Na Eleuteri Mangi, WUSM- Moshi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Tamasha la Utamaduni la Mkoa wa Kilimanjaro ambalo litafanyika Januari 22, 2022 katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika kilichopo Manispaa ya Moshi.
Taarifa ya Tamasha hilo imetolewa na Umoja wa Machifu wa mkoa huo chini ya Mkuu wa Chifu nchini ambaye pia ni Mkuu wa Chifu wa Mkoa wa Kilimanjaro Chifu Frank Mareale wa himaya ya Marangu katika katika kikao cha Machifu wa mkoa huo kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini Moshi.
“Ni heshima mkoa wetu kuwa wa kwanza kutekeleza agizo la Chifu Mkuu Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ambalo alilitoa mkoani Mwanza tarehe 8 Septemba 2021 katika Tamasha la Utamaduni ambalo aliagiza mikoa yote nchini kuendesha matamasha ya utamaduni kwa lengo la kuelimisha jamii na kuendeleza utamaduni wetu” amesema Chifu Mareale.
Akizungumzia Tamasha hilo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emmanuel Temu amesema mkoa wa Kilimanjaro umeitikia agizo la Rais Mhe. Samia Suluhu ambapo alitoa maelekezo kwa mikoa yote nchini kufanya matamasha ya kiutamaduni katika maeneo yao.
“Tumeanza safari kubwa ya kuimarisha utamaduni wa mkoa wa Kilimanjaro, Matamasha haya yatainua na kuibua hazina kubwa ya kiutamaduni miongoni mwa jamii iliyopo nchi nzima itakayotumika kwa manufaa ya tmtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla na yataleta” amesema Dkt. Temu.
Ili kulifanya tamasha hilo kuwa la jamii nzima, Dkt. Temu amesema kuwa vijana wahamasishwe kushiriki hatua itakayowasaidia kujifunza na kuonja uthamani wa utamaduni kama anavyoothamini Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anaonesha kwa vitendo kwa kushiriki matamasha ya utamaduni nchini kudhihirisha kuwa utamaduni ni utajiri ambao unaweza kuwasaidia watu wote kuanzia vijana hadi wazee kama chanzo cha ajira kupitia utalii wa kiutamaduni katika maeneo mbalimbali nchini.
Dkt. Temu amesema kuwa kwa mujibu wa Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997, wananchi wanawajibu wa kuendeleza utamaduni na Serikali ikiwa na wajibu wa kusimamia mila na desturi na kuongeza kuwa tamasha la Kilimanjaro linatarajiwa kuwa na vionjo ambavyo vitakuwa na mvuto kwa watanzania kwa kuonesha vyakula vya asili vya kutosha, mavazi ya asili, ngoma za asili pamoja na historia ya makabila ya Wachaga, wapare, wamasai na wagwemo na kuwa tamasha la mfano ambalo litatoa hamasa kwa mikoa mingine kuandaa matamasha ya kiutamaduni katika mikoa yao.
Tamasha la Kilimanjaro ni utekelezaji wa Sera ya Utamaduni ambayo imetoa mwelekeo wa maendeleo ya utamaduni kwa kuainisha jinsi shughuli za utamaduni zitakavyoendeshwa na kusimamiwa pamoja na kuweka wazi majukumu ya Serikali, wananchi kwa makundi au mmoja mmoja na sekta binafsi ili kufanikisha lengo la kuhifadhi na kuuenzi utamaduni wetu.
Mkuu wa Chifu nchini ambaye pia ni Mkuu wa Chifu wa Mkoa wa Kilimanjaro Chifu Frank Mareale (kulia) wa himaya ya Marangu akimsikiliza Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni nchini kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emmanuel Temu (kushoto) kabla ya kuanza kikao cha Machifu wa mkoa wa Kilimanjaro kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini Moshi.
Chifu Godfriend Kileo (kushoto) wa Siha akichangia mada wakati wa kikao cha Machifu wa mkoa wa Kilimanjaro kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini Moshi. Kulia ni Mkuu wa Chifu nchini ambaye pia ni Mkuu wa Chifu wa Mkoa wa Kilimanjaro Chifu Frank Mareale wa himaya ya Marangu
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emmanuel Temu (katikati) akichangia mada wakati wa kikao cha Machifu wa mkoa wa Kilimanjaro kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini Moshi. Kushoto ni Alaigwanani Gabriel Mollel kutoka wilaya ya Hai na kulia ni Chifu Jabiri Msofe kutoka wilaya ya Mwanga.
Mkuu wa Chifu nchini ambaye pia ni Mkuu wa Chifu wa Mkoa wa Kilimanjaro Chifu Frank Mareale (Katikati) wa himaya ya Marangu akimsikiliza Mratibu wa Tamasha la Utamaduni Mkoa wa Kilimanjaro Joseph Msele wakati wa kikao cha Machifu wa mkoa wa Kilimanjaro kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini Moshi. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika tamasha hilo litakalofanyika Januari 22, 2022 katika Manispaa ya Moshi.
Mkuu wa Chifu nchini ambaye pia ni Mkuu wa Chifu wa Mkoa wa Kilimanjaro Chifu Frank Mareale wa himaya ya Marangu akisoma gazeti ikiwa ni njia mojawapo ya upashanaji habari kujua yanayojiri ndani na nje ya nchi.
Machifu wa Mkoa wa Kilimanjaro wakiwa kwenye kikao mwishoni mwa wiki cha maandalizi ya Tamasha la Utamaduni la mkoa huo ambapo Mgeni Rasmi katika tamasha hilo litafanyika Januari 22, 2022 katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Manispaa ya Moshi anatarajiwa kuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Machifu wa Mkoa wa Kilimanjaro wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kikao cha maandalizi ya Tamasha la Utamaduni la mkoa huo mwishoni mwa wiki ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika tamasha hilo litafanyika Januari 22, 2022 katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika kilichopo Manispaa ya Moshi.
(Picha na Eleuteri Mangi, WUSM- Moshi)
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment