*Majaliwa aipongeza kwa kuibuka na makombe 7 kwenye mashindano hayo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameipongeza timu ya Bunge baada ya kuibuka na makombe saba katika michezo mbalimbali kwenye Mashindano ya 11 ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyomalizika hivi karibuni jijini Arusha.
Amesema kuwa wabunge hao wamefanya kazi kubwa ya kuipambania Tanzania na Bunge la Tanzania mbele ya nchi zote za Afrika Mashariki. “Ile kazi nzuri mliyoifanya ya kuipambania nchi, mmeleta zawadi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania na wabunge wengine.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumamosi, Desemba 18, 2021) alipozipokea timu mbalimbali za Bunge katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma. Timu ya Bunge imeshinda makombe kwenye michezo ya mpira wa miguu, pete, wavu kwa wanawake na wanaume, kikapu kwa wanawake na wanaume na mchezo wa kuvuta kamba wanaume.
“Ninaleta kwenu salamu za faraja kutoka kwa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa mliyoifanya, na faraja nyingine ni kuona wachezaji wengi mmerudi salama, nidhamu mlioinesha katika mashindano haya imetujengea heshima kubwa”
Amesema kuwa ushindi wa timu hiyo unapeleka ujumbe kwenye timu nyingine zinazoshiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa kushiriki kikamilifu na kuiwakilisha vyema nchi kwenye mashindano husika ikiwemo kuwa na matamanio ya kurudi na makombe.
“Tunatakiwa tuandike historia ya ubora wa michezo nchini ambapo tunaona kwasasa kila sekta inaenda vizuri na hata ile inayokuwa inakufa tunaifufua na hii pia imepelekea kupata heshima na sifa ya kupeleka timu yetu ya watu wenye ulemavu kwenye mashindano ya kombe la dunia”
Kwa upange wake, Spika wa Bunge Mheshimiwa Job Ndugai, amesema kupitia michezo hiyo wametoa somo kwa timu nyingine zilizoshiriki michezo hiyo na hatimaye kulipa heshima bunge “ahadi yetu sisi tutasimama na ninyi kwenye maandalizi zaidi mwakani na ninawapongeza sana kwa nidhamu mlioionesha hata mlipochokozwa hamkuchokozeka”
Naye, Meneja wa Timu hiyo Seif Gulamali amemshukuru Spika Ndugai kwa kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri kwenye mashindano hayo jambo lililowezesha kuibua morali na hatimaye kuibuka na makombe “kwa niaba ya wabunge wote tunaomba usituchoke sisi ni vijana wako, endelea kutulea, tunapoleta maombi yetu basi uyapokee kwa mikono miwili.”
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment