WAKANDARASI MIRADI YA MAJI RUVUMA WATAKIWA KUKAMILISHA MIRADI KWA WAKATI | Tarimo Blog


Na Muhidin Amri,Nyasa

WAKANDARASI wa miradi ya maji mkoani Ruvuma, wametakiwa kutekeleza miradi waliyopewa kwa uadilifu na ubora wa hali ya juu ili miradi hiyo iweze kumaliza kero ya upatikanji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, katika Hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa wilaya ya Nyasa Kanali Raban Thomas, wakati wa utiaji saini wa mikataba mitano ya ujenzi wa miradi ya maji inayotarajiwa kutekelezwa katika wilaya nne kati ya tano za mkoa huo.

Jenerali Ibuge, amewataka wakandarasi hao kutumia vizuri nafasi hiyo kuonyesha uwezo wao kwa kujenga miradi yenye ubora ili kuipa serikali imani na kuendelea kuwaamini wakandarasi wa ndani kwa kuwapa miradi mingine.

Mkuu wa mkoa, amewaagiza wahandisi wa miradi ya maji mkoani humo,kusimamia vizuri kazi hiyo ili iwe na ubora na kuhakikisha wakandarasi wanalipwa kwa wakati mara baada ya kukamilisha kazi walizopewa.

Brigedia Jenerali Ibuge,ametaka kuwepo ushirikishwaji wa viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa kwenye miradi hiyo, kwani jambo hilo linaweza kuleta tija katika utekelezaji wa miradi ya maji na miradi mingine ya maendeleo mkoani humo.

Ametoa wito kwa wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za wilaya ambazo miradi hiyo inakwenda kutekelezwa,kuwapa ushirikiano wakandarasi hao ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri na kutambulisha miradi hiyo kwa wananchi kwa kuwa wao ndiyo walinzi wanaoishi katika mazingira ya miundombinu hiyo.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki alisema,mikataba hiyo ni muhimu kwa sababu mahitaji ya maji kwa wananchi na ustawi wa nchi yetu ni makubwa na kuwataka wakandarasi kwenda kutekeleza miradi kwa wakati na kulingana mikataba iliyopo.

Amewataka kutanguliza uzalendo, na kutekeleza miradi hiyo kwa weledi wa hali ya juu,ubora unaotakiwa na ilingane na fedha zilizotolewa na Serikali ili kuleta ufanisi na tija kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma ambao baada ya mikataba hiyo wana matarajio makubwa ya kupata maji kwa haraka.


“maana ya ufanisi ni pale mradi unapotekelezwa na kutoa matokeo mazuri na msipofikia ufanisi ni nadra sana kupata matokeo mazuri ya miradi husika”alisema Ndaki.

Meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini Ruwasa mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga alisema, kwa mwaka wa fedha 2021 Ruwasa mkoa wa Ruvuma imetengewa jumla ya Sh.11,914,448,813.00.

Alisema, fedha hizo zinalenga kuhakikisha miradi yote waliyoipanga katika mwaka 2021/2022 inatekelezwa na kutimiza dhamira ya Serikali ya kumtua mama ndoo kichwani.

Kwa mujibu wa Ganshonga,miradi ambayo mikataba yake imesainiwa itagharimu jumla ya Sh.3,806,744,369.18 fedha zilizotolewa na Serikali Kuu kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19 na itatekelezwa kwa siku 120 na miradi itakayotekelezwa kwa vyanzo vingine muda wake ni siku 180.

Alisema,miradi hiyo inakwenda kutekelezwa kutokana na vyanzo mbalimbali vya fedha ambapo miradi 3 ni ya fedha za Mpango wa maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19 na miradi 2 itatekelezwa kwa fedha za vyanzo vingine(NWF,PBR,GoT na PFR).

Alisema,miradi ambayo imepangwa kutekelezwa imegawanyika katika makundi mawili ambayo ni miradi ambayo taratibu za manunuzi zinafanyika ngazi ya Wizara na miradi ambayo taratibu za manunuzi zinafanyika ngazi ya Mkoa.

Ganshonga alisema, miradi yote ilikuwa katika hatua mbalimbali za kukamilisha usanifu na uandaaji wa taarifa na nyaraka za zabuni kabla ya kuitangaza kupitia mfumo wa manunuzi ya umma ili kuwapata wakandarasi wenye sifa na kutekeleza kazi za ujenzi wa miradi hiyo.

Alisema,katika miradi ambayo utaratibu wa manunuzi ulikuwa unafanywa na Ruwasa mkoa,jumla ya miradi 5 kati ya 15 taratibu zake za zimekamilika.

Alisema,Ruwasa mkoa inaendelea kutekeleza miradi mingine 17 ambayo ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji kwa kutumia wataalam wa ndani kwa mfumo wa force Akaunti.
Mkurugenzi wa kampuni ya Jambela Ltd James Mbeya katikati, akitia saini ya mkataba wa ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa  na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) katika wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wakati wa hafla fupi ya kusaini mikataba ya ujenzi wa miradi ya maji mkoani Ruvuma iliyofanyika ofisi ya Mkuu wa wilaya Nyasa,kushoto anayeshuhudia Meneja wa Ruwasa wilaya ya Songea Mhandisi Mathias Charles na kulia msimamizi miradi wa kampuni ya Jambela Mhandisi Daud Bazilio.
Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki akizungumza jana wakati wa utuliaji saini mikataba ya ujenzi wa miradi  maji inayotekelezwa na wakala wa maji  na usafi wa mazingira(Ruwasa)mkoa wa Ruvuma ambapo jumla ya miradi sita inatarajiwa kutekelezwa katika wilaya nne kati ya tano za mkoa huo,katikati mkuu wa wilaya ya Nyasa Kanal Raban Thomas.
Mkuu wa wilaya ya Nyasa Kanal Raban Thomas kushoto,akimpa mkataba wa ujenzi wa miradi ya maji Mkurugenzi wa Kampuni ya Jambela Ltd James Mbeya,wakati wa hafla ya utiaji sani mikataba ya ujenzi wa miradi ya maji katika wilaya nne kati ya tano za mkoa wa Ruvuma inayotekelezwa na wakala wa maji vijijini na usafi wa mazingira(Souwasa)mkoa wa Ruvuma.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2