Na Mwandishi Wetu, Dubai
WAKATI Maonesho ya Kimtaifa maarufu kama Expo Dubai 2020 yakiendelea Jijini Dubai, Banda la Tanzania limeendelea kutumia maonesho hayo kunadi fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zilizopo nchini.
Makundi ya wawekezaji na wafanyabiashara wa kada tofauti wamekuwa wakifika katika banda hilo kwa lengo la kuuliza maswali mbalimbali ambapo wamekuwa wakijibu kwa ufasaha huku zikitumika mbinu kadhaa kuhawahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Katika banda la Tanzania pamoja na wawekezaji pia baadhi ya viongozi na wafanyabiashara wamefika na kupatiwa taarifa kuhusu fursa za uwekezaji; sababu za kuwekeza Tanzania , na namna ambavyo wawekezaji wanavyosaidiwa kuanzisha uwekezaji wao nchini ndani ya muda mfupi na kwa gharama nafuu kupitia mfumo wa Huduma za Mahala Pamoja (One Stop Facilitation Centre) kwenye Ofisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Kwa mujibu wa Maofisa waliopo katika Banda la Tanzania kwenye maonesho hayo wameiambia Michuzi Blog kwamba miongoni mwa mambo wanayoulizwa ni aina ya vivutio vya uwekezaji anavyopata mwekezaji na kufafanuliwa kwamba vivutio vinavyotolewa ni vivutio vya uwekezaji vya kikodi na visivyo vya kikodi.
Aidha imeelezwa pia kwamba wadau wenye nia ya kuwekeza Tanzania wamehimizwa kwamba Kituo cha Uwekezaji Tanzania ndiyo mlango wa kwanza kwa mwekezaji na kitawasaidia kupata ardhi ya uwekezaji, leseni,vibali na idhini mbalimbali zinazotakiwa kuanzisha mradi husika.
Wawekezaji wamekaribishwa kuwekeza Tanzania huku wakihakikishiwa kwamba tayari nchi ina miundombinu ya kuwezesha uwekezaji katika sekta mbalimbali. Miundombinu hiyo ni kama maji, umeme, barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na masoko.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment