TAASISI Ya Furahika Education College Organization imetangaza fursa ya masomo ya ufundi na maarifa bure kwa watoto wa kike wenye elimu ya darasa la saba na kidato cha nne ili kuwawezesha katika kujikwamua kiuchumi na kuwa msaada kwa familia zao na taifa kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo David Msuya amesema kuwa, taasisi hiyo imekuwa ikishiriki katika masuala mbalimbali ya elimu, afya, haki za watoto na wanawake pamoja na mazingira na kupitia huduma ya elimu bila malipo inatotolewa na taasisi hiyo kwa mwaka 2021 tayari wamefungua dirisha la kuwapokea wanafunzi wapya kutoka Halmashauri mbalimbali nchini ili waweze kujiunga na kupata mafunzo mbalimbali ya elimu na ujuzi wa ufundi na maarifa ikiwemo mafunzo ya hoteli, kompyuta, ushonaji na muziki na kuwa msaada kwa familia na jamii kwa ujumla.
Msuya amesema, fomu za kujiunga na chuo hicho zinapatikana katika website ya chuo 'Furahika Education College' na kwa wanafunzi watakaowahi kujisajili watapata huduma za hosteli bure.
''Chuo chetu hakipokei malipo yoyote isipokuwa ada ya mtihani, chakula kwa wanaafunzi ni bure na tunathamini watoto wa kike na tumewajengea bafu maalumu kwa ajili ya kujisitiri.....Hivyo wanafunzi watakaowahi kujisajili watapata huduma za malazi bure kabisa na kwa wale watakaokosa watapokelewa kama wanafunzi wa kutwa, Niwaombe wazazi na walezi kutumia nafasi hii kuwaleta watoto kupata elimu na kuwaepusha na changamoto mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni.'' Amesema Msuya.
Aidha Msuya amesema wanafunzi watapata ujuzi, maarifa ya maendeleo ya viwanda ili waweze kuajiriwa na kujiajiri wenyewe na wamelenga kutoa wahitimu 200 kila mwaka huku akieleza kuwa wahitimu wengi wa kozi za hoteli na kompyuta tayari wamepata ajira kupitia mchango wa Halmshauri mbalimbali nchini.
Vilevile amesema, changamoto kubwa inayowakabili katika taasisi hiyo ni ukosefu wa taulo za kike kwa wanafunzi na kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza na kushiriki katika upatikanaji wa taulo hizo zitakazowaweka salama zaidi wakati wote wawapo masomoni.
Halmashauri zilizopata fursa za kuwapelekea watoto wa kike kupata mafunzo katika taasisi hiyo ni pamoja na Halmashauri za mkoa wa Dar es Salaam, Kisarawe, Kibaha Mji, Geita, Shinyanga, Kahama, Bukombe, Masasi, Tandahimba, Iringa Mjini, Mtwara, Morogoro, Kilosa na Kilombero.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment