MAAMUZI YA HAKIMU MRISHO KIKWETE | Tarimo Blog

 

Adeladius Makwega,DODOMA.

Siku ya Januari 29, 2022 nilitumia muda wangu mwingi kukamilisha matini zangu juu ya Kabila la Wajita na hususani utani baina yake katika familia, koo na koo na hata Wajita na makabila wengine.

Katika kazi hizo nilipata maswali mengi ambayo niliyajibu. Mojawapo ya swali lilikuwa Je kuna utani wa koo na koo na familia na familia? Wengi walikuwa wakifahamu utani ule wa kabila moja na lingine tu.

Niliweza kuwajibu kuwa utani upo katika madaraja makubwa matatu, Utani wa ndani ya familia mathalani babu na mjukuu, bibi na mjukuu wake na hata mtoto wa mjomba na shangazi, hii pia inabadilika kulingana na kabila moja kwenda lingine.

Hatua ya pili ya utani ni kati ya ukoo na ukoo, katika kabila moja kuna koo nyingi kwa hiyo hilo ni jambo la kawaida ukoo huu kuutania ukoo ule na hatua ya tatu ni ule utani wa kabila na kabila, huu unafahamika na wengi.

Kwa kuwa Wakwere ni watani na Wapogoro leo ngoja nitoe mfano hai wao. Kulifafanua hilo kwa kina leo natoa mfano hai ambapo watani walitaniana hadi mmoja kuvunjika meno na shauri kwenda mahakamani.

Kulingana na mila za Kikwere pale panapofanyika ndoa na Wagongo(watani) huwa hakuna posa inayotolewa. Kama mtu atadiriki kulipa posa hiyo basi wahusika hao wanafariki hapo hapo au katika ndoa yao hawawezi kupata watoto. Wagongo wanachotakiwa kufanya basi hapo hutoa kijichi au jani hiyo huwa ni mahari. Siyo pesa au kitu kingine chochote cha thamani.

Kulingana na mila za Wakwere ndoa hii ina heshima kubwa kuliko ndoa zote japokuwa sasa pesa imetamalaki sana lakini baadhi ya Wakwere bado wanatumia njia hii ya kuoana kwa kuwa ni mila yao.

Mwaka 1944 katika eneo moja la Msoga kulikuwa na ngoma ya Wavibindu, ndugu mmoja ambaye alikuwa akifahamika kama Mbode Lunema ambaye alikuwa Mvibindu ambayo ni ukoo jamii ya Wakwere ndiye alikuwa ni Koro ( kiongozi wa familia ambaye anasimamia mambo yote ya koo chini ya chifu.) huyu alikuwa ni mjomba wa Chifu.

Mbode Lunema (Kolo) alikuwepo katika ngoma hiyo huku akiwa na kitanda chake kizuri amekaa akifuatilia mirindimo ya ngoma hiyo ya nduguze. Jamaa huyu alikuwa amevalia kilemba maridadi kichwani mwake.

Huku Ngoma hiyo ikiendelea Makinamsisi alifika katika ngoma hiyo. Makinamsisi alimfuta Mbode Lunema (Kolo ) na kumwambia maneno haya.

“Kwa kuwa nimefika mimi mmiliki wa ngoma hii ambaye pia ni mjomba wako unawajibu wa kunipisha katika kitanda hicho. Lazima ujifunze tabia njema, ondoa Kilemba chako! Kila unaponiona mimi unawajibu wa kukivua hicho kilemba! Eboo! Wewe ni mjinga! na (Hashakumu si matusi) hanithi wee! Kuwa hapa kama mkuu wa ngoma hii. Ondoka hapo mbwa we!.”

Mbode Lunema (Kolo) alichukizwa mno na akakasilika vibaya, Mkinamsisi hakujali hilo aliendelea kuyatoa matusi kadhaa kwa kwa Kolo .Isitoshe Mkinamsisi alimfuata Kolo na kutaka kumvua kilemba. Mbode Lunema alibaki kukaa katika kitanda chake kile alichokaa. Ugomvi huo uliendelea, mwanakwetu kumbuka kuwa na ngoma inaendelea.

Kwa kuwa Mbode Lunema alikuwa mzee na hakuwa na nguvu za kutosha aliangushwa chini na kuvunjika meno yake mawili. Jambo hli lilimuabisha mno Mbode Lunema

Alikata shauri na kulipeleka mahakamani shauri dhidi ya mgongo (mtani) wake. Shauri hilo lilibisha hodi katika mahakama ya mwanzo ya Msoga na mara baada ya kusajiliwa, Makinamsisi alliitwa mahakamani na kuitikia wito huo.

Mbele ya hakimu wa mahakama ya mwanzo Msoga ambye jina lake nitakutajia baadaye, shauri lilikuwa hivi;

“Makinamsisi alisema kuwa Mbode Lunema (Kolo) nadhani amechanganyikiwa, meno yake mawili yametoka kwa sababu ya ujinga wake, hakuwa na  heshima na mimi, ambaye ni mgongo wake, ambaye ni mkuu wake na anawajibu wa kunitumikia, mimi nazaliwa kwa ukoo wa Wamsisi na yeye ni Mkinavibindu,sisi ni watani. Yeye ni mtumwa kwangu, ninaweza kumfanyia lolote kulingana na ugongo wetu. Hapa mheshimiwa hakimu, Mbode Lunema anakupotezea muda tu.”

Mwanakwetu kumbuka kuwa kesi hipo mezani kwa hakimu na Makinamsisi ana kesi ya jinai ya kumfanyia mtu fujo na kumpiga hadi kumtoa meno mawili.

Mheshimiwa hakimu huyu wa Mahakama ya Mwanzo Msoga alirejea sheria za kimila za Wakwere na utamaduni wao namna wanavyoishi. Aliposikiliza pande zote mbili na mashahidi waliokuwepo katika ngoma hiyo alitoa nafasi ya wazee wa baraza ambao walikuwa wakifahamu sheria hizo za kimila.

Kwa bahati nzuri hakimu naye alikuwa akifahamu sheria za kimila za Wakwere kulingana na umri wake jina lake alikuwa Mrisho Kikwete.

Hakimu Kikwete aliwaomba wazee wa baraza waseme na walipomaliza aliamua kulitupilia mbali shauri hilo. Kwa kuwa huo ulikuwa utani wa koo na koo za wakwere, shida ilikuwa ni kwa yule aliyetaniwa tu, ndugu Mbone Lunema.

Mwanakwetu, haya yote yanathibitishwa na Profesa Tigiti Sengo katika mojawapo ya maandiko yake ya Utani kwa kabila la Wakwere ambapo mwaka 1972 alitembelea mahakama ya mwanzo Msoga-Bagamoyo(Chalinze sasa) na kukutana na Hakimu wa mahakama hiyo ndugu Bakari Mgweno, ambaye alishuhudia kesi hiyo iliyoamuliwa na hakimu Mrisho Kikwete mwaka 1944, Tigiti Sengo (wakati huo nalikuwa ni mwanafunzi wa UDSM) alipatiwa na nakala ya hukumu hiyo.

 

Mwanakwetu naweka kalamu yangu chini kwa swali la leo, Je hakimu Mrisho Kikwete ni  baba wa mheshimiwa akaya Kikwete?

 

Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 


 

 

 

 

 


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2