MIRABA YA WASANII INAHITAJI UTASHI WA WADAU | Tarimo Blog

 


 

……………………………………………………………………….

ADELADIUS MAKWEGA,WHUSM–DODOMA

Suala la kulipwa kwa mirahaba ya kazi mbalimbali za sanaa limepamba moto, huku wizara zinazohusika na jambo hili na wadau wote wa wasanaa wakiwa katika mkao wa kusubiri kutekelezwa kwa zoezi hilo nchini Tanzania.

Hiyo haina maana kwamba suala hili ni geni kwa Watanzania lahasha, linafahamika na wengi ndiyo maana kilio cha kuwa na mirahaba hiyo kimekuwa cha muda mrefu na sasa pengine jawabu lake linakuja kupatikana.

Katika kila kona kumekuwa na mijadala juu ya baadhi ya wadau kama vile maduka, mabasi, saloon na kumbi za starehe namna watakavyoweza lipia huduma hiyo pale watakavyocheza hizo kazi za sanaa.

Hiyo ni hatua kubwa sana kwa taifa letu. Kwani wasanii wa muziki kama vile Mbaraka Mwinshehe, Bi Fatuma Binti Baraka (Bi Kidude), The Kilimanjaro Band, Kwaya ya Injili ya Kijitonyama ni baadhi tu kazi za sanaa za Kitanzania ambazo kwa kiasi walionufaika hata kwa kiasi kupata manufaa kutoka makampuni ya nje ya Tanzania waliokuwa na mikataba nayo.

Je unakumbuka michoro na vinyago vya mashetani vya Mzee Lilanga? Kumbuka katuni za Christian Gregory (Chakubanga)?, fikiria michoro ya gazeti la Sani kama vile katuni za zake za Lodi Lofa, Kipepe, Kifimbo Cheza ambalo ni gazeti linalomilikiwa na familia ya akina Bawji Athumani Mbwana ? Hizo ni sehemu tu ya kazi za sanaa ambazo zimefanywa na Watanzania ambao pengine kunufaika kwao ni thumuni tu ya manufaa yote. Wengine wakifa na kuzikwa na ndoto hiyo katika makaburi yao.

Tuutazame mfano wa kwanza kwa mashirika ya kimatifa; Vyombo Habari vya Kimataifa kwa mfano DEUSTCHE WELL ambapo mie kiasi ninaelewa mazingira yake kidogo, pale makao makuu ya DW Bonn, wao kazi zote za muziki zilizokuwa katika santuri au kaseti ambazo zilikuwa katika analogia zimehifadhiwa katika maktaba ya digitali.

Ndiyo kusema maktaba ya analogia ipo lakini inakuwa kama makumbusho ya kueleza maendeleo ya sayansi na tekinolojia. Katika maktaba ya digitali kila mtangazaji au mtayarishaji wa kipindi katika studio au ofisini kwake anaweza kuingia katika maktaba hiyo na kutafuta iwe wimbo, filamu au chochote kwa nywila maalumu aliyopewa.

Kila kazi sanaa imepewa nambari ya utambulisho ambapo unaweza kuitafuta kwa kutumia jina la kazi au jina la msanii-Kwa mfano wimbo Kijiti wa Siti Bint Saad nambari yake 2347899.

Mtayarishaji wa kipindi anapotayarisha kipindi chake anawajibu wa kuandika muswada wa kipindi. Kwa mfano Kipindi ni Jukwaa la Manufaa, Mtayarishaji ni Ndugu Sudi Mnete, Muda wa kipindi ni Dakika 9 na sekunde 8, Nyimbo zinazochezwa 1.Kijiti-Siti Bint Saad-2347899(Itachewza sekunde 55) 2.Ambush in the Night-Bob Marley 186777 (itachezwa Sekunde 80).3.Alfonsina-Oliver Ngoma (Itachezwa sekunde 70).

Hapo sasa miswada ya yote ya vipindi inakusanywa kwenye mtandao na Mkuu wa Idhaa kwa nyimbo zote zilivyochezwa zinahesabiwa malipo kulingana na mkataba. Huku makampuni yenye mikataba na redio hii yanafuatilia kujua kama mmecheza nyimbo zao na mwisho mnalinganisha taarifa malipo yanafanyika, hapo hakuna ujanja wowote ukicheza lazima ulipe. Mathalani DW wameilipa Sony  nayo inawalipa wanamuziki wake au walithi.

Nakumbuka kwa DW Kiswahili Bi Andrea Schmidt kuna wakati ndiye aliyekuwa mkuu wa idhaa hiyo na msaidizi wake alikuwa ni Mohammed Abdul-Rahman hawa jamaa walikuwa wakisisitiza na wakifuatilia juu jambo hili, je wimbo uliochezwa upo katika maktaba. Wanafuatilia kwa sababu moja kukwepa migogoro ya kisheria na kushitakiwa kucheza kazi za wasanii bila ridhaa zao.

Nachotaka kusema leo ni jambo moja tu suala la kulipwa mirahaba kwa wasanii siyo suala la sheria au kanuni tu,ni suala linalohitaji ushirikiano na nia njema ya pande zote. Upande wa wasanii na wale wanaocheza au kuzitumia kazi hizo

Sheria inaweza kuwepo na mazingira yakawekwa ili kazi hiyo ifanyike lakini wimbo wako usichezwe redio, runinga au kwenye ukumbi fulani ya starehe. Katika mazingira kama haya hiyo sheria au kanuni itasaidia nini? Ili kukwepa gharama ya kulipa mirahaba redio inaweza kuamua kucheza nyimbo za nje ambazo hazifungwi na sheria na kanuni hizo, Je unafanyaje katika mazingira kama hayo?

Sasa hivi vyombo vya habari ni biashara, inawezekana kazi ya sanaa ya msanii fulani haina wapenzi au ikichezwa idadi ya Watazamaji au wasikilizaji inapungua hapo inakuwaje ? Kwa hiyo kazi hiyo haitochezwa. Watakaonufaika ni wasanii wenye majina makubwa na maarufu tu, hata kuibuka kwa wasanii wapya itakuwa kazi kubwa.

Tuangalia mfano wa Redio Tanzania Dar es Salaam(RTD); Hapa Tanzania enzi za RTD waliwahi kuwa na kipindi cha Salaam za Wagonjwa kipindi hiki ni miongoni mwa vipindi maarufu vya RTD na kilikuwa hewani kila jumapili saa 4.02 hadi 5.00 Asubuhi.

Kipindi hiki kiliendelea hata baada ya RTD Kuwa TBC Taifa lakini baadae kilipotea kimyakimya nyuma ya pazia kukiwa na jinamizi ya mirahaba kwani marehemu Omari Kungubaya wakati wa mwisho wa uhai wake alilalamikia kutolipwa chochote kwa sauti yake na kupiga gitaa la galatoni katika kiashiria cha kipindi hiki.

Kulikuwa na madai kuwa sawa Mzee Kungubaya ndiye aliyeifanya kazi hiyo lakini alilipwa fedha kutokana nayeye kukirekodi kiashiria hicho cha kipindi.

Hiyo ni kweli lakini swali ni moja je kiasi alichopewa kinaweza kulingana na thamani ya kazi yake iliyotumika miaka mingi na RTD?

Baadaye kiashiria hicho kilifanyiwa marekebisho kwa midundo ya kisasa kwa maudhui yaleyale lakini hakikuwa na mvuto. Mwisho wa siku kipindi kilisuasua kwa jinamizi lilelile la Marehemu Omari Kungubaya.

  • Wakati umewadiwa
  • Wa salamu za wagonjwa
  • Hospitalini
  • Leo tunawapa pole x2
  • Ajuaye Bwana Mungu
  • Kwa mzima kuwa mfu
  • Mgonjwa kuwa salama
  • Leo tunawapa pole x2
  • Kipindi chenu kinawapa pole
  • Wote tunawapa pole
  • Mungu awajalieni pole x2
  • Tunawapa pole x2.

Panaweza pakawepo na sheria, kanuni na miongozo ikabaki katika masanduku ya ofisini hakika kwa kutumia mifano hiyo miwili ule wa DW na RTD juu mirahaba kwa wasanii  inahitaji utashi wa wadau ili kila upande uwe salama na usiwe mfu kama kilivyokufa kipindi cha salaam za wagonjwa.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2