Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Mwigulu Nchemba akizungumza wakati wa maadhimisho ya nne ya Siku ya Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu Barani Afrika na kuwataka wananchi kushiriki zoezi hilo muhimu linaloendeshwa kote nchini kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA,) Leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia mjadala.
Kaimu Mkurugenzi wa Ulinzi wa Haki za Kisheria kutoka RITA Lina Msanga akizungumza wakati wa maadhimisho hayo na kueleza kuwa Tanzania imekuwa kinara wa usajili wa matukio mbalimbali barani Afrika na kupata fursa ya kutoa mada katika nchi mbalimbali za Afrika juu ya namna bora ya sajili zinazofanyika, Leo jiji Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya RITA Khamis Duhenga akizungumza katika maadhimisho hayo na kueleza kuwa wakala hiyo itaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa usajili wa matukio muhimu, leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa shirikisho la vyama la watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA,) Tulia Mwantala akizungumza wakati wa maadhimisho hayo ambapo amemuomba Waziri kabudi kuangalia namna ya kutatua changamoto ya miundombinu na wakalimani kwa kundi hilo pindi wanapopata huduma.
WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA,) umepongezwa kwa kuendelea kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwasijili pamoja na kupiga hatua kubwa zaidi ya kutumia teknolojia ya simu za mkononi kutoa taarifa za watoto waliozaliwa na kusajiliwa katika vituo vya afya na ofisi za watendaji wa kata jambo lililoongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya kazi hasa wakati huu ambao dunia inapambana na janga la UVIKO-19.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya nne ya Siku ya Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu Barani Afrika yanayoadhimishwa Agosti 10 kila mwaka Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi amesema zoezi la usajili linalofanywa na wakala hiyo ni muhimu na hufanyika kote nchini ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango ya kuwahudumia wananchi na imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali na kuleta matokeo makubwa ambayo pia yanategemewa kupatikana kupitia sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka ujao.
Aidha amesema mpango wa Usajili wa vifo ambao unatekelezwa sambamba na usajili wa watoto unasaidia kutambua idadi ya vifo vinavyotokea nchini sababu za vifo pamoja na kuboresha huduma za afya sehemu mbalimbali na kuitaka wakala hiyo kutoa elimu zaidi kwa jamii kuhusu umuhimu wa uwekaji wa takwimu za matukio muhimu ya binadamu ya vifo, vizazi, ndoa na watoto wa kuasili.
Kabudi amesema, licha kuwepo na changamoto ya janga la UVIKO-19 RITA imepiga hatua kubwa hasa katika matumizi ya teknolojia katika utoaji huduma ambapo hadi sasa huduma nyingi zinazotolewa na wakala hiyo zinatolewa kwa njia ya mtandao wa simu ikiwemo huduma za usajili wa vizazi na vifo kwa kukamilisha maombi kwa njia ya kieletroniki bila kufika ofisi za RITA.
Amesema mikoa 20 tayari imesajili watoto walio chini ya miaka 5 zaidi ya milioni sita na kufikia asilimia 55 kutoka asilimia 13 mwaka 2012 kupitia mpango mkakati wa usajili aliouzindua mwaka 2018 na kutoa matokeo chanya kwa sehemu nyingi nchini kusajili watoto wengi ikiwemo mikoa ya Mara na Simiyu ambayo ndani ya miezi minne ilisajili watoto na kufikia asilimia 80 kutoka asilimia 10 za awali.
Sambamba na hayo Prof. Kabudi amesema katika suala la ndoa sio kila kiongozi wa dini anaruhusiwa kufungisha ndoa kwani kisheria ni mpaka kiongozi huyo awe amesajiliwa na RITA tofauti na hapo ndoa hiyo ni batili.
Aidha amewaomba viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu waliohudhuria katika semina hiyo kuhakikisha kuwa wanatoa maoni ambayo yataboresha haki za watu wenye ulemavu na kuondoa changamoto wanazokabiliana nazo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Ulinzi wa Haki za Kisheria RITA Lina Msanga amesema maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila Agosti 10 barani Afrika yanalenga kuongeza mwamko na kasi ya wananchi ya kusajili matukio muhimu na yanafaa kupewa kipaumbele kwani yanasaidia nchini kufanya mambo ya maendeleo, na Tanzania imekuwa nchi ya mfano barani Afrika na wamekuwa wakialikwa kutoa mada mbalimbali juu masuala ya usajili.
Hata hivyo amesema kauli mbio ya maadhimisho hayo ni uongozi kwa huduma muhimu kujenga mifumo imara ya usajili wa matukio muhimu ya Binadamu Afrika inayowezesha ubunifu jumuishi na inayogatua utoaji wa huduma baada ya kipindi cha Covid 19 ambayo inatekelezwa na Umoja wa Afrika (AU) kwa nchi zote Barani Afrika.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment