Charles James, Michuzi TV
SIKU Moja baada ya Baraza la Mashirika yasiyokua ya kiserikali (NaCoNGO) kuzinduliwa rasmi, Serikali imelitaka baraza hilo kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na uzalendo pamoja na kusimamia miongozo na sheria za baraza hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ambaye ameuisisitiza uongozi uliochaguliwa kuhakikisha unakidhi matarajio ya waliowachagua.
Akizungumza jijini Dodoma leo wakati wa kupokea taarifa na kuzindua baraza hilo l NaCoNGO, Dk Gwajima amesisitiza uzalendo kwa Taifa na kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.
" Kwa Viongozi na wajumbe Wote mliochaguliwa nitoe rai kwenu kufanya kazi kwa bidii, weledi na kutanguliza uzalendo kwa Taifa lenu,lakini zaidi mkidhi matarajio ya wajumbe waliowachagua.
Mimi binafsi kama Waziri wenu niwahakikishia ushirikiano wa Serikali kupitia Wizara na sina shaka n uongozi mpya ila niwatake mhakikishe mnatoa ratiba mapema ya uchaguzi baada ya miaka mitatu ya uongozi huu kumalizika," Amesema Dk Gwajima.
Amesema baraza hilo toka mwaka 2019 lilikua mfu hivyo kuwataka Viongozi hao kutorudia makosa ambayo yalifanyika awali ya kuendesha baraza bila kufanya uchaguzi Ndani ya muda wa kikatiba.
" Ni wazi Baraza lilikua mfu tangu mwaka 2019 kwa sababu hakukua na uchaguzi wowote ulioitishwa kikatiba, hili Baraza ni kubwa na linaaminika, niwaombe muda wa uchaguzi wa kikatiba utakapofika ufanyike na ratiba itangazwe mapema," Amesema Waziri Gwajima.
Waziri pia amemtaka Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo, Lilian Badi kuhakikisha anasimamia vema baraza hilo hasa katika upande wa fedha ambapo amesema kwenye fedha hapakosekani na watu wenye mikono mirefu.
Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa NaCONGO, Lilian Badi amesema wanaahidi kufanya kazi kisayansi na kwa uadilifu mkubwa ikiwa ni pamoja na kuwajibika ambapo amedai wamedhamiria kuona NaCONGO inarudi katika ubora wake.
Badi amemhakikishia Waziri Gwajima kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali ya Rais Samia huku akimuomba kufikisha salamu zao kwake na kumpelekea ombi la kukutana na NaCoNGO.
" Malengo yetu ni kutoa mchango wetu kwa Nchi yetu, hatuwezi kuwa sehemu ya wanaohujumu na kukwamisha Nchi yetu, sisi uzalendo kwanza na tunaahidi kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.
Mhe Waziri tunaomba upeleke ombi letu kwa Rais Samia Suluhu Hassan, tunampa pongezi nyingi Sana kwa kasi kubwa aliyoanza nayo ya kuwatumikia watanzania na pia tufikishie ombi letu kwake la kuomba kukutana nae na kuzungumza nae," Amesema Badi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima akizungumza na viongozi na wajumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali NaCoNGO leo jijini Dodoma.
Aliyekua Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya NaCoNGO, Flaviana Charles akimpa Waziri Dk Dorothy Gwajima taarifa ya uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali NaCoNGO uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma.
Mwenyekiti mpya wa NaCoNGO, Lilian Badi akeleza mikakati yake mbele ya Waziri Gwajima leo wakati wa kikao Chao Cha pamoja na Waziri jijini Dodoma.
Wajumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGO) wakimsikiliza Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima alipofika kuonana na kuzungumza nao baada ya kufanya uchaguzi wa kuwapata Viongozi wapya wa baraza hilo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment