SERIKALI YAIPA DAWASA KAZI MPYA KISARAWE | Tarimo Blog


WIZARA ya maji imetangaza kuongeza eneo la huduma kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ili kusogeza huduma ya maji kwa kutekeleza mradi wa maji Kazimzumbwi hadi Masaki kwenye kata ya Kazimzumbwi Wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani.

Uamuzi huo umekuja mara baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dr Suleiman Jafo ambae ni Mbunge wa jimbo la Kisarawe kutoa ombi kwa Wizara kuipa DAWASA jukumu la kupeleka maji kwenye mradi huo utakaonufaisha kata za Kazimzumbwi, Masaki, Msimbu, Kibuta na Marumbo wenye urefu wa Kilomita 192 baada ya RUWASA kushindwa kutekeleza kutokana na ufinyu wa bajeti.

Akitangaza uamuzi huo kwa mujibu wa Sheria ya Maji sura namba tano, Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso (Mb) amewataka DAWASA kufikisha huduma ya maji kwenye eneo hilo kutoka kwenye mradi wa maji Kibamba - Kisarawe.

"DAWASA mkae na wataalamu wa RUWASA ili mje na utaratibu wa namna ya kutekeleza mradi huu," amesema Mhe Aweso akiwa kwenye ziara ya kutembelea mradi wa maji Kibamba - Kisarawe.

"Kata za Kazimzumbwi, Masaki, Msimbu, Kibuta na Marumbo ni maeneo yenye changamoto ya maji kwa muda mrefu na ambalo halijapata utatuzi," amelezaa Waziri Jafo.

Waziri Jafo ameipongeza DAWASA kwa kazi kubwa ya kutekeleza mradi wa maji Kibamba - Kisarawe kwa bilioni 10.6 kwa Wilaya ya Kisarawe, hii imesaidia sana kuimarisha upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Kisarawe.

Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja ameeleza kupokea jukumu hilo na kusema mradi huo utatekelezwa ndani ya muda muafaka ili wananchi wa kata za Kazimzumbwi, Masaki, Msimbu, Kibuta na Marumbo waweze kunufaika na mradi.

Mradi wa maji Kibamba - Kisarawe unazalisha lita milioni 6 za maji kwa siku ambayo ni zaidi ya mahitaji ya maji kwa Wilaya ya Kisarawe ambayo ni lita milioni 1.2.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akimkabidhi afisa mtendaji Mkuu wa Dawasa mradi mpya wa Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja mara baada ya Ruwasa kushindwa kutekeleza mradi huo
Mbunge wa Jimbo la Kisarawe Dkt. Suleimani Jafo akiweleza Wananchi wa Kisarawe kuhusu  kufikishiwa mtandao wa maji
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Kisarawe Kijiji Cha Sungwi namna serikali ilivyoamua kuhamisha mradi wa Maji kutoka Ruwasa kwenda Dawasa
Mtendaji wa Ruwasa Wilaya ya Kisarawe akitoa maelezo kuhusu mtandao wa maji utakavyo tekelezwa



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2