SHAKA APOKEA TUZO YA RAIS SAMIA KWA KITUO CHA SANAA NA UTAMADUNI CHA VIZIWI TAZANAIA (KISUVITA) | Tarimo Blog

 

Uongozi wa kituo cha sanaa na utamaduni cha viziwi Tanzania (KISUVITA) umempa tuzo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wake katika kuhakikisha haki na usawa wa fursa kwa watu wenye ulemavu nchini ikiwemo kuwawezesha kufanikiwa kushiriki mashindano ya kidunia ya mitindo na urembo Moscow nchini Urusi. 

Tuzo hiyo imewasilishwa na kupokelewa na katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka ofisi ndogo za CCM Lumumba, Dar es Salaam kwa niaba ya Rais Samia.

Wakati wa makabidhiano hayo Katibu mtendaji wa kituo hicho Ndugu Habibu Mborobe amesema wanampongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi mahiri unaowashirikisha, kuwajumuisha na kuwathamini watu wenye ulemavu. 

Wakati wa makabidhiano hayo Katibu mtendaji wa kituo hicho Ndugu Habibu Mborobe amesema wanampongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi mahiri unaowashirikisha, kuwajumuisha na kuwathamini watu wenye ulemavu. 

Akizungumza na ujumbe huo Shaka alisema CCM kupitia katiba yake ibara ya 4 (1)&(2) pamoja na ilani yake ya uchaguzi ibara ya 95 imeeleza wazi kuwa binadamu wote ni sawa hivyo wanastahili kuheshimiwa utu wao bila kubaguliwa kwa rangi, jinsia au maumbile yao. Kwa mantiki hiyo CCM itahakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa, wanaheshimiwa, wanathaminiwa na wanajumuishwa katika mipango na programu mbalimbali za maendeleo ya nchi yetu na serikali.

Aidha ameeleza katiba ya Tanzania Ibara ya 12 inawalinda watu wenye ulemavu hivyo serikali itaendelea kuchukua hatua kadhaa za kuhakikisha misingi madhubuti inawekwa katika kupanga na kutekeleza programu za maendeleo zinazolenga kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu ikiwemo kufahamu takwimu za kundi hili muhimu. 

Aliwaeleza bajeti ya serikali ya mwaka 2021/22 imetenga takribani bilioni 1.6 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa visaidizi kwa watu wenye ulemavu kwenye shule zote nchini. Serikali imeendelea kuhimiza wataalam wa lugha za alama kuwepo kwenye kila tukio ambalo umma unafuatulia ili kuwapa haki watu wenye ulemavu ya uziwi kupata habari.

Vile vile CCM itaendelea kutoa msukumo kwa serikali kuhakikisha watu wenye ulemavu wanaonufaika na mikopo isiyo na riba itokanayo na asilimia 2 za halmashauri bila vikwazo vyovyote.

"Katika kujenga jamii yenye usawa na fursa kwa wote CCM itaendelea kutoa rai na msukumo kwa serikali na sekta binafsi kutambua kuwa watu wenye ulemavu wanayo ndoto na malengo makubwa hivyo wakishirikishwa, wakijumuishwa na wakiungwa mkono kwa kuwekewa mazingira mazuri na wezeshi wana mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa."

Shaka amewashukuru KISUVITA kwa kumpa tuzo Rais Samia ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake kwa watu wenye ulemavu nchini.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2