Na John Walter-Manyara
Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Manyara limetoa elimu ya matumizi sahihi ya umeme kwa wajasiriamali baada ya kuwatembelea kwenye sehemu zao za Biashara katika wilaya zote za mkoa huo.
Hayo yameelezwa na Afisa Mkuu Masoko Bi. Monica Massawe kwa kushirikiana na Mhandisi kutoka Kitengo cha Uwekezaji Ndugu Josephat Marandu pamoja na Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Bi. Marcia Simfukwe katika vikao walivyofanya na wamiliki na waendeshaji Mashine zinazotumia Umeme.
Shirika hilo kupitia Kitengo cha Masoko limesema limeona ni bora kutoa elimu hiyo ya matumizi bora na sahihi ya umeme kwa waendeshaji wa Mashine mbalimbali ikiwemo Mashine za kusaga na kukoboa, kukamua mafuta ya kupikia, mashine za mbao, gereji, viwanda vya uzalishaji vidogo vidogo pamoja na wachimbaji na wachakataji wa madini Mkoani Manyara ili wajue matumizi sahihi ya nishati ya umeme.
Wameeleza kuwa elimu hiyo itawasaidia kujua namna sahihi ya kuitumia nishati hiyo na kuepusha malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwao juu ya gharama za umeme na hatari zake.
Wakiwa katika karakana kwenye gereji mbalimbali na viwandani, wamesisitiza wamiliki na waendesha mitambo hiyo kuhakikisha wanatumia Mashine za kisasa na zilizo bora katika uzalishaji pamoja na kuzingatia uunganishaji wa mitambo ulio sahihi pamoja na ufuataji wa Kanuni za matumizi ya umeme zitakazozuia upotevu wa umeme.
Elimu hii imetolewa katika Wilaya za Babati, Mbulu, Hanang, Simanjiro pamoja na Mererani.
Mbali na kuwatembelea wafanyabiara hao pia Tanesco walifanikiwa kutoa elimu kwa umma kupitia vipindi kwa njia ya redio ambapo watu walipata nafasi ya kupiga simu na kutua ujumbe kuuliza maswali mbalimbali na kujibiwa na maofisa hao.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment