Meneja wa TARURA, Mkoa wa Dar es salaam Eng. Geofrey Mkinga akitoa maelekezo juu ya mfumo wa kielitroniki wa ukusanyaji ushuru wa maegesho unavyofanya kazi leo kwenye mkutano na kamati ya siasa ya Halmashauli Kuu ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba(kushoto) akizungumza na waandishi wa bahari wati wa mkutano na kamati ya siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Dar es Salaam. Picha na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)
*Kate Kamba aipongeza TARURA kwa kufanya kazi kwa uadilifu
MFUMO mpya wa kidigitali wa ukusanyaji wa malipo ya ushuru wa maegesho ulioanza Desemba Mosi mwaka huu umeanza kwa mafanikio makubwa kufuatia makusanyo kufikia milioni 32 hadi 36 kwa siku huku mategemeo zaidi ya kukusanya mapato yakitarajiwa kuongezeka.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao maalumu kilichowakutanisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA,) na viongozi wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM,) Mkoa wa Dar es Salaam Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Dar es Salam Eng. Geofrey Mkinga amesema mfumo huo mpya wa kusanyaji mapato ni muhimu katika kuzuia kuvuja kwa mapato na hiyo imedhihirika baada ya kuanza kwa kutumika kwa mfumo huo ambapo mapato yanayokusanywa yanaonekana na kufikia shilingi milioni 32 hadi 36 kwa siku kuanzia Desemba Mosi mwaka huu.
Mkinga amesema kuwa hadi sasa wameyafikia makundi mbalimbali na kutoa elimu juu ya mfumo huo wa ukusanyaji wa mapato na kukutana na viongozi hao wa Chama tawala ni muhimu kwa kuwa wapo karibu na wananchi na kupitia kikao hicho ni mwanzo wa wakushiriki vikao mbalimbali vya CCM kutoa elimu.
Amesema, katika mfumo huo wa kidigitali mtumiaji wa maegesho anapaswa kulipa ushuru wa maegesho kidigitali baada ya kupatiwa namba ya malipo (control number,) ambapo atatumia kumbukumbu namba hiyo kulipia huduma hiyo ya maegesho kwa kutumia mtandao wowote wa simu au benki za NMB na CRDB au kupitia mawakala wa huduma za fedha.
Kuhusiana na faini Mkinga amesema kuwa mtumiaji wa huduma hiyo atakumbushwa mara mbili na akishindwa kulipa huduma hiyo atatakiwa kulipa ushuru wa maegesho pamoja na faini ya shilingi 10,000, na kueleza kuwa madeni ya nyuma kabla ya kusitishwa kwa mfumo huo yapo na hayafutwa.
Vilevile amewataka watoa huduma za maegesho wapatao 900 kutotoa lugha chafu kwa wateja na Wakala hiyo kupitia wazabuni watawaondoa kazini wote watakaobainika kukiuka taratibu za ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kate Kamba amesema mapato yanayokusanywa na Wakala hiyo ni katika kuendeleza taifa kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara na hospitali.
''Tumeona mfumo ulivyo rafiki kwa maisha yetu ya kitanzania na fedha zote zinaingia katika mapato ya Serikali na zitatumika kwa manufaa ya Watanzania, nawapongeza TARURA kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria.'' Amesema.
Aidha ameiagiza Wakala hiyo kuufanyia kazi mtandao wa barabara Mkoa wa Dar es Salaam ambao asilimia 55 za mtandao wa barabara hizo hazina hali nzuri na kuwataka kushiriki vikao mbalimbali vya chama ili waweze kutoa elimu zaidi.
Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, mtumiaji wa maegesho anatakiwa kulipa Shilingi 500 kwa saa na Shilingi 2,500 kwa siku.
Mkoa wa Mwanza mtumiaji wa maegesho anatakiwa kulipa Shilingi 500 kwa saa na shilingi 1,500 kwa Siku.
Mkoa wa Iringa mtumiaji wa maegesho anatakiwa kulipa shilingi 300 kwa saa na shilingi 1,000 kwa Siku.
Mkoa wa Dodoma mtumiaji wa maegesho anatakiwa kulipa shilingi 300 kwa saa na shilingi 1,000 kwa siku.
Mkoa wa Singida mtumiaji wa maegesho anatakiwa kulipa shilingi 300 kwa saa na shilingi 1,000 kwa siku.
kamati ya siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Dar es Salaam wakimsikiliza Meneja wa TARURA, Mkoa wa Dar es salaam, Eng. Geofrey Mkinga.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment