Serikali imesema kuwa barabara ya Makutano – Butiama – Nyamuswa sehemu ya Makutano – Sanzate (Km 50) kwa kiwango cha lami inayojengwa kwa ushirikiano wa wakandarasi wazawa 10 inatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, alipokuwa mkoani Mara wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.
Chamuriho, amefafanua kuwa mradi huo unaojengwa na Mkandarasi Mbutu Bridge JV kwa kushirikiana na wakandarasi wengine Tisa, umechelewa kukamilika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kubadilika mara kwa mara kwa michoro ya barabara hiyo na pia wakandarasi hao kuwa na uwezo mdogo wa kifedha na vifaa wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
“Wananchi wa Mkoa wa Mara, sasa tutarajie neema katika mkoa huu, barabara hii ipo ukingoni kukamilika, changamoto zilizokuwa zikikabili mradi huu zote zimekwisha, matumaini yangu kuanzia sasa kazi zitafanyika kwa haraka na mradi utakamilika kwa wakati”, amesema Chamuriho.
Aidha, Waziri Chamuriho amesema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutasaidia kupunguza gharama za usafirishaji kutoka eneo moja kwenda jingine na pia kutachochea biashara ya utalii kwenye mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro.
Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Butiama, Mheshimiwa Jumanne Saghini, amesema kuwa anashangazwa na ujenzi wa barabara hiyo kuchukua muda mrefu, hivyo ameiomba Serikali kumbana Mkandarasi ili aweze kumaliza mradi huo kwa wakati na hatimaye wananchi wake waweze kufurahia huduma za usafiri na usafirishaji kama watu wengine.
Naye, Mbunge wa jimbo la Bunda, Mheshimiwa Mwita Getere, ameiomba Serikali kuhakikisha inamkumbusha Mkandarasi kuweka alama za barabarani ili kusaidia masuala ya kiusalama kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Halikadhalika, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS)
mkoa wa Mara, Mhandis Ngaile Mlima, amesema kuwa mradi huo umefika asilimia 89 na kazi ambazo zimekwishafanyika ni pamoja na uondoaji wa tabaka la juu la udongo, upasuaji miamba na kujenga tuta kwa tabaka la chini.
Ameongeza kuwa kazi zinazofanyika sasa ni pamoja na usagaji wa mawe kwa ajili ya kokoto za tabaka la kati la barabara, kuweka tabaka la msingi la barabara, kutengeneza barabara za mchepuo, ufungaji wa mtambo mwingine wa kusaga mawe na maandalizi ya kuweka alama za michoro ya barabarani
Waziri Chamuriho amemaliza ziara yake ya kikazi mkoani Mara, ambapo pamoja na mambo mengine amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Musoma na miradi mbalimbali ya barabara na madaraja.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho (Wakwanza Kushoto), akimwelekeza jambo Mkandarasi Shen Song Tao (Katikati), anayejenga barabara ya Nyamuswa hadi Bulamba, alipofika mkoani Mara kukagua maendeleo ya mradi huo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho
(Kushoto), akiteta jambo na Mbunge wa Butiama, Mheshimiwa Mwita Getere, wakati Waziri huyo alipofika mkoani Mara kukagua maendeleo ya mradi wa barabara ya Makutano – Sanzate (Km 50).
Muonekano wa barabara ya Makutano – Butiama – Nyamuswa sehemu ya Makutano – Sanzate (Km 50) kwa kiwango cha lami, ambayo inajengwa na Mkandarasi mzawa Mbutu Bridge JV kwa kushirikiana na wakandarasi wengine wazawa Tisa. Barabara hii imefika asilimia 89 na inatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu.
PICHA NA WUU
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment