Na Denis Sinkonde, Songwe
Mkuu wa mkoa wa Songwe Omary Mgumba amesema ili kuondoa kero ya foleni katika mpaka wa Tanzania na Zambia katika mji wa Tunduma Kuna haja wizara ya ujenzi na uchukuzi kutengeneza barabara ya njia nne kutoka Mlowo mpaka Tunduma.
Mgumba ametoa kauli hiyo mapema Leo katika kikao Cha ushauri mkoa wa Songwe(RCC) katika ukumbi wa mkoa huo uliopo Nselewa, baada ya barabara kuu ya kutoka Tanzania kwenda Zambia kuwa na foleni ambayo imeleta adha kubwa magari ya mizigo yaendayo nchi za kusini mwa Afrika(SADC) , mabasi yaendayo mikoani na kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo.
Mgumba amesema foleni hiyo imetokea baada ya kutokea mgomo wa madereva kuanzia Februari 14 mpaka Februari 19 mwaka huu ambao umetatuliwa na viongozi wa pande zote mbili Tanzania na Zambia, hivyo foleni hiyo imetokea baada ya magari yaliyopaki mikoa ya Songwe, Mbeya na NJombe na kuanza kuruhusiwa kuingia mpakani hapo.
"Asilimia 65 ya mizigo inayosafirishwa na malori hayo yanatoka bandari ya Dar es salaam hivyo wizara ya ujenzi na uchukuzi ina haja ya kupanua barabara iwe ya njia nne kutoka Mlowo hadi Tunduma ili kuondoa foleni" alisema Mgumba.
Mgumba amesema foleni hiyo imesababisha abiria wa mabasi na magari yaliyotoka Sumbawanga, Tunduma kwenda Mbeya hadi Dar es salaam kukwama hivyo kuzua tafrani ya usafiri.
Malori yaliyokuwa yanayotoka Tanzania kwenda Nchi za Kusini mwa Afrika yamelundikana na kufunga njia kuanzia Kijiji Cha Chimbuya hadi Tunduma mpakani mwa Zambia kuanzia Februari 22, 2022 mpaka leo Februari 23, 2022.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment