VIJANA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA ZILIZOPO SEKTA ZA MIFUGO, UVUVI | Tarimo Blog

Na Mbaraka Kambona,

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewahimiza vijana kuchangamkia fursa zilizopo katika Sekta za Mifugo na Uvuvi ili waweze kuzitumia kujikwamua kimaisha.

Ulega alisema hayo alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam Julai 5, 2021.

Akiwa katika maonesho hayo alisema kuwa vijana waitumie nafasi hiyo ya maonesho kwenda kujifunza fursa mbalimbali za kibiashara na za uwekezaji zinazopatikana katika sekta za mifugo na Uvuvi kwani Wizara ya Mifugo na Uvuvi mambo yake mengi ni ya uzalishaji na biashara.

"Kila  kitu Kilichopo katika Wizara hii ni fursa katika Biashara na ni fursa ya uwekezaji, hivyo tunawashauri vijana kutumia fursa hii ya maonesho kujifunza na kutumia elimu watakayoipata kuboresha maisha yao huko wanakoishi," alisema Ulega

Aliendelea kusema kuwa katika banda la Wizara hiyo kuna Wataalam mbalimbali ambao wanatoa elimu na mafunzo yanayohusu ufugaji, hivyo wakifika hapo watajifunza namna ya kufuga kuku, ng'ombe, mbuzi au Samaki kibiashara.

Aliongeza kuwa kuna vijana wengi wanaotafuta kazi lakini bado hawajafanikiwa, hivyo aliwashauri kwenda kujifunza fursa kubwa za kibiashara zitakazowasaidia kujipatia ajira na kukuza uchumi wa nchi pia.

"Serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Samia Suluhu Hassan imejikita katika kufungua milango ya biashara, kwa hiyo, hivi sasa wale wote wenye kiu ya kujifunza na kufanya kazi ya uzalishaji tunawakaribisha hapa ili waweze kufanya kazi hiyo ambayo itakuwa na manufaa sio kwao tu bali kwa taifa pia,"aliongeza Ulega

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ikiwemo Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) na Wakala ya Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kubuni mafunzo yatakayojumuisha watu wa elimu ya chini kabisa ambao wengi wao ni darasa la Saba.

Alisema kwa sasa vijana ambao hawajasoma wanakimbilia katika kuendesha Bodaboda kwa maana ndio njia wanayoiona rahisi ya kujipatia kipato huku akizitaka taasisi hizo kuja na mkakati maalum wa kuanzisha mafunzo ya kuwafundisha vijana hao fursa mbalimbali zilizopo katika sekta hizo mbili na wakazitumia kujiajiri na kufanya uzalishaji mkubwa utakaowezesha hata nchi kupata mapato.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akiangalia moja ya mbegu za malisho aina ya Juncao zinazozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 28- Julai13, 2021.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa Wadau wa Uvuvi kuhusu Samaki aina ya Kambakochi alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 28- Julai13, 2021. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel akimuangalia kuku wa mapambo kutoka Malaysia ambaye bei ya kumnunua ni Shilingi Laki Saba na Nusu. Prof. Ole Gabriel alimkuta kuku huyo katika moja ya mabanda ya Wadau wa Mifugo waliopo katika Banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 28- Julai 13, 2021.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) akielekeza jambo  kwa Maafisa wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) kuhusu machinjio ya Samaki aina ya Jodari alipotembelea Banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 28 - Julai 13, 2021.
 
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2