Vyuo vya uhandisi vyatakiwa kuongeza udahili wanafunzi | Tarimo Blog

RAI imetolewa kwa vyuo vinavyofundisha masomo ya uhandisi nchini kuongeza udahili wa wanafunzi ili kukidhi hitaji la soko.

Ombi hilo limetolewa na Msajili wa Bodi ya Usajili Wahandisi (ERB), Mhandisi Patrick Barozi wakati wa mjadala wa Kongamano la Wahandishi Vijana lilifanyika jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Barozi alisema ERB hadi sasa imesajili wahandisi 31,729 wanawake wakiwa 3,344 idadi ambayo ni ndogo kulingana na hitaji lao kwa jamii.Alisema kulingana na idadi ya Watanzania idadi hiyo haitoshi kutekeleza miradi hivyo ni jukumu la vyuo vinavyofundisha masomo hayo kuongeza udahili.

"Hadi sasa ERB imesajili wahandisi 31,729 ambao wamehitimu kwenye vyuo vyetu kama Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kitivo cha Uhandisi (CoET), Taasisi ya Tenkolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo cha Ufundi Arusha, Chuo cha St.Joseph na vingine," alisema.

Msajili alisema iwapo vyuo hivyo vitaongeza udahili Tanzania itakuwa na wahandisi wengi wa fani mbalimbali ambao watasaidia kwenye uzalishaji na kukuza uchumi.Alisema wameamua kuandaa kongamano hilo la wahandisi wa vijana ili kuwawezesha kubaini fursa na changamoto katika kufanikisha mapinduzi ya nne ya viwanda.

Barozi alisema kongamano hilo lililenga kuonesha umma kundi hilo muhimu kwa maendeleo ya nchi na kuleta tija kwa vijana wahandisi."Pia tunaamini jukwaa hilo litachochea bunifu mbalimbali zinazobuniwa na vijana hao na namna ya kuziendeleza," alisema.

Barozi alisema wahandisi vijana wamekuwa wakitumika katika miradi mbalimbali kama ujenzi wa reli, madaraja, barabara, viwandani, umeme na maji jambo ambalo linatoa matumaini.Alisema kauli mbiu ya kongamano hilo ni fursa na changamoto kwa mhandisi kijana katika kufikia mapinduzi ya nne ya viwanda, hivyo ni imani yao ni kuona vijana hao wananufaika nayo.

Msajili alisema ERB imejipanga kuandaa kongamano la wahandisi vijana kila mwaka ili kuwaandaa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kabla ya kuajiriwa au baada ya kuajiriwa.Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Profesa Ninatubu Lema aliwataka wahandisi hao kujiuliza watafanyia nini jamii ili kuchangia mabadiliko ya kiuchumi, viwanda na maendeleo.

Alisema wahandisi vijana ni kundi muhimu katika kuchochea mabadiliko na maendeleo nchini hivyo wakiamua kutumia taaluma zao kwa weledi mafanikio yatapatikana."Napenda kuwaasa vijana wangu mfanye kazi kwa uhakika ili uache alama itakayokumbukwa milele na sio kukimbilia kujinufaisha wenyewe," alisema.

Mwenyekiti huyo alimtolea Mhandisi Lulu Dunia ambaye anasimamia Mradi wa Daraja la Tanzanite kuwa ameonesha mafanikio makubwa hivyo anapaswa kuigwa.Wakizungumzia kongamano hilo wahandisi vijana Samwel Sumari, Neema Njanga, Emmanuel Lazaro na Getrude Christopher wamesema ni muhimu kwao na linapaswa kuwa endelevu.

Wahandisi hao wamesema kongamono hilo limewafungua kwa kutambua fursa zilizopo kwenye sekta hiyo na namna ya kujiajiri ili kusaidia kukuza uchumi na maendeleo nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Profesa Ninatubu Lema akizungumza na wahandisi vijana kwenye Kongamano lililofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.
Msajili wa Bodi ya Wahandisi (ERB) akizungumza na wahandisi vijana kwenye Kongamano lililofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.
Wahandisi Vijana wakiwa kwenye Kongamano liloandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), lilifanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.
Wahandisi Vijana wakiwa kwenye Kongamano liloandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), lilifanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2