STAMICO YAANIKA MIKAKATI YAKE KATIKA KUENDELEZA SEKTA YA MADINI NCHINI, YAGUSIA WACHIMBAJI WADOGO | Tarimo Blog


Na Said Mwishehe, Michuzi TV.

UWEPO wa makaa ya mawe yanayotumika kutengeneza mkaa mbadala umekuwa moja ya kivutio kikubwa cha wananchi wengi wanaofika katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa kufika kwenye banda la Shirika la Madini la Taifa(STAMICO) huku shirika hilo likiweka wazi katika maonesho hayo mbali ya kutoa elimu kupitia watalaamu wao, wapo tayari kupokea maoni na kufanya kazi.

Akizungumza na Michuzi Blog na Michuzi TV, Ofisa Uhusiano wa Shirika la STAMICO Bibiana Ndunguru amesema tangu yalipoanza maonesho ya biashara ya kimataifa katika Viwanja vya Mwalim Nyerere ,Dar es Salaam kumekuwa na idadi kubwa ya wananchi wanaofika kwenye banda lao na wengi wamekuwa na sababu tofauti lakini kubwa wanavutiwa na yale ambayo wamekuwa wakiyaona na kuyasikia kutoka kwa watalaamu wao.

"Wananchi wengi wanaokuja hapa wanakuja kuangalia sampuli za makaa ya mawe ambazo tumekuja nazo hasa makaa ambayo yanatumika kutengeneza mkaa mbadala ambayo ndio teknolojia mpya.Wanataka kufahamu kuhusu huu mkaa unafanyaje kazi, unatengenezwa na nini, na faida yake kwa ujumla na upatikanaji wake.Pia wapo wanaouliza kuhusu kiwanda cha kusafisha dhahabu kilichozinduliwa hivi karibuni.

"Hivyo hivyo wanapokuja hapa wanataka kujua kinafanyaje kazi, dhahabu zinapatikana wapi na mwisho wa siku zinakwenda wapi na faida ya kiwanda hicho kwa Watanzania , kwa hiyo watalaam wetu wanatumia nafasi hii ya maonesho ya biashara kuwaelezea na kukusanya maoni,"amesema.

Kuhusu mkaa mbadala STAMICO wamekuwa wakieleza wananchi faida zake, kwanza kabisa ni kupunguza matumizi ya mkaa unaotokana na miti ili kuzuia uharibifu wa mazingira kwani watu wengi wanatumia mkaa unaotokana na miti,hivyo miti mingi inakatwa kwa hiyo wao wanaeleza ni kwa namna gani mkaa mbadala utasaidia kutunza mazingira.

Ndunguru amesema STAMICO wamekuwa wakichimba makaa ya mawe kwa hiyo yapo ambayo wanayauza makaa yakiwa mazima kulingana na mahitaji ya mteja lakini kuna vumbi linalobakia ambalo hilo badala ya kuliacha kuwa uchafu wameamua kulibadilisha na kulitumia kutengeneza mkaa mbadala.

Aidha amesema wananchi ambao wanafika kwenye banda lao wamekuwa wakiwafahamisha kuwa STAMICO ni shirika la Serikali linalofanya kazi mbalimbali ikiwemo ya kuwekeza kwenye sekta ya madini kwa kuchimba na kuendeleza migodi inayomilikiwa na Serikali.Mpaka sasa kuna migodi miwili inayomilikiwa na Serikali ambao ni mgodi wa dhahabu wa STAMICO na mgodi wa makaa ya mawe.
Pia kuwalea na kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuwapa elimu ni kwa namna gani wanaweza kuachana na uchimbaji hatarishi na sio rafiki kwao kwa afya zao na maisha yao, pia sio rafiki kwa mazingira."Kwa hiyo tunawataka kuachana na uchimbaji huo ili wahamie kwenye uchimbaji bora na wenye tija".

"Kwa upande mwingine tunatoa ushauri wa kimazingira, na utafiti,tunafanya kazi za ubia katika baadhi ya migodi na shughuli zetu , kwa mfano tunaubia katika kiwanda cha dhahabu.Kuhusu mikakati yetu ni kuifanya STAMICO iwe njia au lango kuu la kuwezesha uchumi ambao unaotegemea sekta ya madini,"amesema Ndunguru.

Ameongeza pia kuangalia kwa namna gani wachimbaji wadogo wanaweza kunufaika kupitia STAMICO kwa kuwapa elimu ya kutosha ili mwisho wa siku waachane na uchimbaji wenye athari, waje kwenye uchimbaji mzuri.

"STAMICO tunataka kuleta uchimbaji mdogo wenye tija , pia tunataka kuifanya sekta ya madini kuwa na manufaa kwa jamii ili isiwe tu sekta ya madini inawanufaisha watu wachache, ndio maana unaona tunajitahidi kutafuta wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta ya madini, tumejenga kiwanda cha kusafisha madini na teknolojia ambayo inatumika pale itabaki pia kwa Watanzania.

Aidha amesema kwenye banda lao kuna kundi la wachimbaji wenye usikivu hafifu ambao waliwakusanya pamoja kutoka kanda ya ya ziwa kutoka Wilaya ya Sengerema, Geita, Mwanza , Chato na maeneo mengine ya kanda ya ziwa.Tuliwachukua na kuwapa elimu ya uchimbaji mdogo ambao ni salama, hivyo walikuwepo hapa, wanaelezea kwa namna gani wananuifaka na uwepo wa STAMICO.

Ujumbe wa STAMICO kwa Watanzania hasa wanaokwenda kwenye banda lao, wamewaomba wawe mabalozi wazuri kwa wengine baada ya kupata kila aina ya ufafanuzi kutoka kwa watalaamu wao."Pia tunatumia nafasi hii kukusanya maoni, hivyo tutaendelea kuyapokea lengo letu ni kuijenga STAMICO yetu kwa manufaa ya Watanzania wote."

Wananchi wakiwa kwenye banda la Shirika la STAMICO wakiendelea kupata maelezo kutoka kwa maofisa na watalaam wa shirika hilo wakati maonesho ya 45 ya biashara ya Kimataifa yakiendelea Viwanja vya Mwalim Nyerere,Dar es Salaam.
Mmoja wa maofisa wa Stamico akitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea banda la Shirika hilo
Mmoja wa maofisa wa Shirila la Madini la Taifa( STAMICO) akifafanua jambo akiwa kwenye banda la shirika hilo lililopo viwanja vy Mwalim Nyerere maarufu Sabasaba
Mmoja wa maofisa wa Shirila la Madini la Taifa( STAMICO) akifafanua jambo akiwa kwenye banda la shirika hilo lililopo viwanja vy Mwalim Nyerere maarufu Sabasaba
 
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2