WAZIRI MKUU MAJALIWA AITISHA KIKAO NA VIONGOZI WA WIZARA KUJADILI TOZO ZA MIAMALA | Tarimo Blog

TUMESIKIA! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Serikali kusema kwamba imesikia malalamiko na maoni ya wananchi juu ya sheria mpya iliyopitishwa ya tozo za miamala ya Simu ambapo Waziri Mkuu ameitisha kikao cha kujadili jambo hilo.

Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba amesema jambo hili tayari limefika kwa viongozi wakuu wa Nchi ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitisha kikao baina yake na Wizara ya Fedha na Ile ya Mawasiliano kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi jambo hilo.

Dk Nchemba amesema kikao hicho kitafanyika kesho Jumanne hivyo kutumia nafasi hiyo kuwaomba watanzania kuendelea kuwa watulivu na kuisikiliza Serikali yao na siyo kusikiliza maneno ya watu ambao wamekua wakifanya upotoshaji mitandaoni.

" Niwaombe watanzania muwe watulivu, jambo hili limeshafika kwa viongozi wetu wakuu na Rais wetu Samia Suluhu Hassan ameguswa nalo na amesikia maoni ya watanzania hivyo tayari ameshatoa maelekezo kwetu ya kufanyia kazi hoja zote zinazotolewa na wananchi.

Tunaamini kupitia kikao na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kesho tutatoka tukiwa na muelekeo wa pamoja, kwa hatua ya Sasa niwasihi watanzania kuendelea kuwa na imani na serikali yao na kumuunga mkono Rais Samia katika utekelezaji wa majukumu ya kuijenga Nchi yetu," Amesema Dk Nchemba.

Ametoa rai kwa wale wote wenye nia ovu kuacha kufanya upotoshaji kwa wananchi na badala yake amewaomba watanzania kusikiliza maelekezo yote yanayotolewa na viongozi na kuahidi kuyatolea ufafanuzi na maelekezo mambo yote ya kikanuni.

" Rais Samia ana nia njema ya kuijenga Nchi yetu, ni jukumu letu kama wananchi kuendelea kumuunga mkono na siyo kusikiliza wababaishaji wanaofanya upotoshaji," Amesema Waziri Nchemba.

Kwa upande wake Waziri wa Habari na Mawasiliano, Dk Faustine Ndugulile amesema wizara yake itaendelea kushirikiana na wizara ya fedha katika kutolea ufafanuzi sheria hiyo huku akiwaondoa hofu wananchi na kuwahakikishia kuwa Serikali yao ni sikivu na inajali wananchi wake.

 Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2