NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA),Mkoa wa Mwanza,limewaasa watumishi wa Idara ya Mahakama na vyombo vya dola,kutenda haki kwenye kesi zinazohusu taasisi za dini ili kuondoa migogoro inayoweza kusababisha taharuki na uvunjifu wa amani.
Pia amewaonya waislamu mkoani humu wasiruhusu chokochoko zinazolenga kuwarudisha nyuma kwenye suala la maendeleo yao na uwe wimbo wa kila mmoja katika kufikia malengo waliyojiwekea lakini kwenye baadhi ya taasisi za kiislamu, kumeibuka jambo ambalo analiona, kadiri wanapofanya vizuri wapo watu wanazuia mazuri yasiendelee kufanyika.
Kauli hiyo imetolewa jana na Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke, wakati akifunga maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislamu ulioanza Agosti 10 mwaka huu na kutoa mwelekeo wa nini wanakihitaji katika mwaka mpya wa 1443 wa kiislamu.
Alisema baadhi ya watumishi wa Idara ya Mahakama waliokosa maadili na uaminifu wakiwemo wa vyombo vingine vya dola, wanapokea na kusikiliza mashauri yenye sura ya migogoro inayohusu taasisi za kidini kwa hila na kuwataka wawe makini ili wasijiingize kwenye migogoro hiyo na kuwa sehemu ya kuvunja amani.
Sheikhe huyo wa Mkoa wa Mwanza alidai baadhi wanapokea kesi zenye sura ya migogoro ya kidini na kusikiliza upande mmoja bila wadaiwa kuitwa kujitetea ilhali inahusu taasisi za kiimani,wamekosa maadili na uaminifu, wawe makini wanapotoa maamuzi bila kuathiri amani ya nchi.
“Niviombe vyombo vinavotoa haki mfano mahakama,kumekuwa na hila na ujanja ujanja unaotumika, mtu anawahi mahakamani,akifika baadhi ya watendaji waliokosa maadili na uaminifu,wanapokea kesi za aina hiyo na wanaambiwa tuiendeshe na isikilizwe upande mmoja,huyo Bakwata haambiwi,haitwi na hafahamishwi,na huyo hakimu anasikiliza kesi upande mmoja kwa siku moja wakati ni jambo linagusa hisia za umma,linaweza kuhatarisha uvunjifu wa amani,” alisema na kuongeza kuwa;
“Kwa unyenyekevu mkubwa nikiwa kiongozi wa waislamu Mkoa wa Mwanza, niwaombe baadhi ya watendaji wa mahakama,wawe makini na amani ya nchi,chonde chode na ni vizuri tukafahamiana amani hailindwi na mhimili mmoja tu wa serikali,kama jeshi,usalama wa taifa,polisi kwamba hao ndio wanahakikisha amani ya nchi inakuwepo au Rais, Waziri Mkuu,mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya,hapana, amani ya nchi inalindwa na vyombo vyote.”
Alisistiza kuwa taasisi za dini zinawajibu wa kulinda amani ya nchi, lakini alikwenda mbali zaidi kuwa Mahakama na Bunge pia vinawajibu huo,hivyo wanapopelekewa mashauri ya aina hiyo na watu kuwa Bakwata imeingia kwenye misikiti yao, hawaulizwi imeingiaje,Bakwata haihitwi na kuulizwa imekuwapo na inasimamia misikiti hiyo tangu lini, kunakuwa na walakini.
Alisema watu au mtu huyo aulizwe amekuwa kiongozi toka lini, kwa muda gani,aliwekwa na nani,lakini hakimu kuhukumu kesi hiyo bila kuzingatia hoja za pande mbili,inaweza kuleta athari na matatizo gani kwenye jamii, na kwamba baadhi ya taasisi za kiislamu wapo watu wanazuia maendeleo,pia wamechukua mali za BAKWATA na kuzikabidhi kwenye taasisi zingine kinyume.
Sheikhe Kabeke alisema kufanya hivyo wanazua mtafaruku,wanaleta mpasuko na migogoro,hivyo BAKWATA haitaki kuona mali za waislamu zinahamishiwa taasisi nyingine baada ya kuondoa mitafaruku,ugomvi baina ya waislamu, makundi na taasisi zote za kiislamu zimesimama pamoja,waislamu wamerudisha imani na wametoa mali na viwanja vyao na kuleta wakfu, wamejenga misikiti, kuisajili na kuikabidhi BAKWATA.
Mwenyekiti Mwenza huyo wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini aliviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuwa makini na matukio hayo,ni ukweli usiopingika kuwa wana baraza au viongozi wa BAKWATA hawatakubali kuona misikiti yao inachukuliwa na taasisi nyingine,hilo likiachwa bila kuangaliwa kwa macho makini litaleta mgogoro mkubwa.
“Mtu anakuja kusema msikiti huu ama kiwanja hiki hakina mtu,hakina mmiliki hivyo navikabidhi kwenye taasisi fulani ya kiislamu, wakati anafahamu kiwanja hicho au msikiti huo kwa muda wa zaidi miaka 30 kiko chini ya Baraza Kuu la Waislamu,sasa ukifanya hivyo maana yake wewe hauleti tu matatizo madogo,bali mtafaruku na mpasuko kati ya waislamu,”
“Bakwata inayosimamiwa na Mufti,tulijiwekea utaratibu,hatuko tayari kuona mali za waislamu kurudi tuliko toka,zinamilikiwa na watu wachache,mali na vitu vya waislamu vitaendelea kumilikiwa na kusimamiwa na waislamu lakini mtu anakwambia nataka kuusajili msikiti ndani ya taasisi yako,wewe kiongozi wa taasisi hiyo unakubali,unasema karibu unausajili,aha jambo ambalo humwulizi kwa miaka 15 msikiti huu upo ulikuwa chini ya taasisi gani?” alihoji Sheikhe Kabeke.
Aliziomba baadhi ya taasisi akisema mwaka 1442 walikwenda vizuri sana katika hali ya umoja na kuyashika maelekezo ya Mufti, basi wanaotaka kuvuruga wasiwalazimishe waislamu kuingia kwenye mitafaruku na ugomvi kwa kuwa waislamu ni kitu kimoja,na wanafahamu wakiingia kwenye mizozo isiyo ya lazima wanaweza kujenga kitu kibaya sana kikaharibu mazuri yote yaliyokwisha kufanyika.
Aidha alilishukuru jeshi la polisi kusimama imara kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa kwa kuwadhibiti wakorofi wanaoleta chokochoko katika baadhi ya maeneo,Mwanza imetulia na kuwaasa mwaka 1443 wasizue chokochoko na ugomvi wa kurudisha tena waislamu nyuma kwa yale yaliyosemwa zamani na kuonyooshewa vidole,kwani ndani ya Quran Mwenyezi Mungu amesema Shikamaneni katika dini ya Mwenyezi Mungu msifarakane.
Hivyo, mali ikiwa ya taasisi fulani ibaki ilivyo na iwe na ushahidi,ikiwa chini ya BAKWATA vivyo hivyo,asije mtu akasema nakuja kusajili msikiti kwenye taasisi yako na wewe kiongozi ukakubali bila kutafakari na kufanya utafiti, huko ni kusababisha chokochoko na uvunjifu wa amani. Aliongeza kiongozi wa dini ameamua kupaza sauti kulinda amani ya yetu nchi, waislamu na viongozi wa serikali,iwe mahakama na polisi wasikubali kuingia kwenye migogoro ya kuhatarisha amani na kuleta machafuko kwenye jamii,wasipokuwa makini wanapotoa maamuzi ya kesi zenye sura ya migogoro ya kidini, Bakwata haiko tayari kuona hata dhiraa moja ya mali yao inachukuliwa na taasisi zingine kinyume.
Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke (wa tatu kutoka kulia) akizungumza na waandishi wa habari jana wakati akihitimisha siku ya mwaka mpya wa 1443 wa Kiislamu.Picha na Baltazar Mashaka
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment