NDEJEMBI AONYA VITENDO VYA RUSHWA VINAVYOFANYWA NA WATUMISHI WA IDARA ARDHI MKURANGA | Tarimo Blog


NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi ameonya vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga.

Akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga katika kikao kazi chake na watumishi hao, Ndejembi amewataka kujirekebisha na kufanya kazi kwa uadilifu na weledi ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima inayosababishwa na utendaji kazi wao usioridhisha.

Ameongeza kuwa, watumishi wa Idara hiyo ya ardhi wakiendelea na utamaduni wa kufanya kazi kwa kuweka maslahi binafsi mbele wataipotezea Serikali mapato na kuwanyima haki wananchi wa Mkuranga kupata maendeleo yanayotokana na kodi itayokusanywa na Serikali katika Halmashauri hiyo.

Akisisitiza uadilifu kwa watumishi hao, Mhe.Ndejembi amewataka wabadilike kwa sababu wamekuwa wakilalamikiwa kuwaonea wananchi kwa kuwaomba rushwa na kutowashauri vizuri kwenye masuala yanayohusu umiliki wa ardhi.

“Nimeambiwa hapa Mkuranga hata mimi nikihitaji shamba natakiwa kuwa na kitu kidogo cha kuwapatia watumishi wa Idara ya ardhi ambao wameweka maslahi yao binafsi mbele, na wala sitaki kumtaja mtu mmoja mmoja hapa zaidi ya kuwasisitiza mbadilike”, Ndejembi amefafanua.

Kuhusiana na migogoro inayoibuka Naibu Waziri Ndejembi amewataka Watumishi wa Idara hiyo kuwa watatuzi wa migogoro badala ya kuwa chanzo cha migogoro.

Ndejembi amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wa Halmashauri hiyo, ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya  wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Bi. Jessy Mpangala akiwasilisha changamoto ya kiutumishi inayomkabili kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao wilayani Mkuranga chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2