WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wanaoishi katika makazi ya wakimbizi ya Mishamo Wilayani Tanganyika kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao kwa kutoa taarifa za watu wanaoingia eneo hilo kutoka nchini bila kufuata utaratibu.
Amesema eneo hilo limekuwa kimbilio la wahalifu wakiwemo wezi na wawindaji haramu hivyo amewasihi wakazi hao kusimamia ulinzi na usalama.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Alhamisi, Agosti 26, 2021) alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo na utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi katika Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi, Amesema Serikali haifurahii kuona wakazi wa maeneo hayo wanaruhusu watu wasiokuwa na vibali kuingia katika eneo hilo.
“Ninawaomba msimamie usalama katika eneo hili, Mshiriki kuzuia wenzenu wanaokuja kutoka nchi jirani hata kama ni ndugu zenu, kama hajaingia kwa kufuata utaratibu toa taarifa kwa Mkuu wa Makazi, lazima tushirikiane kuifanya nchi hii kuendelea kuwa na historia yake ya Amani na utilivu.”
Aidha, katika kuhakikisha wanasimamia suala la ulinzi na usalama, Waziri Mkuu amewataka wakazi hao watumie vikao vyao vya kijamii kukemea vitendo vya kihalifu na waelimishane juu ya umuhimu wa kulinda na kudumisha amani. Pia wahamasishane kufuata taratibu wakati wanapotoka na kuingia katika makazi hayo.
Awali Waziri Mkuu alitembelea kituo cha Afya Mishano ambacho Serikali ilitoa Milioni 400 ili kufanya maboresho na sasa kituo hicho kimejenga chumba cha upasuaji na wodi ya mama na watoto na amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuboresha miundombinu ya huduma za Afya katika maeneo yote nchini.
Akizungumzia maboresho ya kituo hicho ambacho pia kina uwezo wa kutoa huduma ya upasuaji wa dharula kwa akina mama, Mkazi wa Kijiji cha Mishamo, Stella Jonasi amesema awali kina mama walikuwa wanahangaika kwa kukosa sehemu ya kujifungulia hivyo kuwalazimu kusafiri kwa umbali mrefu hadi mpanda kufuata huduma hiyo.
Naye Emmanuel Kijumba, Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha Kituo hicho pamoja na kuongeza idadi ya Madaktari, wauguzi na kuwezesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment