NAIBU WAZIRI CHANDE AWAONYA WANAOFANYA SHUGHULI ZA KIBINADAMU NDANI YA MITA 60 KUTOKA KWENYE VYANZO VYA MAJI | Tarimo Blog


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Hamad Chande (katikati) akikagua daraja linalotengenezwa baada ya lile la awali kusombwa na mafuriko kwenye mto Furua.

Mhe. Naibu Waziri Chande akiwa na Wananchi kukagua eneo ambalo ni mto Furua uliacha asili yake na kusababisha mafuriko kwenye kijiji cha Misegese Wilaya ya Malinyi Mkoa wa Morogoro.

Naibu Waziri Chande akiwa kwenye ziara ya kukagua athari za mafuriko kwenye kijiji cha Misegese Wilaya ya Malinyi Mkoa wa Morogoro.

Wa kwanza kutoka kushoto ni Meneja kanda ya Morogoro Rufiji Bi. Amina Kibola akifuatilia maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri (hayupo kwenye picha)kwenye kikao cha kupokea malalamiko ya Wananchi wa Wilaya ya Malinyi kuhusu adha wanayoipata ya mafuriko ya mara kwa mara.

Mbunge wa jimbo la Malinyi Mhe. Antipas Zeno akielezea kero zinazolalamikiwa na Wananchi Wilaya ya Malinyi kwenye kikao kilichofanyika kwenye kijiji cha Misegese

………………………………………………………………….

Morogoro,

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Hamad Chande amewaonya wanaofanya shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji waache mara moja ili kudhibiti athari za uharibifu wa mazingira kama mafuriko.

Ameyasema hayo wakati akiongea na wakazi wa kijiji cha Misegese kilichopo Wilayani Malinyi mkoani Morogoro. Kijiji hicho kinakabiliwa na mafuriko  kwa miaka mitano mfululizo kutoka kwenye mto Furua, imeelezwa kuwa mafuriko hayo yamesababishwa na shughuli za kilimo na ufugaji zinazofanywa ndani ya mita 60 kutoka kwenye mto huo.

“Kutunza mazingira iwe ni sehemu ya utamaduni wetu, kufanya shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji ni kuharibu mazingira na Serikali inapata hasara kugharamia miundo mbinu inayoharibiwa na mafuriko,  hivyo naviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuzuia wote wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye mto Furua ili kuzuia athari hizi zisiendelee kujitokeza.

Wakati huo huo Naibu Waziri Chande amewasihi wananchi wa kijiji cha Misegese kuwa wavumilivu wakati Serikali ikijiandaa kutatua tatizo hilo.

“Nawaagiza Wataalamu kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC, baada ya muda mfupi kuanzia sasa warudi kwa ajili ya kutathmini namna ya kurejesha mto kwenye asili yake hivyo nawaomba wananchi muwe wavumilivu”.

Aidhaa Mhe. Chande ameongeza kuwa taka ni fursa ya ajira, wananchi wanapaswa kutumia taka na kuzibadili kuwa bidhaa kwani hiyo itasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira nchini.

” Natoa rai kwa wananchi kuchukulia taka kama njia ya kujiingizia kipato kwa kuzibadili kutoka taka mpaka kuwa bidhaa zingine, jambo hili litasaidia kutunza mazingira yetu yawe safi na salama”.

Nae meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Kanda ya Morogoro Rufiji Bi. Amina Kibola amesema maagizo aliyoyatoa Mhe. Naibu Waziri watayafanyia kazi kwa kurudi kwa ajili ya kutathmini eneo lililoathirika na mafuriko na kuangalia namna ya kulikabili ili athari hizo zisiendelee kujitokeza.

Bi. Amina ameongeza kuwa ni lazima sasa Wananchi wafuate miongozo, taratibu na sheria za matumizi bora ya ardhi ili kulinda mazingira yetu.

Naye Katibu Tawala Wilaya ya Malinyi Bw. Bahati Joram amesema Wilaya ya Malinyi imekuwa inakumbwa na mafuriko kwa miaka mitano mfululizo jambo ambalo linaleta adha kubwa kwa wananchi pamoja na uharibifu wa miundombinu hasa ya barabara. Hivyo wamepokea maagizo ya yaliyotolewa na Naibu Waziri Chande ya kuwaeleimisha wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka mto Furua, na watakao kaidi hatua za kisheria watachukuliwa.

Naye Mbunge wa Malinyi Mhe. Antipas Zeno amemuomba Naibu Waziri Mhe. Chande kuyatafutia ufumbuzi matatizo malalamiko ya Wananchi wa jimbo la Malinyi hasa kuleta watalaamu waje kutathmini chanzo cha tatizo la  mafuriko na namna ya kulitatua.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2