WAZIRI MULAMULA KUONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KWENYE MKUTANO WA NNE WA TUME YA PAMOJA YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA KENYA. | Tarimo Blog



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ataongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (Joint Commission for Cooperation-JCC) kati ya Tanzania na Kenya unaofanyika jijini Nairobi, Kenya kuanzia tarehe 19 hadi 24 Agosti, 2021.

Akiwa nchini Kenya, Mhe. Balozi Mulamula anatarajiwa kukutana kwa mazungumzo na Mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Balozi Raychelle Omamo tarehe 23 Agosti 2021 pamoja na kutembelea Chuo cha Ulinzi cha Taifa cha Kenya ambapo atatoa mhadhara kwa mada isemayo “Mtazamo wa Tanzania kwenye Agenda ya Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama”.

Mkutano huu ulioanza katika ngazi ya wataalam tarehe 19 hadi 22 Agosti 2021, umeongozwa na Balozi Naimi Aziz, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki huku upande wa Kenya ukiongozwa na Balozi George Orina, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika na Umoja wa Afrika.

Pamoja na mambo mengine Mkutano wa Wataalam umejadili agenda mbalimbali za ushirikiano ambazo zitawasilishwa kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kitakachofanyika tarehe 23 Agosti 2021 kabla ya Mkutano wa Nne wa Tume ya Ushirikiano kuhitimishwa na Mkutano wa Mawaziri tarehe 24 Agosti 2021.

Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano utashuhudia uwekwaji saini wa hati tatu (3) za makubaliano (Memorundum of Understanding – MoU) ambazo ni; Hati ya Makubaliano ya Mashauriano ya Kisiasa na Kidiplomasia. Kusainiwa kwa kwa makubaliano haya kutaendeleza na kuimarisha mahusiano mazuri ya kisiasa na kidiplomasia yaliyopo kati ya Tanzania na Kenya.

Hati nyingine itakayosainiwa ni kuhusu Uhakiki wa Mpaka kati ya Tanzani na Kenya. Kusainiwa kwa Hati hiyo kutazipa Nchi zote mbili msingi wa kisheria wa kuhakiki mpaka uliowekwa na wakoloni kwa kuuimarisha na kuweka alama zinazoonekana ili kuondoa mwingiliano wa jamii za mpakani na hivyo kupunguza migogoro ya mara kwa mara.

Mwisho ni Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia. Hati hii inalenga kuanzisha ushirikiano kati ya taasisi za pande zote katika maeneo ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ili kuleta manufaa kwa nchi zote katika kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo wa masuala ya elimu ya juu, Sayansi na teknolojia kwa pande zote.

Tanzania na Kenya zimeendelea kutekeleza masuala mbalimbali ya ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji, siasa na diplomasia, elimu, uhamiaji, utalii, kazi, afya, usafirishaji, ulinzi na usalama.

Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ilianzishwa rasmi mwezi Septemba 2009 jijini Arusha, Tanzania na kufuatiwa na Mkutano wa Kwanza wa Tume hiyo uliofanyika jijini hapo mwaka 2009. Mkutano wa Pili wa Tume hiyo ulifanyika jijini Nairobi, Kenya mwezi Septemba 2012 na Mkutano wa Tatu ulifanyika jijini Dar es Salaam mwezi Desemba 2016.

Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya unafanyika ikiwa ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Uhuru Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya walipokutana wakati wa ziara ya Mhe. Rais Samia iliyofanyika nchini Kenya mwezi Mei 2021.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2