Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma yaanza kuifasiri Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995. | Tarimo Blog

Katibu – Idara ya Ukuzaji Maadili, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Waziri Kipacha (katikati) waliokaa akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa Sekretarieti ya Maadili wanaoshiriki kazi ya kutafsiri Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa lugha ya Kiswahili inayofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema mjini Morogoro.Katibu – Idara ya Ukuzaji Maadili, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Waziri Kipacha (katikati) akifungua kikao kazi cha Maafisa wa Sekretarieti ya Maadili Pamoja na Maafisa kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu kazi ya kutafsiri Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa lugha ya Kiswahili katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema mjini Morogoro, tarehe 27 Desemba, 2021. Wengine kutoka kushoto kwake ni Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria Bi Emma J. Gelani na Katibu Msaidizi – Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Mashariki Bw. Hendry Sawe.

 


SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeanza kutekeleza kwa vitendo takwa la kisheria la kuifasiri Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa lugha ya Kiswahili linalotokana na marekebisho kwenye kifungu cha 84(1) na (2) cha Sheria ya Tafsiri za Sheria (Interpretation of Laws Act). Kazi hiyo inayofanywa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Edema, mjini Morogoro kuanzia tarehe 27 – 31 Desemba, 2021.

Akifungua kikao kazi hicho kwa niaba ya Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi, Katibu – Idara ya Ukuzaji Maadili Bw. Waziri Kipacha alisema kuwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura ya 398 ilitungwa kwa lugha ya kingereza na hapakuwa na nakala rasmi iliyo kwenye lugha ya Kiswahili na hata iliyopo haikupitia utaratibu rasmi unaotamabulika.

Kwa mujibu wa Bw. Kipacha, mwaka huu yamefanyika marekebisho kwenye kifungu cha 84(1) na (2) cha Sheria ya Tafsiri za Sheria (Interpretation of Laws Act), Sura ya 1, kupitia kifungu cha 4 cha the Written Laws (Miscellaneous Amendments) Act, Na. 1 ya 2021 na kuagiza kuwa lugha ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitakuwa ni Kiswahili pamoja na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo kwa sasa zipo kwa lugha ya Kingereza zitafasiriwa kwa lugha ya Kiswahili.

Bw. Kipacha aliendelea kubainisha kuwa kutokana na marekebisho hayo kuweka takwa la kufasiri Sheria zote kwenye lugha ya Kiswahili ikaonekana ni vema kufanya kazi hii ya ufasiri wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma sasa kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza kupitia Mradi wa kuzijengea uwezo Taasisi katika kupambana na rushwa nchini Tanzania.

Bw. Kipacha alitumia fursa hiyo kuwataka washiriki wa kazi hiyo ambao wengi wao ni wanataaluma ya sheria kwa ngazi ya shahada na kuendelea kutumia taaluma zao za sheria na kuwatumia vizuri Maafisa kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Kurugenzi ya Uandishi wa Sheria ili waweze kupata kitu kizuri.

“Nawakumbusha kuwa kazi hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Mapambano dhidi ya Rushwa, awamu ya III (NACSAP-III) hivyo ni sehemu ya kipimo kwa Taasisi yetu katika utekelezaji wa mapango huo na baadae tutatolea taarifa ya utekelezaji kwenye mamlaka husika” alifafanua Bw. Kipacha.

Uwepo wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa lugha ya Kiswahili itawasaidia wadau wake hususani wananchi wa kawaida kuifahamu Sheria hii kwa lugha wanayoifahamu hivyo kuisaidia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kusimamia utekelezwaji wake.




Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2