Na Mwandishi wetu, Karatu
OFISA ardhi Mteule wa Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha, Faraji Rushagama, amechukua fomu na kujitosa kuwania nafasi ya uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rushagama ambaye ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) amesema ameamua kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya spika ili mhimili wa kutunga sheria uwe na ladha tofauti.
Rushagama ametoa msimamo huo wakati wa mahojiano na waandishi wa habari jana juu ya kinyang'anyio cha uspika.
Amesema ameamua kutia nia kwa kuwa kiti hicho kipo wazi na katiba inampa fursa hiyo kwa mujibu wa ibara ya 82 ambapo Spika siyo lazima awe mbunge bali anaweza kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.
"Nafikiri naona kabisa kwamba kwa sasa Spika ajaye anapaswa asiwe mbunge ili watanzania wapate ladha tofauti," amesema Rushagama.
Amesema pamoja na kuwa na vigezo Nchi inahitaji kiongozi shupavu wa kuongoza mhimili wa kutunga sheria.
"Kwa sasa Bunge linahitaji Spika ajaye anatakiwa asitumie ubabe bali weledi ili kusaidia wananchi na kulinda maslahi ya Taifa," amesema.
Mwanasheria huyo anayewania kiti cha uspika amesema anatokana na wananchi wa kawaida wasio wabunge hivyo anaamini atafanya vizuri zaidi kwa kuwa hataegemea upande wowote ambao unalenga ujimbo.
Kuhusu watu wanahoji kuwa yeye ni mdogo amesema hayo ni mambo ya kizamani kwa kuwa Bunge halibebebwi na mbeleko kusema kwamba litamlemea.
"Kikubwa sana hapa ni miongozo, kanuni na taratibu za uendeshaji kuzingatiwa lakini pia busara kwa maslahi ya watanzania zinapoonekana zipewe nafasi ," amesema.
Alipoulizwa kuhusu sheria zinazopigiwa kelele ikiwemo sheria ya ndoa na sheria ya huduma za habari amesema utungaji wa sheria una taratibu zake.
Wakili huyo ameeleza kuwa sheria zikilalamikiwa ni kwamba wakati zinatungwa zilikuwa zinafaa ila kwa sasa kama hazifai atatoa ushauri na kufuata kanuni kwa serikali inayoleta miswaada Bungeni ili zitungwe sheria nzuri.
Vile vile amesema hakuna sababu ya kung'ang'ana na sheria ambazo ni kandamizi kwa serikali na wananchi.
Je Rushagama ni nani? huyu ni wakili ambaye ni mzaliwa wa wilaya ya Karagwe mkoa wa Kagera, Ofisa ardhi Mteule wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.
Elimu yake ana stashahada ya sheria kutoka chuo kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, stashahada ya uzamili katika usuluhishi na upatanishi (ISW), Sheria kwa vitendo (LST) mutawaliwa.
Anayo pia shahada ya uzamili akibobea katika sheria za kimataifa na kazi kutoka Chuo kikuu Huria Tanzania (OUT) na anasomea sheria ya uzamivu katika sheria za kimataifa chuo kikuu ambacho hakukitaja.
Diwani wa kata ya Qurus Danstan Panga amesema kada huyo ataweza kuongoza Bunge kwa kuwa ni mwanasheria ambaye ameishafanya kazi za kijamii.
Panga amesema kuwa kada huyo anaaminika sana kwa Karatu ana misimamo hivyo ataendesha Bunge kwa uwazi na haki.
Diwani huyo amedai ataweza kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan na ataondoa sheria kandamizi ambazo zinaitesa serikali na wananchi.
"Tutakuwa na imani na Bunge na tutaitangazia dunia kuwa wananchi wanaweza kuongoza mhimili huu," amesema Panga.
Amesema kuwa ni mtetezi wa haki hivyo anaomba wanaoteua wamwamini kwakuwa anatoka Karatu sehemu yenye siasa za kimkakati kwa muda mrefu.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment