Gekul: Michezo ina mchango mkubwa katika kuongeza ufahamu wa masomo | Tarimo Blog

 Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akifungua Mashindano ya michezo mbalimbali ya Vyuo Vikuu nchini kwa mwaka 2021 chini ya Chama cha Michezo ya Vyuo Vikuu Tanzania (TUSA) ambayo yanafanyika kwa siku saba kuanzia Desemba 14, 2021 katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
Msanii wa muziki wa Singeli, Sholo Mwamba akitumbuiza wakati wa ufunguzi wa Mashindano ya michezo ya Vyuo Vikuu nchini kwa mwaka 2021 chini ya Chama cha Michezo ya Vyuo Vikuu Tanzania (TUSA) ambayo yanafanyika kwa siku saba kuanzia Desemba 14, 2021 katika Chuo Kikuu cha Dodoma.

Baadhi ya wanamichezo kutoka vyuo mbalimbali wakiwa katika hafla ya ufunguzi wa Mashindano ya michezo ya Vyuo Vikuu nchini kwa mwaka 2021 chini ya Chama cha Michezo ya Vyuo Vikuu Tanzania (TUSA) ambayo yanafanyika kwa siku saba kuanzia Desemba 14, 2021 katika Chuo Kikuu cha Dodoma.


Na Eleuteri Mangi, WUSM, Deodoma
NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul ametoa rai kwa vyuo vikuu vyote ambavyo ni wanachama wa Chama cha Michezo ya Vyuo Vikuu Tanzania (TUSA) kuleta wanafunzi wao kushiriki katika mashindano yajayo kwa kuwa michezo ina mchango mkubwa katika kuongeza ufahamu wa masomo.

Naibu Waziri Gekul ametoa rai hiyo Desemba 14, 2021 jijini Dodoma wakati anafungua Mashindano ya michezo mbalimbali ya Vyuo Vikuu nchini kwa mwaka 2021 ambayo yatafanyika kwa siku saba katika Chuo Kikuu cha Dodoma.

“Tutambue kuwa michezo ina mchango mkubwa katika kuongeza ufahamu wa masomo na kuchangamsha akili ya mwanafunzi katika kukabiliana na masomo yake. Wanafunzi wanaofanya vizuri darasani na kufanikiwa katika masomo yao na baadae kwenye maisha ni wale wanaoshiriki michezo” amesema Mhe. Gekul.

Ili kufanikisha na kuyafanya mashindano hayo kuwa endelevu, Naibu Waziri Gekul amewahimiza Wakuu wa vyuo kutenga bajeti na kushiriki katika michezo ambapo wataalamu wamethibitisha kuwa “akili yenye afya iko kwenye mwili wenye afya” na kuongeza kuwa michezo ina nafasi ya pekee katika maisha ya kila mwanachuo na kuwasisitiza wanachuo kuitumia michezo hiyo vizuri ili kuzidi kuboresha afya na akili za wanamichezo ambayo itaboresha ufaulu wao katika vyuo wanavyosoma.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mhe. Gekul amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Jemedari wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ipo mstari wa mbele katika kuhakikisha michezo inaendelezwa nchini na kuwanufaisha Watanzania kwa kusimamia sekta ya michezo kwa karibu zaidi.

Aidha, Naibu Waziri amesema kuwa suala la michezo nchini siyo la hiyari, bali dira ya Serikali imelenga kuhakikisha kila mtu anashiriki michezo na Rais Mhe. Samia amekuwa mahiri kuonesha njia kwa utayari wa Serikali anayoiongoza kuweka mkazo kwa kurudisha michezo ya Shule za Msingi (UMITASHUMTA), Shule za Sekondari (UMISSETA) pamoja na Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) ambayo imefanyika kwa mafanikio makubwa mwaka 2021.

Ili kuwa na usimamizi thabiti wa michezo nchini, Serikali imetenga fedha katika bajeti ya mwaka 2021/2022 ambayo imepitishwa na Bunge kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Michezo hatua ambayo inasaidia watu kujenga afya zao, kuimarisha muungano kwa pande zote mbili na itasaidia kupunguza bajeti ya vifaa tiba kwa watu kufanya mazoezi zaidi kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Gekul amewataka viongozi wa vyama vya michezo na vilabu vya michezo watumie fursa ya mashindano hayo ya vyuo vikuu ili waweze kujionea vipaji vya wanamichezo kutoka vyuo mbalimbali wanaoshiriki michezo hiyo na kuwasajili kwenye vilabu vyao ambayo itakuwa ni fursa kwa vijana kupata ajira kutokana na vipaji walivyonavyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Michezo ya Vyuo Vikuu Tanzania (TUSA) Bw. Winston Mdegela ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wanaoendelea kuupata kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuwapa miongozo katika suala la michezo hatua ambayo imewasaidia kushiriki mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mwenyekiti huyo amesema Shirikisho pia linawaandaa wanamichezo kwa michezo ya Afrika Mashariki (EAUG), Michezo ya Afrika (FASU) na Michezo ya Dunia (FISU) ambapo mwaka 2022 shirikisho hilo litashiriki Mshaindano ya Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika nchini Uganda.

Naye Kaimu Mkamu Mkuu wa Chuo cha UDOM Prof. Tenge Albino amesema mbali na vyuo vikuu kutekeleza majukumu matatu ambayo ni kufundisha, kufanya utafiti na kutoa ushauri amesisitiza kuwa afya ya akili hujengwa na mwili wenye afya njema na kuongeza kuw michezo inatengeneza vijana kufanyakazi kwa pamoja.

Zaidi ya hayo, Prof. Tenge Albino amesema Cho cha UDOM kimefanya michezo kuwa sehemu ya maisha ya wanafunzi na watumishi wao ambapo pia wameanzisha dawati maalum la michezo chuoni hapo.

Jumla ya vyuo 20 vinashiriki mashindano hayo licha ya TUSA kuwa na wanachama zaidi ya vyuo vikuu 45. Vyuo vinavyoshiriki mashindano hayo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo Kikuu cha Waislam Morogoro, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE), Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala na Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa.

Vyuo vingine vinavyoshiriki mashindano hayo ni Chuo Kikuu cha Arusha, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Zanzibar, Chuo Kikuu cha Iringa, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo cha Kikuu cha Sayansi na Technologia cha Nelson Mandela Arusha.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2