizigo yetu, tukiamua kusafiri nayo huo ndio uzalendo , nimefika kwenye banda la kampuni hii kwasababu mimi ni mzalendo na niko tayari kutumia usafiri huu wa meli.Kitu ambacho kimenivutia kwanza ni uzalendo ,tuvipe thamani vitu vya nyumbani.

"Unaposhindwa kukipa thamani chako cha nyumbani kwako Tanzania huko ni kukosa uzalendo, hivyo moja ya kazi yangu katika Sabasaba hii nataka kuhubiri uzalendo kwa kuwataka wananchi kutumia bidhaa za Tanzania ambazo ni za kwetu kabisa, kwa mfano mimi nikisafiri kwenye kampuni ya Tanzania nitaongiza mapato kwenye nchi yangu kwa ujumla lakini nikisafirisha mizigo yangu kwa kutumia meli za Tanzania maana yake fedha inarudi nchi kwetu, hiyo neno uzalendo lina sentensi chache tu.Ndio maana nikafunga safari kutoka huko kuja kwenye kampuni hii."

Kwa upande wake Ofisa Operesheni wa Kampuni ya Huduma za Meli Anthony Nyamhanga amememshukuru Mpoto kwa kuhamasisha wananchi kutumia meli zilizopo kwenye maziwa makuu huku akitumia nafasi hiyo kueleza kuwa wako mbioni kuanza kutengeneza meli kubwa ya mizigo ambayo itatoa huduma katika ukanda wa Bahari ya Hindi.

"Hivi karibuni tutakwenda Bahari ya Hindi kwa ajili ya kujenga meli kubwa ya mizigo na hivyo kupanua huduma zetu katika ukanda huu wa bahari ya Hindi.Meli hiyo itakapokamilika itahudumia mataifa mbalimbali duniani,'amesema Nyamhanga.

Kuhusu kampuni hiyo , amesema inamilikiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na kusimamiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kwamba ilianzishwa kutoka idara ya huduma za meli iliyokuwa chini ya Shirika la Reli Tanzania(TRC) na kuwa kampuni ya huduma za meli iliyoanzishwa Sheria ya kampuni Tanzania Desemba 8,1997 na kutunukiwa cheti cha usajili.

"Dira yetu ni kuwa kampuni inayoongoza kwa huduma za usafiri kwa njia ya maji yenye ushindani , tegemeo na yenye kumjali mteja.Dhima yetu ni kutoa huduma ya usafiri yenye kuongoza , inayotegemewa , ya uhakika ,endelevu na salama kabiashara,"amesema.

Msanii Mrisho Mpoto(kushoto) akikabidhiwa kalenda ya Kamppuni ya Huduma za Meli na Ofisa Operesheni wa Kampuni hiyo Anthony Nyamhanga(kulia) baada ya msanii huyo kufika katika banda lao lililopo kwenye Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimaifa yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Mrisho Mpoto(kushoto) akiteta jambo na Ofisa Operesheni wa Kampuni ya Huduma za Meli Anthony Nyamhanga
Msanii Mrisho Mpoto akisaini kitabu cha wageni baada ya kufika banda la Kampuni ya Huduma za Meli
Mrisho Mpoto akiwa na wasanii wa kikundi cha ngoma za asili akielekea banda la Kampuni za Huduma za Meli kwenye Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea viwanja vya Mwalim Nyerere ,Dar es Salaam
 
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2