Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akisalimiana na wananchi wa Wilaya ya Bunda wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mara.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Nassari, akizungumza jambo mbele ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati Waziri huyo alipowasili wilayani hapo kukagua ujenzi wa barabara ya Nyamuswa – Bulamba (km 56.4), mkoani Mara.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akimsikiliza mwananchi wa Wilaya ya Bunda wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mara.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa mwananchi wa Wilaya ya Bunda wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mara
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mara Mhandisi Vedastus Maribe, akimuonesha Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, hatua za ujenzi wa barabara Makutano – Sanzate (km 51) kwa kiwango cha lami, mkoani humo.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Nyamuswa – Bulamba (km 56.4) inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Mara.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Makutano – Sanzate (km 51), inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Mara. Ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 91.
PICHA NA WUU
…………………………………………………………..
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Bunda waliopisha ujenzi wa barabara ya Nyamuswa – Bulamba (km 56.4) kwa kiwango cha lami, kulipwa fidia zao kiasi cha shilingi zaidi ya bilioni mbili (2).
Prof. Mbarawa amezungumza hayo mara baada ya kuwasili wilayani hapo, mkoani Mara na kukutana na baadhi wa wananchi ambao bado hawajalipwa fidia zao na kusisitiza kuwa Serikali inatambua jambo hilo na itawalipa wale wote wanaostahili kwa mujibu wa sheria.
“Serikali yenu ni sikivu hivyo fedha zitaletwa hapa na wananchi watalipwa fidia zao ili mkandarasi aendelee na kazi zake bila ya kusimama”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amemtaka wasimamizi wa mradi huo kumsimamia mkandarasi anayejenga barabara hiyo ili kupata barabara yenye viwango na itakayodumu kipindi kirefu.
“Hatutaki barabara hii baada ya miaka miwili mitatu ianze kuharibika, na jibu lake ni moja tu kuwa waadilifu, kuwa wazalendo na kutumia muda mwingi kuisimamia barabara hii kwa weledi”, amefafanua Prof. Mbarawa.
Aidha, Prof. Mbarawa amesikitishwa na tabia za baadhi ya wafanyakazi katika mradi huo kujihusisha na vitendo vya wizi wa mafuta, saluji na vifaa vya ujenzi na kusema kwamba wanarudisha kasi ya maendeleo ya mradi huo na kuelekeza vyombo vya ulinzi kuendelea kuwafuatilia watu hao na kuchukua hatua za kisheria kwa wale watakaobainika.
“Vijana mkipata fursa ya kufanya kazi katika miradi ni heshima hivyo kujihusisha na vitendo vya wizi ni kuhujumu mradi na mfahamu kuwa hamumuibii mkandarasi bali mnaiibia Serikali na wananchi kwasababu vifaa hivyo vimenunuliwa kwa fedha za walipa kodi”, amesema Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Nassari, amemueleza Waziri kuwa mpaka sasa watu wanane (8), wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma hizo na wakati wowote watafikishwa mahakani.
Akiwasilisha taarifa ya mradi, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mara Mhandisi Vedastus Maribe, amemueleza Waziri huyo kuwa ujenzi wa barabara hiyo unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 46.5, gharama za Mhandisi Mshauri ni kiasi cha shilingi Bilioni 2.337 na mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Agosti, 2022.
Mradi wa barabara ya Nyamuswa – Bulamba (km 56.4) inayojengwa kwa kiwango lami ni kiungo muhimu kwani inaiunganisha Wilaya ya Bunda, Serengeti na Butiama pia inaunganisha Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Mikoa ya Kaskazini pamoja na Kisiwa vya Ukerewe.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa, amekagua ujenzi wa jengo la Ofisi la Halmashauri ya wilaya ya Butiama na kumuagiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kukamilisha ujenzi wa jengo hilo mapema mwanzoni mwa mwaka ujao ili waweze kutumia jengo hilo.
“Jengo hili lilisimama muda mrefu lakini sasa fedha zinakuja kwa wakati na kazi zinaendelea hivyo TBA malizeni haraka ili wafanyakazi na waweze kuhamia hapa kuendelea na majukumu yao kiurahisi”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri Mbarawa yupo mkoani Mara kwa ziara ya siku mbili ya kukagua utekelezaji wa miradi inayoendelea kutekelezwa na Wizara yake.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment