Na Mwandishi Wetu, Dar Es Saalam
KATIBU wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema Mwenyekiti wa CCM Rais Samia Suluhu Hassan, ameelekeza kuhakikisha Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT), inaimarika zaidi na kutatua changamoto zake.
Shaka aliyasema hayo leo baada ya kuwatembelea watumishi wa bendi hiyo yenye makazi yake Mwananyamala, jijini Dar es Salaam.
Amesema katika hatua za kutekeleza agizo hilo, Chama kitatua changamoto kadhaa zinazoikabili bendi hiyo ambazo ya namna moja zinachangia kukwamisha mafanikio ya utendaji wake huku akieleza hatua hiyo inalenga kuiimarisha TOT ili iendane na ukomavu na uimara wa CCM.
"Chama kitahakikisha TOT inaMmarika zaidi na kuzitatua changamoto zote zinazoikabili kwa nguvu zote ili bendi hii iendane na ukomavu na uimara wa Chama Cha Mapinduzi wakati tukiazimisha miaka 45 ya kuzaliwa CCM mwakani 2022,"amesema.
Aidha, Shaka amesisitiza watumishi wa TOT kujianda vyema kuelekea maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM, ambapo sherehe zake zitafanyika Februari 5, mwakani.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wote wa TOT, Mkurugenzi Mkuu wa bendi hiyo, Gasper Tumaini alisema uamuzi wa Katibu wa Shaka kuwatembelea, kuzungumza nao na kuwasikiliza umewajengea ari na matumaini makubwa ya kuimarishwa zaidi kwa bendi yao na kutekeleza majukumu yao katika mazingira mazuri zaidi kama ilivyokua dhamira ya kuanzishwa kwake.
Tumaini amemwomba Shaka kufikisha salamu za TOT za mshikamano kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia ya kwamba wanaridhishwa na namna anayoiongoza nchi, hivyo wapo pamoja naye.
Bendi ya TOT ilianzishwa mwaka 1992 na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa lengo la kuleta hamasa ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi.
Februari 5, mwaka 2022 CCM, itaadhimisha miaka 45 tangu kuanzishwa kwake Februari 5, mwaka 1975 baada ya kuunganishwa kwa vyama vya ASP na TANU.
Awali akitangaza maadhimisho hayo mapema mwezi huu, Shaka alisema yatakuwa ya aina yake yakipambwa na matukio mbalimbali.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment