WANANCHI WILAYA YA LUDEWA WATAKA KUJUA KIKOMO CHA MICHANGO YA SHULE VIPAJI MAALUM | Tarimo Blog

Na. Shukrani Kawogo, Njombe.

Kufuatia kuwepo kwa malalamiko mengi ya wananchi wa wilaya ya Ludewa mkoani Njombe juu ya kukithiri kwa michango ya ujenzi wa shule ya vipaji maalum inayojengwa wilayani humo, mbunge wa jimbo la Ludewa aja na mkakati wa kuwapa ahueni wananchi hao.

Malalamiko hayo yametolewa katika maeneo mbalimbali aliyokuwa akipita mbunge huyo katika ziara yake ambapo wananchi hao wamedai kuwa wamekuwa wakichangishwa mara kwa mara na kila awamu kiwango kimekuwa kikiongezeka kitu ambacho kinapelekea michango hiyo kuwa kero kwao.

Christopher Luoga ni mkazi wa kijiji cha amani kata ya Mundindi amesema wanashindwa kuelewa mwisho wa michango hiyo ni lini maana wamekuwa wakichangishwa bila kupewa taarifa ya mapato na matumizi wala kuambiwa hatua iliyofikia  ya ujenzi huo.

" Mheshimiwa mbunge mimi naomba kufahamishwa michango hiyo tutachangia mpaka lini na kama serikali imeamua kutuachia wananchi tujenge wenyewe tujue maana hii michango ilianzia elfu moja moja kwa kila mwananchi ikawa inapanda kidogo kidogo na sasa imefikia shilingi elfu tano", Alisema Luoga.

Aidha kwa upande wa mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga amesema wamemshauri mkuu wa wilaya hiyo Andrea Tsere pamoja na mkurugenzi Sunday Deogratias na kukubaliana kuwa wananchi wamejitahidi kwenye ujenzi hadi shule imeonekana hivyo wenyeviti wa kijiji wanapaswa kubandika orodha ya majina na michango iliyotolewa na wananchi.

Amesema pia waliwasiliana na waziri pamoja na kamishna wa elimu ili shule hiyo ipate usajili na kuanza kupata bajeti za seriali kwakuwa wananchi hao katika maeneo yao wanatoa michango mingi ya maendeleo.

Sanjali na hilo mbunge huyo amesema kuwa aliwasilisha maombi TAMISEMI kuiomba serikali kumalizia maboma yaliyopo katika jimbo lake kwakuwa serikali imekuwa ikihamasisha wananchi kujenga maboma na inapofikia hatua ya kuezeka jengo la utawala serikali inaleta fedha kwaajili ya kumalizia maboma hayo.

Ameongeza kuwa katika kituo cha afya cha Mlangali seeikali ilileta Ml. 500, kituo cha afya cha kata ya Makonde Ml. 700 na Kata ya Milo Ml. 700 na sasa serikali imemuahidi kumalizia maboma 40 ndani ya jimbo hilo.

"Wananchi mmekuwa na moyo sana wa kujitoa katika kuchangia maendeleo ya ujenzi wa shule, zahanati na majengo mengineyo hivyo natoa wito kwa watendaji wa kata kupiga picha maboma yaliyopo na kuyafikisha kwa afisa mipango ili kuweza kuona uwezekano wa kuingiza katika maboma hayo 40.

Mbunge huyo mpaka sasa tayari amekwisha fanya ziara katika vijijji 28 na bado anaendea katika vijiji vingine ambapo lengo la ziara hilo ni kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

 Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph kamonga (aliyeshika kuku) akipokea zawadi ya kuku kutoka kwa kiongozi wa UWT kata ya Mundindi ambapo sambamba na kuku pia wamemzawadia mahindi kiasi cha gunia mbili.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga(kushoto) akimsikiliza mzee ambaye ana ulemavu wa macho ambaye amempa zawadi mbunge huyo zawadi ya mahindi debe moja, miwa pamoja na mkungu wa ndizi.
Diwani wa kata ya Mundindi Wise Mgina akizungumza na wananchi wa kijiji cha Amani katika mkutano wa mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kuwasili katika kijiji hicho kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi.
.
Katibu siasa na uenezi wa chama cha mapinduzi  wilaya ya Ludewa akizungumza wakati wa mkutano wa mbunge wa jimbo la Ludewa baada ya kufanya ziara katika kijiji cha amani kata ya Mundindi wilayani humo.
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Ludewa Stanley Kolimba akizungumza na wananchi katika ziara ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Amani kata ya Mundindi wakifuatilia mkutano wa mbunge baada ya kufanya ziara kijijini hapo.
Baadhi wa wakazi wa kijiji cha Njelela kata ya Mundindi wakiselebuka baada ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kuwasili katika kijiji uicho.

 


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2