MTENDAJI MKUU TEMESA AWAAGIZA WATUMISHI KUFANYIA KAZI CHANGAMOTO | Tarimo Blog

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala wa pili kulia akipokea maelezo kutoka kwa meneja wa Kikosi cha Umeme TEMESA Mhandisi Pongeza Semakuwa kulia wakati alipotembelea Kota za Magomeni jana kukagua mradi huo ambao Kikosi cha Umeme kimeshiriki kusimika mifumo ya Umeme na elektroniki.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala (aliyevaa suti) akipokea maelezo kutoka kwa mmoja wa wasimamizi wa mfumo wa kielektroniki wa kutumia kadi, (N-Card) ambao umesimikwa katika jengo jipya la abiria (waiting lounge) katika kivuko cha Magogoni upande wa Kigamboni. Mashine hizo zinatarajiwa kupunguza tatizo la misururu na misongamano iliyokuwa ikilalamikiwa katika kivuko hicho.


Mashine za kielektroniki zinazotumia mfumo wa kadi, (N-Card) zilizosimikwa katika jengo jipya la abiria (waiting lounge) katika kivuko cha Magogoni upande wa Kigamboni. Mashine hizo zinatarajiwa kupunguza tatizo la misongamano iliyokuwa ikilalamikiwa katika kivuko hicho kwa muda mrefu kwani abiria atakua na uwezo wa kuweka fedha kupitia mifumo ya simu na mawakala na kuepuka kukata tiketi kama ilivyokuwa hapo awali.


Muonekano wa jengo jipya la abiria (waiting lounge) lililojengwa katika kivuko cha Magogoni upande wa Kigamboni. Jengo hilo jipya linatarajiwa kupunguza tatizo la misongamano iliyokuwa ikilalamikiwa katika kivuko hicho kwa muda mrefu kwani lina uwezo wa kuchukua abiria wengi zaidi kwa wakati mmoja.


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala kulia akionyeshwa namna mashine ya kisasa ya kupimia uwiano wa matairi ya gari (wheel balancing machine) inavyofanya kazi wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua karakana ya Mt. Depot iliyopo Keko jijini Dar es Salaam.


Meneja wa Karakana ya TEMESA Vingunguti Mhandisi Liberatus Bikulamchi akisisitiza jambo wakati akitoa taarifa kuhusu kazi zinazofanywa na karakana hiyo kwa Mtendaji Mkuu wakati wa ziara ya Mtendaji kukagua shughuli za utendaji kazi wa karakana hiyo jana.

PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (DAR ES SALAAM)

*****************************

Na. Alfred Mgweno (Dar es Salaam)

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala amemaliza ziara fupi ya kiutendaji Mkoani Dar es Salaam na kuwataka watumishi wa Mkoa huo kuanza mara moja kuzifanyia kazi changamoto ambazo zinatolewa na wateja wanaotumia huduma za Wakala huo.

Akiwa katika ziara hiyo fupi iliyochukua siku mbili, Mtendaji Mkuu alianza kwa kutembelea Ofisi ya Kikosi cha Umeme Keko Darajani jijini Dar es Salaam akiambatanana na Meneja wa kikosi hicho Mhandisi Pongeza Semakuwa ambapo alipata wasaa wa kuzungumza na menejimenti ya kikosi hicho kabla ya kuzungumza na wafanyakazi ambapo aliwapongeza kwa jitihada wanazozifanya na akawataka wafanyakazi hao kuhakikisha huduma wanazotoa zinaendelea kuwa bora ili kuhakikisha wanafungua fursa za maendeleo na mafanikio kwa Taasisi zingine ambazo wanafanya nazo kazi.

‘’Niwapongeze sana, mnaonyesha mnafahamu mnachokifanya na hii ni mojawapo ya timu za TEMESA ambayo imejipanga, inafahamu inafanya nini, kwahiyo hongereni sana’’. Alisema Mtendaji Mkuu ambapo aliwataka watumishi hao kujitafakari na kua chanzo cha utatuzi wa maeneo ya changamoto wanazokumbana nazo na kutosubiri makao makuu kuja na majawabu ya changamoto hizo.

‘’Mimi binafsi lakini pia Serikali kwa ujumla ina matumaini makubwa sana na TEMESA, TEMESA inatazamwa kama kitu kikubwa sana, ina uwezo wa kufanya makubwa zaidi, ya kuwa na tija zaidi, ya kusukuma zaidi maendeleo ya nchi hii kuliko anavyofanya sasa, kwahiyo tunachangamoto ya kuishi mategemeo ya serikali’’, Alimaliza Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa TEMESA itahakikisha yale ambayo yanatekelezeka yanatekelezwa kwa mustakabali wa TEMESA na Taifa kwa ujumla.

Aidha Mtendaji Mkuu pia alipata wasaa wa kutembelea kituo cha Wakala wa Ukodishaji Magari (Government Transport Agency GTA) katika ofisi zake zilizopo Keko Darajani ambapo Meneja wa kituo hicho Mhandisi Margareth Julian alimtembeza na akapata wasaa wa kukagua magari ya kukodisha pamoja na yadi zinazosimamiwa na kituo hicho zilizopo Magomeni Usalama na Temeke jijini Dar es Salaam. Mtendaji Mkuu alimuagiza meneja wa kituo hicho kuhakikisha anasimamia kwa karibu mikataba ya wapangaji wa yadi zinazomilikiwa na Wakala ili Wakala ufaidike na uwepo wa yadi hizo kama mali ya Taasisi huku akisisitiza kila kinachofanyika kifanyike kwa tija na ufanisi wa hali ya juu.

Mtendaji Mkuu pia alitembelea kituo cha Magogoni Kigamboni ambapo alizungumza na watumishi na menejimenti ya kituo hicho. Akizungumza katika kikao na watumishi, Mtendaji Mkuu aliwataka watumishi hao kupokea changamoto wanazozipokea kivukoni hapo na kutengeneza mikakati bora ya kutatua changamoto hizo na malalamiko wanayoyapokea.

‘’Kikubwa ni hicho kwamba japo kutakua na malalamiko, tusirudi nyuma, tusikate tamaa na hata mara moja tusichukie, tuwe tunatatua changamoto, tuimarishe sana utoaji wa elimu, mtu anaweza akapinga tu kitu kwasababu hana elimu ya kutosha kwahiyo tutilie mkazo sana kwenye utoaji wa elimu’’.

Mtendaji Mkuu pia alimuagiza Mkuu wa kivuko Mhandisi Samwel Chibwana kuhakikisha wateja wote ambao wanatumia mfumo mpya wa kadi (N-CARD) kurejeshewa pesa zao ambazo zilizonekana kukatwa kimakosa kwenye mifumo baada ya kutokea hitilafu ya kiufundi kwenye kadi zao siku ya Tarehe 21 Disemba, 2021.

Mtendaji Mkuu alihitimisha ziara yake ya siku mbili kwa kutembelea karakana za MT. Depot pamoja na karakana ya Vingunguti zilizopo jijini Dar es Salaam ambapo ameendelea kusisitiza kwamba TEMESA ni watoa huduma na kazi kubwa ya karakana hizo ni kuhudumia magari ya Serikali huku akiwataka watumishi hao kutambua dhamana kubwa waliyopewa na Serikali kusimamia magari hayo.

‘’Sisi ndio chombo kinachowezesha Serikali ifanye kazi, yale magari ya Serikali ndio yanawezesha shughuli za Serikali kufanyika, yanabeba viongozi wetu, yanabeba nyaraka mbalimbali, tunawezesha mzunguko wa lile gurudumu linaloitwa Serikali kufanya kazi, kwahiyo kumbe sisi ndio chombo kinachowezesha Serikali kufanya kazi, hili ni jambo zito kabisa.’’ Alisema Mtendaji Mkuu na kuwasisitizia kwamba TEMESA inapaswa kutambua kwamba imepewa dhamana ya kuhakikisha Serikali inafanya kazi zake kwa ufanisi na hivyo kama itasuasua na kufanya kinyume, Serikali pia itasuasua katika kufanya kazi zake kwa ufanisi na kwa ukamilifu.

Aidha, katika ziara hiyo, Mtendaji Mkuu pia alipata wasaa wa kutembelea mradi wa nyumba za makazi zilizopo magomeni Kota, mradi ambao Kikosi cha Umeme kimeshiriki kusimika mifumo ya umeme na elektroniki ambapo Meneja wa Kikosi hicho Mhandisi Pongeza Semakuwa alimtembeza katika majengo hayo na kujionea kazi zote za umeme ambazo kikosi cha umeme kimetekeleza katika mradi huo.

Nao mameneja wa vituo hivyo walipata wasaa wa kueleza changamoto ambazo vituo vyao vinakutana nazo katika shughuli zao za kila siku za kiutendaji ambapo Mtendaji Mkuu aliwaahidi kuzifanyia kazi changamoto hizo na kuzitatua kwa wakati ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa uhakika na ubora uliotukuka.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2