Wakulima Wa Tumbaku Tabora Na Kigoma Waipokea Vema Bima Ya Afya Ya NBC. | Tarimo Blog

 WAKULIMA wa zao la tumbaku katika mikoa ya Tabora na Kigoma wameonyesha kuridhishwa na mpango wa bima ya afya kwa wakulima unaojulikana kama Ushirika Afya unaotekelezwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kupitia vyama vikuu vya ushirika katika mikoa hiyo.

Kupitia mpango huo benki hiyo inawajibika kuwasilisha moja kwa moja michango ya bima ya afya kwenda Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa niaba ya wakulima watakaosajiliwa kupitia akaunti ya benki hiyo.

Wakulima hao walielezea hisia hizo kwenye kwenye hafla fupi za utiaji saini hati za makubaliano ya kiutendaji baina ya Benki ya NBC , NHIF na vyama vikuu vya wakulima wa tumbaku katika mikoa hiyo zilizofanyika hivi karibuni na kuhudhuliwa na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali na wakulima wa zao hilo.

Wakizungumza kwenye hafla hizo, Mwenyekiti wa Chama kikuu cha wakulima wa tumbaku kanda ya Magharibi,(WETCU) Bw Hamza Kitunga na Makamu Mwenyekiti wa Chama kikuu cha wakulima wa tumbaku Mkoa wa Kigoma (KTCU) Bw Elikana Bwenda pamoja na kuipongeza Benki ya NBC kwa huduma hiyo sahihi waliiomba benki hiyo pia kuangalia namna ya kuanzisha bima ya mazao ili kuwapa uhakika wa kipato kupitia sekta hiyo muhimu.

“Kwetu sisi wakulima suala zima la afya ndio kitu cha muhimu zaidi. Changamoto kwetu ilikuwa kwamba kipato chetu ni cha msimu na hivyo inatuwia vigumu kumudu gharama za afya kipindi ambacho hatuna hela. Tunawapongeza sana benki ya NBC kwa kutufikiria kwenye hili.’’ Alisema Bw Bwenda

Zaidi pia wakulima hao walitoa wito kwa benki hiyo na NHIF kuwahakikishia uwepo wa huduma bora za afya kupitia mpango huo ili kuepuka malalamiko yanayoweza kujitokeza.’’ aliomba.

Akizungumzia mpango huo, Mkuu wa Kitengo cha wateja wadogo wa Benki ya Taifa ya Biashara, NBC,Raymond Urassa alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa makubaliano yaliyofikiwa wiki chache zilizopita Jijini Dar es salaam baina ya benki hiyo, NHIF na Mrajisi wa vyama vya Ushirika nchini.

“Kimsingi ni kwamba kupitia mpango huu benki ya NBC inatoa mkopo wa huduma hii kwa wakulima ili waweze kupata matibabu kupitia mfuko wa NHIF kwa vile pesa za wakulima huwa ni za msimu wakati changamoto ya dharula za kiafya huwa hazina msimu zinajitokeza wakati wowote,’’ alifafanua.

Kwa mujibu wa Bw Urassa, kupitia mpango huo mkulima atachangiwa kiasi cha sh 76,800 kwa mwaka na ikiwa mkulima ana mwenza wake nae atachangiwa kiasi cha sh 76,800 ambapo pia kila mtoto atachangiwa sh 50,400 kwa mwaka.

“Bima hii itatolewa na NHIF na itapatikana kwenye matawi yote ya NBC nchi nzima hivyo naomba wakulima wachangamkie fursa hii. Kwa upande wetu maofisa wa benki tumejipanga kuwatembelea wakulima wanachama wa ushirika zaidi kuhakikisha wanawapatia habari hii njema kupitia benki ya NBC,’’ aliongeza Bw Urassa.

Kwa upande wao Kaimu meneja wa NHIF mkoa wa Tabora, Bw Dia Liundi pamoja na Kaimu Meneja wa NHIF mkoa wa Kigoma Bw Gwamaka Mwakyome walisema licha ya vipaumbele kadhaa wanavyoweza kupatiwa wakulima ikiwemo mikopo mbalimbali bado wanaweza kushindwa kujikwamua dhidi ya changamoto zinazowakabili iwapo suala la afya kwao halitapatiwa kipaumbele.

“Kipaumbele muhimu kwa wakulima kinatakiwa kuwa afya yao kwanza ndio uwezeshwaji mwingine kama mikopo ya fedha na zana za kilimo ifuate na hii ndio sababu tunawapongeza sana benki ya NBC kwa kuliona hili sababu mkulima hata apatiwe kila kitu kama suala la afya yake halijapatiwa suluhisho bado atakwama tu na hata taasisi zilizomuwezesha pia zitajikuta zinashindwa kufikia malengo ya uwezeshaji huo,’’ alifafanua Bw Mwakyome.

Naye, Bw Cathbert Dongwe, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika wilaya ya Uvinza, Mkoani Kigoma licha ya kuipongeza benki ya NBC pamoja na NHIF kwa mpango huo pia ameshauri mpango huo kuwa endelevu ili uweze kuwasaidia wananchama wa vyama vingine vya ushirika ili nao waweze kunufaika na mpango huo.

Mkuu wa Kitengo cha wateja wadogo wa Benki ya Taifa ya Biashara, NBC, Raymond Urassa (Kushoto) Kaimu Meneja wa (NHIF) mkoa wa Kigoma Bw Gwamaka Mwakyome (Kulia) pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Chama kikuu cha wakulima wa tumbaku Mkoa wa Kigoma (KTCU) Bw Elikana Bwenda (Katikati) wakionesha mikataba ya ushirikiano baina ya taasisi zao kwenye mpango wa bima ya afya kwa wakulima unaotekelezwa na benki hiyo kwa kushirikiana na NHIF kupitia vyama vikuu  vya  ushirika  katika mikoa mbalimbali  wakati hafla fupi za utiaji saini hati za makubaliano hayo iliyofanyika mkoani humo hivi karibuni.


Mkuu wa Kitengo cha wateja wadogo wa Benki ya Taifa ya Biashara, NBC, Raymond Urassa (Kulia) na Makamu Mwenyekiti wa Chama kikuu cha wakulima wa tumbaku Mkoa wa Kigoma (KTCU) Bw Elikana Bwenda wakibadilishana hati ya makubaliano ya kiutendaji kwenye mpango wa bima ya afya kwa wakulima unaotekelezwa na benki hiyo kwa kushirikiana na NHIF kupitia vyama vikuu  vya  ushirika  katika mikoa mbalimbali nchini wakati hafla fupi za utiaji saini hati za makubaliano hayo iliyofanyika mkoani humo hivi karibuni.


Mkuu wa Kitengo cha wateja wadogo wa Benki ya Taifa ya Biashara, NBC, Raymond Urassa (wa pili kushoto -  walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi pamoja na maofisa  wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Chama kikuu cha wakulima wa tumbaku Mkoa wa Kigoma (KTCU) na wakulima wa tumbaku mkoa wa Kigoma.


Mkuu wa Kitengo cha wateja wadogo wa Benki ya Taifa ya Biashara, NBC, Raymond Urassa (Kushoto) na Mwenyekiti wa Chama kikuu cha wakulima wa tumbaku kanda ya Magharibi,(WETCU) Bw Hamza Kitunga wakibadilishana hati ya makubaliano ya kiutendaji kwenye mpango wa bima ya afya kwa wakulima unaotekelezwa na benki hiyo kwa kushirikiana na NHIF kupitia vyama vikuu  vya  ushirika  katika mikoa mbalimbali nchini wakati hafla fupi za utiaji saini hati za makubaliano hayo iliyofanyika mkoani humo hivi karibuni


Kaimu meneja wa NHIF mkoa wa Tabora, Bw Dia Liundi  (kulia) na na Kaimu Meneja wa (NHIF) mkoa wa Kigoma Bw Gwamaka Mwakyome (Kulia) pamoja Mwenyekiti wa Chama kikuu cha wakulima wa tumbaku kanda ya Magharibi,(WETCU) Bw Hamza Kitunga wakionesha mikataba ya ushirikiano baina ya taasisi zao kwenye mpango wa bima ya afya kwa wakulima unaotekelezwa na benki hiyo kwa kushirikiana na NHIF kupitia vyama vikuu  vya  ushirika  katika mikoa mbalimbali  nchini.

Mwenyekiti wa Chama kikuu cha wakulima wa tumbaku kanda ya Magharibi,(WETCU) Bw Hamza Kitunga akizungumza kwenye hafla hiyo.


Mkuu wa Kitengo cha wateja wadogo wa Benki ya Taifa ya Biashara, NBC, Raymond Urassa (Kushoto-walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi pamoja na maofisa  wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Chama kikuu cha wakulima wa tumbaku kanda ya Magharibi (WETCU) na wakulima wa tumbaku mkoa wa Tabora.




Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2