Watendaji wa sekta wameaswa kuheshimu sheria za utumishi | Tarimo Blog

Hemed akizungumza katika kongamano la nne la kitaifa la utawla bora lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni ambapo alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuacha kutumia mitandao ya kijamii katika kuwachonganisha wananchi na viongozi.
Muwakilishi wa Kituo cha huduma za sheria (LSF) Bw. Deo Bwire akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais juu ya mafanikio yaliofikiwa na LSF ambapo kimefanikiwa kutoa ruzuku kwa Zaidi ya taasisi 200 za Kisheria Nchi nzima.

WATENDAJI wa sekta mbalimbali wametakiwa kuheshimu sheria za utumishi wa umma katika majukumu yao ili kusimamia misingi ya utawala bora.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo wakati akilifungua kongamano la nne la kitaifa la utawala bora lililofanyika katika ukumbi wa Shekh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Alisema ni vyema watendaji kuachana na vitendo vyenye mnasaba wa uvunjaji wa misingi ya utawala bora ikiwemo rushwa, kutokuwa na mwenendo mzuri wa kimaadili , na kuwataka kufuata sheria za utumishi wa umma na sheria zote zilizowekwa na Serikali kupitia katiba.

Alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watumishi kukiuka sheria na taratibu za kiutumishi ikiwemo kuchelewa kuingia kazini, kuondoka kabla ya muda pamoja na udanganyifu jambo ambalo linazorotesha utendaji wa kazi katika ofisi za umma.

Mhe. Hemed alieleza kuwa suala la utawala bora ni suala linalozingatia misingi ya ufanisi wenye tija, na kueleza kuwa ni matarajio kongamano hilo litaamsha ari na hamasa ya kuimarisha utawala bora ndani ya Zanzibar.

‘’Napenda nikukumbusheni kuhusu suala la utawala bora, kwamba ni suala linalozingatia misnigi ya ufanisi na tija, utawala wa sheria na haki za binadamu , ushirikishwaji , kuzuwia rushwa, kuzingatia maadili na uadilifu , uwajibikaji na uwazi na kuzingatia matakwa ya wananchi’’ Amesema Mhe. Hemed.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali imeanzisha taasisi mbali mbali kama vile Tume ya maadili ya viongozi wa umma, mamlaka ya kuzuwia rushwa na uhujumu wa uchumi na nyenginezo kwa ajuli ya kuimarisha na kusimamia maadili ya viongozi na wa utumishi wa umma lengo likiwa ni kuimarisha utawala bora.

Mhe. Hemed alifafanua kwamba, taasisi na makundi mbali mbali nchini zinawajibu katika kuheshimu na kuimarisha maadili, haki za bindamu , uwajibikaji na kupiga rushwa, ili kusimamia haki na wajibu kwa wananchi wanaotaka huduma.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema katika kupunguza vitendo vya rushwa, Serikai imeweka mfumo wa malipo kwa njia ya Elektroniki kwa taasisi za Serikali ili kuimarisha uwajibikaji na kuzuwia vitendo vya rushwa visiendelee katika taasisi za umma.

Mhe.hemed aliwataka viongozi waliopewa dhamana kujitahidi kuwa wabunifu katika kupanga na kutekeleza mipango iliyopo ili kuendeleza jitihada zinazochukuliwa na Serikali.

Mhe. Hemed alitumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kuisadia Serikali katika kusimamia misingi ya utawala bora, na kuwatahadharisha wananchi wanaotumia mitandao ya kijamii kwa kuisema vibaya Serikali kutokana na kueka mbele maslahi yao binafsi.

Kwa upande wake Waziri Nchi Afisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na utawala bora Mhe. Haroun Ali Suleiman aliwakumbusha viongozi kusimamia haki za wafanyakazi, pamoja na kuhakikisha wananchi hawadhulumiwi katika maeneo yao ya kazi.

Mhe. Haroun alisema (LSF) imekuwa kichecheo cha utawala bora katika katika utendaji na usimamizi wa masuala ya sheria ambapo alitumia fursa hiyo kuiomba taaisi ya LSF kuisaidia mahakama ili kesi ziweze kuhukumiwa haraka na kuondokana na mrindikano wa kesi.

Nae Katibu Mkuu Afisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na Utawala Bora Seif Shaaban alisema Wizara imekwishakamilisha mapitio ya hali halisi ya utawala bora, ambapo kwa sasa wapo katika hatua ya kupitia sera ya utawala bora.

Kwa upande wake muwakiishi wa kituo cha huduma za sheria (LSF) Deo Bwire alisema kipaumbele cha taasisi hiyo ni kuongeza mashirikiano kwa taasisi kusimamia haki, sheria na utawala bora pamoja na kupiga vita ruhswa, ambapo hadi sasa wanafanya kazi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Mafunzo na Mahakama kwa kuhakikisha wanasimamia vyema utekelezaji wa misingi ya utawala bora.

Kauli mbiu ya kongamano hilo inasema “Piga vita rushwa, heshimu haki za binadamu, uadilifu na uwajibikaji kwa maendeleo ya uchumi endelevu”

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2