HONGERA KWA KUMBUKUMBU YA KUZALIWA MICHUZI | Tarimo Blog

Muhidin wa Michuzi, Issa ni jina la baba,
Siku hii twakuenzi, kwa maneno japo haba,
Kama wahitimu kozi, unazidi kuwa baba,
Hongera kwa kumbukumbu, siku uliyozaliwa.

Michuzi mengi twaenzi, kwa maisha yako baba,
Makubwa yale ya kazi, unazofanya si haba,
Tukifanya uchunguzi, kweli kaka umeshiba,
Hongera kwa kumbukumbu, siku uliyozaliwa.

Wewe ni mtangulizi, blogu zilizoshiba,
Watoto hata walezi, huko mengi wanashiba,
Kazi kazi si mapozi, tunakukubali baba,
Hongera kwa kumbukumbu, siku uliyozaliwa.

Wewe mwalimu Michuzi, wengi wakuita baba,
Tena mwajiri Michuzi, vijana kwako washiba,
Una upendo Michuzi, shida zinapotukaba,
Hongera kwa kumbukumbu, siku uliyozaliwa.

Mwandishi nguli Michuzi, na kwa picha umeshiba,
Kwa umma unayo dozi, huko unayo nasaba,
Ofisi yako Michuzi, pia wengi yatubeba,
Hongera kwa kumbukumbu, siku uliyozaliwa.

Ngekuwa mimi Michuzi, ngetaka niitwe baba,
Na ningeringa kichizi, kwa jinsi nilivyoshiba,
Wewe hunayo mapozi, heshima kwa wote baba,
Hongera kwa kumbukumbu, siku uliyozaliwa.

Tunakutana Michuzi, myaka mingi siyo saba,
Japo u bize Michuzi, salamu za kwako si haba,
Wajaa utu Michuzi, kukuiga si uzoba,
Hongera kwa kumbukumbu, siku uliyozaliwa.

Tunamuomba Mwenyezi, mema yale yameshiba,
Hayo yeye akujazi, sawa wema wako baba,
Na akupe utatuzi, mabaya yanokuziba,
Hongera kwa kumbukumbu, siku uliyozaliwa.

Kimataifa Michuzi, huko unatajwa baba,
Kitaifa we Michuzi, jina kubwa watubeba,
Sasa uandae kozi, vema tuweze kushiba,
Hongera kwa kumbukumbu, siku uliyozaliwa.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
28/8/2021

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2