RAIS SAMIA: SITAKI NIWAFICHE MAKATO TOZO ZA MIAMALA TUTAENDELEA KUCHUKUA,TUMEPUNGUZA KWA ASILIMIA 30 | Tarimo Blog


*Aahidi kutekeleza miradi yote iliyoachwa na Magufuli, agusia hulka ya wanadamu


Na Said Mwishehe, Michuzi TV

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema anatambua kuwa baada ya bajeti ya Serikali kupitia makato ya tozo kwenye miamala ya simu kumekuwepo na malalamiko mengi, hivyo Serikali imeamua kupunguza kwa asilimia 30 lakini akaweka wazi makato hayo yataendelea kuwepo na wala hawezi kuficha.

Ameyasema hayo leo Septemba 2,2021 akiwa eneo la Tegeta katika Jimbo la Kawe mkoani Dar es Salaam akiwa safari kuelekea Bagamoyo mkoani Pwani ambako anakwenda kwa ajili ya kurekodi filamu inayozungumzia mila, desturi na tamaduni za Mtanzania.

Akiwa anazungumza na wananchi hao wa Jimbo la Kawe Rais Samia amesema Serikali ya Awamu ya Sita ina mambo mengi wanaendelea kuyafanya ikiwemo ya kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ambayo iliachwa na Serikali ya Awamu ya Tano ambayo amewahakikishia Watanzania kuwa miradi hiyo lazima itatekelezwa kama ilivyokusudiwa.


"Nataka niwaahidi tutaimaliza miradi yote iliyopo kama ilivyopangwa , lakini pamoja na hayo kuna miradi ambayo inakwenda moja kwa moja kwa wananchi ikiwemo miradi ya elimu ,afya, barabara, umeme na maji,.Nawahakikishia tena tutakwenda kuitekeleza kama Ilani ya uchaguzi inavyosema.


"Nyuma huko tulikuwa tunatekeleza Ilani kupitia misaada ya wahisani lakini sasa wahisani wamebadilika badala ya kutoa hisani wanakuja tufanye biashara halafu tugawane faida ,hivyo faida tunayoipata na kodi tunayokusanya ndio tunafanya maendeleo. Ndugu zangu kwenye bajeti iliyopita tuliweka tozo kwenye mambo ya fedha za mitandao haya, yamepigiwa kelele sana , nimesikia , nimekaa na watalaam tumepunguza kwa asilia 30 ya tozo hizo.


"Lakini nataka kuwaambia tozo zitakuwepo na sitaki kuwaficha , kwasababu tozo zile ambazo tumekusanya kwa ile miezi miwili tuliyoanza nayo tumekusanya zaidi ya Sh.bilioni 60 na fedha hizo zimepelekwa kujenga vtuo 220 vya afya , hivyo tunajenga wenyewe na ndio siasa yetu ya Tanzania, tunajitegemea wenyewe,"amesema Rais Samia.

Amefafanua kuwa lengo la Watanzania kufanya maendeleo kwasababu wafadhili wanaposaidia wanaweka na masharti yao, hivyo fedha zinazokusanywa na Serikali ndizo hizo zinakwenda kufanya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.

"Kama mnavyojua Januari mwakani kuna wimbi kubwa la watoto wanaotaka kujiunga na elimu ya sekondari lakini pia watoto wapya wanaoingia darasa la kwanza,hatuna wa kutujengea madarasa bali sisi wenyewe, fedha tutakazozikusanya Septemba na Oktoba tunakwenda kujenga madarasa zaidi ya 500 ili watoto wetu wakute madarasa yako tayari,"amesema.

Aidha amesema pamoja na yote yanayofanyika , wanadamu hawaachi kusema."Ukifanya watasema na usipofanya watasema , bora tufanye waseme wakione kuliko kutofanya kwa kuogopa maneno yao, si ndio?Lakini wanasema kelele za mlango hazimuachishi mwenye nyumba kulala kwasababu ameshazizoea, vyovyote itakavyokuwa kusemwa kupo.

"Lakini tuangalie tunakwenda wapi, tunakusanya fedha kwa ajili gani? Maendeleo yakionekana ndugu zangu msichoke, sisi ndio watanzania tunawajengea na watoto wetu wa kitanzania lakini mengine tunajingea wenyewe kizazi kilichopo na kizazi kijacho.

"Yaliyosemwa na Meya wa Kinondoni na Mbunge wa Kawe kuwa kuwa kuna mabilioni yameteletwa hizo fedha tunazikusanya wenyewe kupitia tozo zetu, misaada ya wahisani siku hizi ni michache,"amesema Rais Samia.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Wananchi wa Kijiji cha Tegeta Jijini Dae es salaam, alipokuwa njiani akielekea Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani leo Sept 02,2021 kwa kwa ajili ya kuendelea kurekodi kipindi maarufu cha Royal Tour kitakachotangaza Utalii, Biashara na Uwekezaji Nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Wananchi wa Kijiji cha Zinga Bagamoyo alipokuwa njiani akielekea Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani leo Sept 02,2021 kwa kwa ajili ya kuendelea kurekodi kipindi maarufu cha Royal Tour kitakachotangaza Utalii, Biashara na Uwekezaji Nchini. PICHA NA IKULU.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2