WANANCHI KATA YA NDURUMA WILAYANI ARUMERU WAIOMBA SERIKALI KUWAJENGEA DARAJA LA MUDA MTO NDURUMA | Tarimo Blog



Na Pamela Mollel,Arumeru

Wananchi wa vijiji 4 vya kata ya Nduruma Wilayani Arumeru wameiomba Serikali kuwapatia daraja la muda kwenye mto Nduruma ambao umekuwa tishio kila ifikapo msimu wa mvua kwa mafuriko na kukata mawasiliano

Ombi hilo lilitolewa hivi karibuni mbele ya Mkurugenzi wa wa halmashauri ya Wilaya ya Arusha ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa madarasa,Vyoo vya wanafunzi wa kike pamoja na mradi wa uvunaji maji ya mvua uliofadhiliwa na shirika lisilokuwa la kuserikali Ndoto in Action katika shule ya msingi Marurani

Mwenyekiti wa kijiji hicho Jacob Mollel alisema kuwa moja ya changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni mafuriko ya mto Nduruma hasa kipindi cha masika inakata mawasiliano kati ya kijiji cha marurani na Nduruma ambapo ndipo wanapata huduma za kiafya na usafiri kwenda Arusha mjini

"Wakinamama wajawazito wanajifungulia njiani kutokana na mafuriko hayo ya mvua"alisema Mollel

Aliiomba Serikali iwasaidie daraja la muda ili kuokoa kina mama wanaojifungulia njiani pamoja na wanafunzi wa maeneo hayo kukosa vipindi kutokana na changamoto ya kushindwa kufika shuleni


Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Arusha Wilayani Arumeru Suleimani Msumi alisema kuwa watafika katika eneo hilo na kuona ni kwa namna gani wataweka daraja la muda

Msumi aliipongeza Shirika la Ndoto in action kwa kazi kubwa wanayofanya katika mashule kwa kuwezesha miradi mbalimbali yenye lengo la kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi

Mkurugenzi wa shirika la Ndoto in Action Hussein Salim alisema lengo la taasisi hiyo ni kuona shule ina miundombinu rafiki na wezeshi ambayo itaweza kusaidia wanafunzi wanapokuwa mashuleni waweze kujifunza katika hali ambayo ni rafiki huku ikiwezesha ufaulu wanapokuwa mashuleni

"Sisi kama taasisi tunatarajia tunapofanya kazi mashuleni tunahakikisha madarasa yapo imara na kama ni chakavu tutakarabati "alisema Salim


Aidha alisema miradi waliozindua katika shule hiyo imegharimu zaidi ya shiliingi Milioni Mia Moja,miradi hiyo ni uvunaji wa maji ya mvua matenki 8 ya lita elfu 500,ujenzi wa vyoo kumi vya wasichana na chumba maalumu kitakachowezesha mabinti kujisaidia wanapokuwa katika kipindi cha hedhi pamoja na ujenzi wa vyumba 4 vya madarasa

Mwalimu Mkuu katika shule hiyo Elisante Mollel alisema miradi hiyo itasaidia kupunguza mrundikano wa wanafunzi madarasani kwa kuwa kabla ya mradi huo shule ilikuwa na uhitaji wa 14 hivyo upatikanaji wa madarasa 4 utasaidia upungufu wa vyumba vya madarasa shuleni

Shule ya msingi Marurani ilianza rasmi mwaka 1975 na inajumla ya wanafunzi 406,waalimu 7 na upande wa taaluma imekuwa ikipanda mwaka hadi mwaka

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Arusha Wilayani  Arumeru  Suleimani Msumi  akizindua ujenzi wa vyumba 4 vya madarasa katika shule ya msingi Marurani iliyofadhiliwa na Shirika  la Ndoto in Action,kulia ni mkurugenzi wa  shirika hilo Hussein  Salim akishuhudia uzinduzi huo

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Marurani
Muonekano wa jengo la choo cha wasichana lililofadhiliwa na shirika  hilo
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Arusha DC Suleimani Msumi akinawa mikono mara baada ya kuzindua mradi wa uvunaji maji katika shule hiyo
Moja ya darasa lililojengwa na shirika la Ndoto in Action
Mtendaji wa  kijiji cha Marurani Jacob Mollel  akizungumza  na waandishi wa habari juu ya changamoto  ya mto Nduruma
Choo cha wasichana  kabla hakijakarabatiwa
Mkurugenzi  wa shirika la Ndoto in Action Hussein Salim akitoa maelezo kwa mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Arusha DC Suleimani Msumi kulia
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Marurani Elisante Mollel  akisoma risala kwa mgeni rasmi

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2